Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Bumbuli kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Makamba, ameelezea kusikitishwa kwake na
masuala ya imani ya kishirikina kupiga hodi kwenye Jimbo lake.
January Makamba, Mbunge wa Bumbuli
Akielezea kwa kina kwenye
akaunti yake ya facebook, Makamba alisema kuwa Ijumaa na Jumamosi walikwenda Bumbuli watu wanaodai wana uwezo wa kutoa wachawi na kuamua kuwachangisha watu
fedha kwa ajili ya zoezi hilo na kudhalilisha wazee na kina mama
wengi na kusababisha wanyanyaswe na kufanyiwa fujo.
January Makamba kushoto akizungumza na baadhi ya wananchi wake jimboni Bumbuli hivi karibuni.
Alisema kuwa baada ya kuona hivyo, aliamua kuzungumza na viongozi na Mkuu wa Wilaya
kwamba watu hao wafukuzwe mara moja na wakamatwe kwasababu zoezi hilo ni
kinyume cha Sheria za nchi.
"Vilevile, katika zama hizi mambo ya uchawi na kutafuta wachawi hayana
nafasi kabisa. Ni mambo ambayo yametubakiza nyuma kimaendeleo miaka nenda rudi.
"Baada ya witch-hunters kufukuzwa kuna baadhi ya
vijana walioratibu ujio wao walienda kituo cha polisi Bumbuli na kujaribu
kung'oa dirisha na kuvunja mlango. Kituo cha Polisi hakijachomwa moto. Pia wakaenda
kwenye Ofisi ya Afisa Tarafa na kujaribu kuvunja Ofisi," alisema Makamba.
Aliendelea kusema kuwa wote wamekatwa Jumapili na kupata message nyingi za wapiga kura wakimpongeza kwa kuzuia upuuzi na wengine wakitaka waruhusiwe watoa uchawi.
"Kama viongozi, tunayo kazi
kubwa ya kuelimisha watu kuhusu hizi imani.
Changamoto kwetu kule sio tu masuala ya
barabara, maji, umeme, nk lakini pia haya masuala. Bahati mbaya imani za
kichawi zimeshamiri sana kwenye jamii nyingi za Kiafrika na kazi ya kuziondoa
ni kubwa sana.
"Mara nyingi zinatokana na maendeleo kuwa duni
lakini vilevile imani hizo ni chanzo cha maendeleo duni. Hadithi ya kuku na yai
kipi kilianza, bahati nzuri hali imetulia. Kilifanyika kikao cha
Madiwani wote, wenyeviti wote wa vijiji na Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa
kuweka msimamo wa pamoja kuhusu haya masuala ikiwemo elimu kwa umma," alisema.
No comments:
Post a Comment