KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha
Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers
kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi
mbili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa
Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile
kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa
Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi
ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure
uwanjani.
Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya
sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji
mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora
iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.
Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome
Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000
kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria
ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani
iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa
kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.
Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa
uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji
imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu
kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.
Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja
la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake
litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za
kinidhamu.
Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza
ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika
kwa mechi za FDL msimu ujao.
No comments:
Post a Comment