1. UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika,
Kufuatia
marekebisho kadhaa ya kanuni hususan zinazolenga kwa sasa Utaratibu wa Kutunga
Sheria kuhusiana na mambo ya fedha, nasi kama Kambi Rasmi ya Upinzani tutafanya
marekebisho katika utaratibu tutakaotumia katika kutoa maoni yetu kwa
Serikali.
Kwa muda mrefu, kufuatia utaratibu wa mfumo wa
bajeti ulivyokuwa huko nyuma, tulitumia muda mwingi kuishauri serikali namna
bora ya kuboresha bajeti na utendaji wake wa kazi. Hata hivyo, kwa bahati mbaya
sana, serikali hii imekuwa siyo sikivu vya kutosha hata kama pale ambapo ushauri
unaotolewa uko wazi kwa masilahi na mustakabali mwema wa Taifa
letu.
Aidha, pale ambapo Serikali imechukua maoni
yetu, mara nyingi imekuwa haina ustaarabu wa kutambua, kukiri na kushukuru
mchango wa Kambi ya Upinzani, bali mbele ya macho ya umma imeendelea kutoa
kebehi kujaribu kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani havina ufumbuzi mbadala
kwa matatizo yanayolikabili Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Tatizo kubwa la Serikali inayoongozwa na CCM ni
kukosa weledi wa kutekeleza kikamilifu vipaumbele vyake pamoja na kuviainisha
kupitia Mpango wake wa miaka 5, bajeti na programu mbalimbali. Hali hii inaweza
kutafsiriwa kama uwezo duni wa kusoma alama za nyakati ikiwemo kubuni na
kusimamia inachokiamini. Ni dhahiri vilevile unapolazimika kufanya jambo
usiloliamini au lisilo kipaumbele chako, bali cha kulazimishwa na mazingira
unatekeleza bila kujua undani wake na hatma yake ni kuharibu zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mtambuka, Mwaka
huu tutajielekeza kuzungumzia mambo makuu machache ambayo sisi tunaamini ni
vipaumbele muhimu ambavyo Waziri Mkuu na wasaidizi wake wanapashwa kuja na
majibu ya kueleweka kwa Watanzania. Aidha, mengine yatawasilishwa kupitia hotuba
zetu mbalimbali katika Wizara husika.
2. TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, NA MCHAKATO
WA KATIBA MPYA NA MSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa
Spika,
Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge lako tukufu
lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Kufuatana malalamiko mengi kuhusu utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria hiyo
na kufuatia vikao kati ya Mheshimiwa Rais na Kamati Maalum ya CHADEMA pamoja na
wadau wengine, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho wakati wa Mkutano wa Sita wa
Bunge hili uliofanyika mwezi Februari mwaka 2012.
Marekebisho hayo yalikuwa ni awamu ya kwanza ya
awamu tatu za marekebisho ya Sheria hiyo kwa mujibu wa makubaliano yetu na
Mheshimiwa Rais. Awamu nyingine mbili za marekebisho zilitarajiwa kukamilika
kabla ya mwisho wa mwaka jana, yaani 2012. Hata hivyo, hadi nasoma maoni haya
leo hii, Sheria ya Marekebisho ya Katiba haijafanyiwa marekebisho mengine
yoyote.
Mheshimiwa Spika,
Mara baada ya marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kupitishwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa
wajumbe na watendaji wakuu wa Tume na Tume yenyewe ilianza kazi mwezi Mei, 2012.
Kwa maana hiyo, hadi kufikia leo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeshafanya kazi
kwa karibu mwaka mmoja.
Kwa masikitiko makubwa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba katika kipindi hiki
mtiririko wa matukio kadhaa ndani na nje ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imethibitisha kwamba haina weledi, dhamira au nia ya kusimamia mchakato huru
usiofungamana na upande wowote.
Katika mwaka wa kwanza wa mchakato wa
upatikanaji Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imethibitisha hofu
tuliyokuwa nayo toka mwanzo kwamba lengo la mchakato wa Katiba Mpya uliowekwa
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni kuhakikisha kwamba mabadiliko
pekee yakayokuwepo ni yale yenye kulinda matakwa ya CCM na Serikali yake au yale
pekee yatakayokuwa na Baraka za “Status Quo”.
Mheshimiwa Spika,
Kwanza, Tume haikuweka utaratibu wowote
madhubuti wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya
ili kuwaandaa wananchi kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha.
Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume ya kupokea maoni ya wananchi, wajumbe wa
Tume walipewa jukumu la kuwaeleza wananchi juu ya Katiba Mpya kwa muda usiozidi
nusu saa!
Kwa kulinganisha, Tume ya Katiba ya Kenya
ilifanya kazi ya kutoa elimu kwa umma kwa nchi nzima kwa muda wa miezi sita
kabla ya kuanza kukusanya maoni ya wananchi wa Kenya juu ya Katiba Mpya. Matokeo
yake ni kwamba mchakato wa Katiba Mpya wa Kenya umeiletea nchi hiyo Katiba Mpya
ya mwaka 2010 ambayo imeanza kudhihirisha ubora wake kwa jinsi ambavyo mambo
yatokanayo na Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa hivi karibuni
yalivyotatuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Pili, muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni
ya wananchi ulikuwa mdogo sana ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa
Watanzania. Katika Majimbo karibu yote ya uchaguzi Tanzania Bara, Tume
iliendesha wastani wa mikutano saba kwa kila jimbo kwa lengo la kukusanya maoni
ya wananchi.
Katika mikutano hiyo wananchi walitakiwa kutoa
maoni yao kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa dakika tano kila mmoja na
mikutano yenyewe ilichukua muda wa masaa matatu ikiwa ni pamoja na muda wa
kutambulishana wajumbe wa Tume na mambo mengine yaliyo nje ya kuchukua maoni ya
wananchi.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba
kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba kwa
waandishi habari tarehe 5 Januari mwaka huu, hadi awamu nne za kukusanya maoni
ya wananchi zinakamilika tarehe 19 Desemba, 2012, Tume ilikwisha kufanya
mikutano 1,776 kwa nchi nzima. Aidha, kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti
Warioba, hadi kufikia kipindi hicho wananchi wapatao 64,737 walikwishatoa maoni
yao kwa kuzungumza wakati wananchi 253,486 walitoa maoni kwa njia ya maandishi,
na wengine 16,261 walitumia njia ya “posta, tovuti ya Tume, mitandao ya kijamii
na ujumbe mfupi wa simu za mkononi....” Kwa hiyo, kwa mujibu wa taarifa hizi za
Mwenyekiti wa Tume, kati ya Watanzania takriban milioni 45, ni Watanzania
334,484 ndio waliotoa maoni juu ya Katiba Mpya hadi kufikia tarehe 4 Januari,
2013. Idadi hii ni sawa na asilimia 0.7 ya Watanzania wote! Na hao ndio
waliotoa maoni yao kwa muda wa dakika tano kila mmoja, wakiwamo waheshimiwa
Wabunge wa Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika, ni wazi, kwa takwimu
hizi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa vyovyote vile, Katiba Mpya
itakayotokana na maoni haya haiwezi kuwa Katiba Mpya ya Watanzania wote.
Utaratibu wa hovyo namna hii utazaa Katiba Mpya ya hovyo!!! Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa hovyo hauwezi kutupatia Katiba
Mpya yenye maridhiano ya kitaifa kwa ajili ya kutatua migogoro mingi ya kisiasa,
kijamii na kidini ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa.
Mheshimiwa Spika,
Tatu, licha ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kutangaza kuwa Tume itakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yake, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kila dalili za Tume kutokuwa huru au kuutafsiri
uhuru vibaya. Kwa mfano, kuna ushahidi kwamba Tume imekuwa na mawasiliano ya
karibu na Serikali na Ofisi ya Rais kwa namna ambayo inaashiria Tume kutokuwa
huru. Ndio maana katika hotuba yake ya kumaliza mwaka uliopita na kufungua Mwaka
Mpya, Rais Jakaya Kikwete alilitangazia taifa ratiba ya kazi za Tume ambayo Tume
yenyewe ilikuwa haijawahi kuitoa hadharani.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alitangaza
sio tu kumalizika kwa awamu za kukusanya maoni ya wananchi, bali pia alitangaza
ratiba ya Tume kuanza kuchukua maoni ya vyama vya siasa, taasisi nyingine na
‘makundi maalum’, tarehe ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya,
Mikutano ya Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba na hata tarehe ya kura
ya maoni na upitishwaji wa kura ya maoni kuihalalisha Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika, Rais asingeweza
kufahamu ratiba hii yote bila kupatiwa taarifa ama na Tume yenyewe ama na
watendaji au watumishi wake au na wajumbe wa Tume. Mbali na taarifa ya kwisha
kwa awamu ya tatu ya zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, taarifa hizi hazikuwa
zimetolewa hadharani na Tume kabla ya hotuba ya Mwaka Mpya ya Rais
Kikwete!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetambua siku
zote kwamba msemaji rasmi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni Mwenyekiti wa Tume
Joseph Warioba. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijawahi kusikia wala kuona
mahali popote ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imempa Rais Kikwete jukumu
la kuwa msemaji wa Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kama Rais
anaweza kupatiwa taarifa za kina namna hiyo kuhusiana na shughuli za Tume, kuna
uhakika gani kwamba yeye au Serikali yake hawatoi kwa Tume maelekezo ya
kichinichini juu ya nini cha kufanya, kwa namna gani na kwa wakati
gani.
Mheshimiwa Spika,
Nne, wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikitoa
taarifa za kina juu ya shughuli zake kwa Rais Kikwete na Serikali yake, Tume
hiyo hiyo imetangaza wazi wazi kwamba haiwajibiki kwa Bunge kuhusu utekelezaji
wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. Zaidi ya kumtuma Naibu Katibu wa Tume,
viongozi wa Tume kama vile Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume
wamekataa kuhudhuria vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili
kuieleza Kamati juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na
Katiba ya Nchi.
Katika hili, Tume imeungwa mkono na Serikali
hiyo hiyo inayoelekea kupata taarifa za kina juu ya utekelezaji wa kazi zake!
Hii ni licha ya kupatiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 za walipa kodi wa
Tanzania zilizoidhinishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya
kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, wakati Tume inaharibu mchakato wa Katiba
Mpya kama tulivyoonyesha hapa, Bunge – kwa kupitia kwa Kamati yake – limezuiliwa
kuhoji shughuli za Tume kwa hoja kwamba Tume iko huru.
Mheshimiwa Spika, hii inaweza kuwa mara
ya kwanza kwa chombo cha umma kinachotumia mabilioni ya fedha za umma
kilichopewa majukumu ya umma na Sheria iliyotungwa na Bunge hili tukufu kukataa
kuwa chini ya usimamizi wa kikatiba wa Bunge (parliamentary
oversight)!
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imesikitishwa sana na kushindwa kwa Kamati husika ya Bunge kudai madaraka yake
ya usimamizi yasipuuzwe na Tume na/au Serikali. Udhaifu huu wa Bunge na Kamati
unaweza kuligharimu Taifa endapo mchakato wa Katiba Mpya utachakachuliwa na
kuliingiza Taifa katika machafuko ya kisiasa, kidini au kijamii.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu juu ya uwajibikaji wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwa matumizi ya mabilioni ya fedha za umma
iliyoyaidhinishiwa mwaka jana na inayoyaomba mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Tano, Tume imetengeneza utaratibu wa mabaraza ya
kikatiba ambao kwa ushahidi wa mwanzo tu unaonyesha kwamba hayo ni mabaraza ya
CCM na sio mabaraza ya katiba ya Watanzania wote. Hili limefanyika kwa
kupitiaMwongozo Kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake,
uliotolewa na Tume mwezi Februari mwaka huu. Kwa mujibu wa Muundo huu, wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watachaguliwa na Kamati za Maendeleo za Kata
(maarufu kama ‘WDC’) baada ya kuwa wamechaguliwa moja kwa moja na wananchi
katika vijiji na mitaa. Wajumbe wa WDC ni Madiwani wa Kata ambao ni Wenyeviti
wake, Watendaji wa Kata ambao ni Makatibu na Wenyeviti wa Vijiji au
Mitaa.
Mheshimiwa Spika, kwa kufuatana na
chaguzi za vijiji na mitaa za mwaka 2009, zaidi ya asilimia 90 ya vijiji na
mitaa inaongozwa na wenyeviti ambao ni wanaCCM. Aidha, kutokana na Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2010, zaidi ya asilimia 80 ya Kata zote nchini zinaongozwa na madiwani
wa CCM. Hawa ndio waliochagua wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba tangu
mwanzoni mwa wiki iliyopita. Matokeo yake, kwa taarifa ilizo nazo Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kutoka sehemu mbali mbali za nchi yetu, kila mahali wagombea
ambao hawakuwa wanaCCM walienguliwa katika ngazi ya uchaguzi wa vijiji au mitaa
au wameenguliwa na WDC baada ya kushinda katika ngazi hizo.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi
kwamba viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa
waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kwamba
wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika chaguzi za
vijiji, mitaa au kata. Mfano mzuri ni wa Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome
aliyeitisha mkutano wa wenyeviti wote wa mitaa ya Musoma Mjini na kuwapa
maelekezo ya kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa wanachama wa CCM hawapati nafasi
katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya au Manispaa hiyo.
Mheshimiwa Spika, licha ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kupatiwa maoni ya wadau kwamba utaratibu huo utaharibu
mchakato wa Katiba Mpya, Tume ilikataa kata kata kuubadilisha Muundo wa Mabaraza
haya. Ni wazi kwamba Tume inafahamu inachokifanya.
Ni wazi vile vile kwamba Tume inafahamu matokeo
ya hicho inachokifanya, yaani kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni
ya wanaCCM. Na wala haihitaji shahada ya uzamivu kufahamu kwamba Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya yenye kutawaliwa kwa kiasi hicho na wanaCCM yatatoa maoni ya
aina gani juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yatakayoijadili. Itakuwa ni Katiba Mpya
kwa jina tu, mambo mengine ya msingi yatabaki vile vile. Kwa maneno mengine,
itakuwa ni Katiba ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile kile.
Mheshimiwa Spika, Uchakachuaji wa
mchakato wa Katiba Mpya wa aina hii ndio ulioiingiza Zimbabwe katika machafuko
makubwa ya kisiasa toka mwaka 1998 na Kenya mwaka 2007/2008. Kwa utaratibu huu
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inaelekea Serikali ya CCM inaelekea kutotaka
kujifunza kutokana na yaliyowakuta jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu wa
Zimbabwe.
Mheshimiwa Spika,
Sita, Serikali imekataa ama imeshindwa kuheshimu
makubaliano iliyofikia na wadau mbali mbali ikiwemo CHADEMA, kufanya marekebisho
zaidi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa sababu hiyo, bado haijulikani
wajumbe mia moja na sitini na sita watakaotokana na taasisi mbali mbali
zilizotajwa na Sheria hiyo watateuliwa kwa utaratibu gani na nani atakayefanya
uteuzi huo.
Vile vile, bado hakuna muafaka juu ya uhalali wa
idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar kushiriki
katika mjadala wa Katiba Mpya kwenye masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania
Bara wakati hakuna mjumbe hata mmoja wa Tanzania Bara anayeweza kushiriki katika
mijadala ya kikatiba inayohusu masuala ya Zanzibar yasiyokuwa Mambo ya
Muungano.
Zaidi ya hayo, bado hakuna majibu
yanayotosheleza yanayompa Rais mamlaka ya kuliitisha upya Bunge Maalum la Katiba
na kulielekeza ‘kuboresha’ masharti ya Katiba Mpya mara baada ya Bunge hilo
kuipitisha. Aidha, haijulikani ni uhalali upi wa kisheria na kikatiba
utakaoiruhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuendesha kura ya maoni ya
kuhalalisha Katiba Mpya kwa sababu Katiba na Sheria za Uchaguzi za sasa
hazitambui wala kuweka utaratibu wa kuendesha kura ya maoni.
Mheshimiwa Spika, kushindwa kwa Serikali
kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya
marekebisho katika maeneo tajwa ni ushahidi wa wazi kwamba Serikali ya CCM haina
nia ya dhati na dhamira safi ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba Mpya
inayoistahili.
