MAMBO FULANI MUHIMU
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIONA watu wanatembea asubuhi au tunapokutana nao
maofisini, ujuwe kuwa si wote wanafurahia uhusiano wao au ndoa kwa wale
waliobarikiwa jambo hilo, zaidi ya maumivu na kilio kila wakati.
Diamond na Wema Sepetu enzi za upendo wao
Wapo watu ambao kila muda wa kurudi majumbani mwao
unapofika, hakika wanatamani wakati urudi nyuma ili waendelee kukaa maofisini
mwao.
Aidha, kwakuwa hilo haliwezekani, basi wanaona suluhu kubwa
ya kutuliza akili zao ni kukimbilia kwenye vijiwe vya kahawa au pombe na kukaa
hadi usiku wa manane.
Haya ni mambo ya ajabu sana. Huwatokea watu wengi katika
uhusiano, hasa wale mapenzi yanayowajia kwa upande wenye karaha na machungu ya
aina yake.
Wapo watu katika mapenzi ni wasumbufu sana. Hao hawataki
kujua kuwa wapenzi wao, wachumba au wana ndoa wao wameamua kutulia na wao.
Kwasababu ya kushindwa kufahamu walau robo ya upendo wa
wenzao, wameamua kufanya vituko, hivyo kuwa njia ya wenzao kutamani kuwa mbali
nao.
Haya si mambo mazuri katika suala zima la uhusiano wa
kimapenzi, hivyo wadau tunatakiwa tulijuwe hilo kwa faida ya wapenzi wetu kwa
ujumla.
Uhusiano ambao hauna maelewano, huo hauwezi kuwa na mashiko
wala kuendelea kuchanua. Tutakuwa na uhusiano wenye mashaka makubwa.
Tutazalisha watu wanaotamani kutoka nje ya ndoa kwasababu
sisi tuliokuwa nao hatuwavutii au hatufanyi mambo ambayo wao yanawafarahisha.
Kwasababu hiyo, ndio maana wapo watu ambao licha ya kujiita
wapo kwenye ndoa, lakini hawajawahi kugusana na wana ndoa wenzao kwa kipindi
hata cha miezi sita kama sio mwaka.
Wana ndoa hao huishi kama mtu na dada yake au mama yake
mkwe. Huyu amelala kule na mwingine yupo upande ule. Tena kama kitanda ni cha
futi sita kuendelea ndio balaa.
Nani amuanze mwenzake. Uchokozi hapo hauruhusiwi. Mmoja
akijitia kukosea na kumgusa mwenzake kwa bahati mbaya, huenda matusi
yakaporomoshwa.
Hayo ni mambo ya kushangaza na kuogopesha kupita kiasi,
maana licha ya watu kuwa kwenye ndoa, lakini hawaishi kama wana ndoa.
Ndio maana hapo mwanzo wa mada hii nilisema kuwa vitanda
vinajua vitu vingi mno vya wanandoa. Huo ndio ukweli wa mambo.
Kuna msomaji wangu mmoja aliandikia meseji kuwa yeye
anateswa na mume wake. Dada huyo akasema ameamua kumuacha kama alivyo.
Kama hivyo ndivyo, ina maana hakuna hata kupeana haki ya
ndoa? Kwa mtindo huo, bado tutaajita ni wana ndoa? Haya ni mambo yaliyoenea kwa
wana ndoa wengi.
Kwa kulijua hilo, nadhani kila mmoja ajaribu kuangalia kwa
wakati gani anatumia kufanikisha ulinzi wa ndoa yake, uchumba au uhusiano wake.
Kila mmoja ajaribu kufumba macho japo kwa dakika moja
kufikiri alipotoka na mtu wake pamoja na kuombea dua uhusiano wake kwa faida ya
mtu wake.
Ushike mkono wa mtu wako. Upeleke mdomoni mwako kwa njia ya
upendo, ukiutaka radhi baada ya kuukosa kwa kipindi ambacho kitendo kama hicho
kukifanya kilikuwa ni agharabu
Katika suala la migogoro ya kimapenzi, wakati mwingine
kunakuwa hakuna sababu inayoonyesha chanzo zaidi ya ujana, utoto na kutokujua
njia nzuri za kulinda uhusiano huo, hivyo naamini ni wakati wetu sasa kulinda,
kuthamini na kuona tuna kila sababu ya kuheshimu watu wetu kwa faida ya
uhusiano wetu na kuacha kasumba zetu.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment