Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Beijing Construction
Engineering Group, jana imeonyesha rasmi picha za Uwanja Mpya wa Yanga
utakavyokuwa mara baada ya kuingia mkataba wa ujenzi wake mwishoni mwa mwezi
ujao kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo.
Uwanja mpya wa Yanga utakavyoonekana baada ya kukamilika.
Uwanja huo utakaokuwa na hadhi
ya aina yake, utajengwa kwa thamani waya zaidi ya Dola Milioni 50, huku ukichukua
eneo la hekta 11.5 katika eneo lote la Yanga, Jangwani City.
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam katika kikao cha viongozi wa Yanga, kilichoongozwa na Mjumbe wa Bodi ya
Udhamini ya Yanga, Francis Kifukwe, Meneja Msaidizi wa kampuni hiyo iliyojenga pia
Uwanja wa Taifa, Zhang David Chengwei, alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo
itategemea na makubaliano kutoka kwa Yanga.
“Utakuwa ni uwanja wenye hadhi
na uwezo mzuri kiasi ambacho kitaiweka Yanga katika kiwango kizuri mno, ingawa
hayo pia yatategemea makubaliano yetu na klabu kwa ujumla.
Katika ujenzi huu kwanza
tulipewa kazi ya kuandaa ramani nzuri kwa ajili ya Uwanja huo wa kisasa wa
Yanga, hivyo tunawaachia wahusika kwa ajili ya kuona kile kitakachofuata baada
ya kuwaonyesha jinsi kazi hiyo itakavyoanza,” alisema Chengwei.
Aidha, Kifukwe alisema kuwa,
waliwaagiza wataalamu hao tangu mwishoni mwa mwaka jana, jambo ambalo
wamelifanikisha kwa kuwaita na kuzungumza nao kwa kirefu huku wakionyesha kwa
vitendo mwanzo na mwisho wa ujenzi huo wa Uwanja.
“Baada ya kuonyeshwa jinsi
uwanja huu utakavyokuwa utakapokamilika, tutakaa kwa pamoja kujadili gharama
rasmi na kuwajulisha pia wana Yanga hatua hii, maana hii ni klabu ya wanachama
na wanapaswa kufahamishwa hatua kwa hatua.
“Tutapitia wote gharama za Dola
Milioni 50 kwa chagua la kwanza, Dola Milioni 40 na 30, huku tukitarajia
kukutana na serikali kuangalia namna gani ramani ya Hekta 11 itatimia,” alisema
Kifukwe.
Kwa mujibu wa Kampuni hiyo
iliyopewa kazi ya kujenga uwanja huo wa kisasa wa Yanga, kukamilika kwake
kutabadilisha kabisa eneo hilo na kuvutia zaidi kutokana na ramani na jinsi
walivyoupanga uwanja huo utakaokuwa wa kuvutia.
No comments:
Post a Comment