Aidha, si nia ya CHADEMA kuendelea kushiriki na
kubariki mchakato huu kama ulivyo sasa kwani ishara zote ziko wazi kuwa Katiba
inayokusudiwa ni ile tu itakayokidhi matakwa ya Wana- CCM na Washirika wake na
hivyo kutokutimiza azma ya kuwa na Katiba itakayoponya majeraha mbalimbali na
kurejesha uzalendo, mshikamano na upendo wa dhati miongoni mwa Watanzania na
kisha mfumo wa Utawala utakaokidhi mahitaji ya wakati.
Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA inatangaza rasmi kwamba: CHADEMA itajitoa ushiriki
wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi
hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, yaani tarehe 30 Aprili,
2013:
- Kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
-
Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:
- Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba;
- Vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara;
- Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni;
- Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba nay a kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni;
3.
ANGUKO LA ELIMU TANZANIA: ANGAMIZO LA KIZAZI NA JANGA LA TAIFA.
Mheshimiwa
Spika,
Nianze
kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa kumnukuu Rais wa 55 wa Marekani, John F.Kennedy
(1917 – 1963);
“Our progress as a nation can be no
swifter than our progress in education. The human mind is our fundamental
resource”
Mheshimiwa Spika,
Siku za karibuni kumekuwepo mjadala mzito sana
kuhusiana na hali ya elimu nchini. Pamekuwepo na malalamiko mengi sana yakiwemo
yaliyomtaka Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa na Naibu wake Mhe Phillip
Mulugo wajiuzulu kama ishara ya uwajibikaji wa kisiasa. Ni dhahiri kuwa elimu
yetu kama Taifa imeporomoka kwa kiasi kikubwa cha sasa kuhatarisha mustakabali
wetu kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja tu
umepita tangu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA itoe
angalizo kali kwa Serikali juu ya kasi kubwa ya kuporokoka kwa Elimu ya Tanzania
na hivyo kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuliepusha Taifa na balaa
hilo. Hata hivyo, Serikali hii ya CCM imeendelea kupuuza ushauri mzuri inayopewa
bure na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na matokeo yake ni kwamba anguko la
mwaka huu ni kubwa kuliko maanguko yote yaliyowahi kutokea katika Historia ya
Tanzania ambapo asilimia 60.6 (240,903) ya wanafunzi waliofanya mtihani wa
kidato cha nne wamepata daraja sifuri na wengine asilimia 26.02 (103,327) daraja
la nne. Jumla ya kufeli huku ni zaidi ya asilimia 86.62 au sawa na
Mheshimiwa Spika, kufuatia kufeli huku
kwa kutisha kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2012, wadau wengi walitaka
baadhi ya viongozi wa sekta ya elimu akiwemo waziri kuwajibika. Ni bahati mbaya
sana kuwa Waziri Mkuu ni mmoja wapo wa viongozi Wakuu aliyestahili kuchukua
hatua za kuwawajibisha wahusika lakini hakufanya hivyo. Badala yake, akakimbilia
kuunda tume ya uchunguzi, ilhali yeye mwenyewe Waziri Mkuu, Waziri wake wa elimu
na serikali yake yote ikijua fika nini kinasababisha kuporomoka kwa elimu yetu.
Yumkini, kama kweli serikali hadi leo haijui sababu ya kuporomoka kwa elimu
yetu, basi haina tena sifa wala weledi wa kusimamia siyo tu elimu, bali maisha
ya kila siku ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kufeli
huku hakuwezi kuchukuliwa kama bahati mbaya hasa ikiwekwa maanani kuwa mserereko
wa watoto wetu kufeli umeshika kasi chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne
hasa kuanzia mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2007, ufaulu wa
vijana wetu wa kidato cha nne ilikuwa (90.3%), 2008 (83.6%), 2009 (72.5%) na
2010 (50.4%). Kufuatia mserereko huu wa kufeli, serikali iliunda timu
iliyoshirikisha wataalam kadhaa kubaini chanzo chake na tiba ya muda mfupi, muda
wa kati na muda mrefu. Timu hii iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Bw. Francis M.
Liboy wa TAMISEMI ilikamilisha ripoti yake mwaka 2011 na kutoa mapendekezo
kadhaa kwa serikali. Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa anaijua ripoti hii
kwani ndiye aliyeandika dibaji yake. (Angalia kiambatanisho A)
Mheshimiwa Spika, mbali na ushauri wetu
wa mara kwa mara, serikali hii imebeza kwa nguvu zote juhudi mbalimbali
zinazofanywa na wadau wengine wenye kuumizwa na kusikitishwa na kuporomoka huku
kwa elimu. Watanzania ni mashahidi namna katika Mkutano wa Kumi wa Bunge, hoja
binafsi ya Mheshimiwa James Mbatia (Mb) kuhusu udhaifu ulioko katika sekta ya
elimu ilivyochukuliwa kimzaha na kutolewa majibu mepesi na Serikali kinyume na
kanuni za bunge na hatimaye kuyazima maazimio ya bunge ya kuinusuru elimu ya
Tanzania yaliyokuwa yamependekezwa katika hoja hiyo. Ni katika mkutano huohuo wa
Bunge ambapo hoja binafsi ya Mheshimiwa Joshua Nassari (Mb) kuhusu Baraza la
Mitihani linavyoathiri elimu ya Tanzania iliondolewa katika orodha ya shughuli
za mkutano wa kumi wa Bunge bila ridhaa ya mtoa hoja kinyume na kanuni ya
58(5).
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali ya
CCM chini ya mwavuli wa wingi wa wabunge wake bungeni, cha kuzivuruga hoja hizi
na hivyo kusababisha maazimio ya bunge juu ya hoja hizi kutotekelezwa ni udhaifu
mkubwa sana kwa chama kinacho tawala cha CCM na Serikali yake na ni ushahidi
uliokamilika kwamba Elimu kwao sio kipaumbele cha taifa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ambayo Elimu
sio kipaumbele chake, haiwafai Watanzania kwa karne hii. Kuendelea kuukumbatia
utawala na aina hii ni kukaribisha maafa yasiyoepukika kwa Taifa. Mbali na
kulisababishia Taifa hili aibu kubwa mbele ya majirani zetu na jamii ya
kimataifa kwa vijana walio wengi wa Kitanzania kuonekana kuwa na elimu ya
mashaka na isiyoweza kuhimili ushindani wa soko la ajira, ubovu wetu wa elimu
umedumaza uwezo wetu wa ndani wa kusimamia rasilimali za Taifa, Aidha kambi
Rasmi ya Upinzani inawapa angalizo wananchi wote wa Tanzania kwamba haya yote
yanatokea kwa kuwa Serikali ya CCM haijaiweka Elimu kuwa kipaumbele cha taifa na
kwamba umefika wakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala kwa
kuchagua chama chenye nia ya dhati ya kuleta mabadilko kitakachounda Serikali
inayojali elimu ya watoto wao na bila shaka chama hicho hakiwezi kuwa CCM
tena.
Mheshimiwa Spika, Taifa kupitia hotuba
hii linataka kujua Serikali ina nini cha kusema kuhusiana na utafiti huu
iliofanya mwaka 2011, imetekeleza mangapi kati ya mapendekezo 27 yaliyotolewa.
Aidha ni kwa nini imeunda tume nyingine kwa kutumia fedha za walipa kodi wa nchi
hii ingali ripoti nyingine inayohusu somo hilo hilo ikiwa mkononi.
4.
UNYANYAPAA WA FIKRA VYUO VIKUU
Mheshimiwa
Spika, pamoja na nia njema ya katiba ya nchi yetu kuheshimu haki ya uhuru wa
mawazo kama ilivyowekwa bayana katika Ibara ya 18(a) na Ibara ya 20(1) kwa kutoa
uhuru wa mtu kushirikiana na wengine, kumekuwepo na propaganda mbalimbali hasa
kwenye taasisi za elimu ya juu, zenye kuminya nafasi na uhuru wa vyama vya
upinzani kuendesha shughuli zake kwa usawa, uwazi na kwa haki katika ngazi ya
elimu ya juu kama ambavyo chama tawala kimejiwekea na kujitengenezea mazingira
hayo.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alisema hivi: "Lakini kutoa uongozi maana yake siyo
kuwanyang'anya watu wenyewe mamlaka yao. Watu lazima wafanye uamuzi wao wenyewe
kuhusu maisha yao ya baadae kwa kufuata njia za demokrasia. Uongozi hauwezi
kuchukua nafasi ya demokrasi; uongozi lazima uwe sehemu ya
demokrasi"
Mheshimiwa Spika, tafakuri ya nukuu hii
imekuja wakati ambao ushiriki wa wanafunzi wa elimu ya juu katika siasa
unaonekana kulemea upande moja tu wa kukipendelea na kukipa uwezo chama tawala
katika shughuli zake kwenye taasisi hizo. CCM wamefikiri na kuamua kuanzisha
mkoa maalumu kwa sasa wakitambua kuwa vyuo (hasa vyuo vikuu) haviruhusiwi
kuendesha shughuli za siasa vyuoni, kama ilivyo majeshi, makanisa au misikiti na
ili kuthibitisha hilo wameelekeza pia shughuli za mkoa maalumu ulioanzishwa
zifanyike nje ya chuo. Lakini tujiulize na kutafakari zaidi kuhusu
mshindo (impact) wa shughuli za mkoa maalumu wa kisiasa ndani ya himaya
za vyuo vikuu na elimu ya juu nchini.
Mheshimiwa Spika, ni ngumu kuamini kuwa
shughuli za siasa vyuoni, ambazo Tanzania Commission of University Act imeweka
bayana kuwa ni kosa, zitaweza kudhibitiwa ikiwa vyama vingine vinajiwekea
uhalali na mazingira ya kuingiza wanavyuo kwenye siasa, jambo ambalo udhibiti
wake ni mgumu kwa mamlaka husika hasa vyuoni kwa kuwa wanavyuo hufanya vikao vya
siasa kwa siri, na kwa nyakati ambazo uongozi wa vyuo hauna taarifa.
Mheshimiwa Spika, kwa uangalifu mkubwa,
ningependa kutoa angalizo kuwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitokubali
unyanyapaa wa fikra wa aina yoyote utakaoendana na kujenga matabaka kutokana na
utofauti wa mitazamo baina ya jamii ya wasomi kwa kuwa, kutoka taasisi
mbalimbali za elimu ya juu , chimbuko la viongozi mahiri wa nchi hii pamoja na
nchi nyingine mbalimbali duniani limechipukia. Kambi Rasmi ya Upinzani,
itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa taifa kwa kupitia wanafunzi wa
elimu ya juu, wanapata fursa mbalimbali za kuikomboa jamii ya kitanzania ambayo
inadumazwa kwa unyanyapaa wa fikra.
Mheshimiwa Spika, njia pekee ya kufuta
unyanyapaa wa fikra kwa vijana waliopo kwenye elimu ya juu ni kwa Serikali
kurejesha rasmi na kuruhusu uwepo wa siasa katika elimu ya juu na vyuo vikuu
vyote nchini kama shughuli ambazo ni nje ya masomo ili kusaidia kujenga uwanja
wa demokrasia katika serikali za vyuo na vile vile itasaidia katika kuweka
mazingira ambapo wasomi wetu wanaanza kujifunza mbinu na utendaji wa kisiasa
katika mazingira ya elimu ili waweze kujifunza kuishi pamoja, kupingana kwa hoja
na kujua jinsi ya kuvumiliana katika mazingira ya tofauti mbalimbali za
kiitikadi, imani, na mtazamo kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya
CHADEMA ya mwaka 2010. Hapa nikisisitiza maneno ya baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere juu ya kuboresha maisha ya Watanzania:
"Tukiwasaidia watu wa Tanzania kuendelea,
ndiyo tunaiendeleza Tanzania. Maana Tanzania Ni ya Watanzania Na Watanzania Ni
wote, Hakuna mtu mwenye haki ya kusema "Mimi ndiyo watu". Wala hakuna Mtanzania
mwenye haki ya kusema " Najua linalowafaa watanzania na wengine lazima
wafuate".
No comments:
Post a Comment