https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, April 01, 2013

Gambo Cup iwe chachu ya maendeleo ya michezo Korogwe



SIWEZI KUVUMILIA


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa michezo, wakiwamo wa mpira wa miguu wanaelewa kuwa klabu za Simba, Yanga na nyingine za Ligi Kuu msingi wake mkuu upo kwenye ligi za mchangani.
Mrisho Gambo kushoto akishuhudia Ridhiwan Kikwete akikabidhiwa jezi za michuano hiyo ya Gambo Cup wilayani Korogwe.

Na kama hiyo haitoshi, pia msingi wake upo kwenye klabu zinazoshiriki Ligi ndogo, zikiwapo zile zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini TFF, zinazoitwa kama Ligi ya TFF.

 Mkuu wa Wilaya Korogwe, Mrisho Gambo
Ligi hizo, hakika zinaposhirikisha vijana wenye vipaji vya aina yake, hutoa wachezaji wanaokwenda kuwika kwenye klabu kubwa au hata kuwapo kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars.

Ili tuliamini jambo hili, tunapaswa kuwakumbuka wachezaji ambao kwa sasa ni mategemeo makubwa kwa Taifa letu. Mchezaji kama Mbwana Samatta, alianzia katika klabu ya Mbagala Market, baadaye ikaitwa African Lyon, ambapo pia alipita njia na kutua Simba ambayo nayo ikamuuza nchini Kongo kwa klabu ya TP Mazembe.

Huyu na wengine wengi, akiwamo Thomas Ulimwengu, Kigi Makasy na wengineo hakika wananifanya niamini kuwa siku zote, msingi wa soka letu upo kwa vijana hao.

Ni kutokana na hilo, najaribu kuvuta picha, namna gani viongozi wa chama na serikali wanakuwa kwenye msingi wa kuendeleza michezo kama msingi wa maendeleo ya wapiga kura wao.

Ukiangalia katika wilaya ya Korogwe, miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na mguso mkubwa katika suala zima la michezo, ikiwamo soka, ambapo timu mbalimbali zilikuwa zikifanya vyema.

Timu kama vile Manundu Shooting ni kati ya zile ambazo zilitishia hata timu za Tanga Mjini, ikiwamo Coastal Union. Wilaya nzima ya Korogwe, hasa kutokana na kukua kwake kimaendeleo, kulisababisha mguso na joto la kila mmoja kujiingiza kwenye michezo.

Hata hivyo, katikati mambo yalionekana kama vile yameanza kudorora, hadi tuliposhuhudia ujio mpya wa Mkuu wa Wilaya, Mrisho Gambo, umekuwa kwenye malengo ya kuwekeza zaidi kwenye michezo kwa kuona ni msingi wa kimaendeleo wa watu wake.

Tunampongeza mwanasiasa huyo ambaye hakika ligi yake inayojulikana kama Gambo Cup, inashirikisha timu mbalimbali kutoka kwenye wilaya hiyo inayokua siku hadi siku.

Kwasababu hiyo, ni wakati sasa wa vyama vya michezo, kwenye wilaya hiyo, hasa wa Chama Cha Soka wilayani Korogwe (KRFA) kupambana na kutumia nafasi hiyo vizuri.

Wataalamu wa mambo wanasema ikiwaka mulika. Vinginevyo tutaona athari ya viongozi kushindwa kutumia nafasi zao kwa maendeleo ya Taifa. Kwa bahati mbaya, siku zote nimekuwa nikishindwa kuvumilia kuona kuwa tunakosa viongozi wenye uthubutu.

Suala hilo lipo zaidi kwa wadau wa michezo, ndio maana tunashuhudia mikoa mingi ikikosa mashiko katika michezo. Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama nikiulaumu Mkoa wa Tanga kwa miaka ya hivi karibuni, maana kwa kiasi fulani wamekuwa wakijitahidi hadi kufanikisha kuwa na timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu, kama vile Coastal Union ya Tanga Mjini na Mgambo Shooting.

Huu ndio ukweli. Lakini bado tunapaswa kufanya bidii kubwa, hasa kwa kuona wenye uwezo wao, wakiwamo Wakuu wa wilaya, Wabunge na Makampuni yanakuwa kwenye mipango ya kuendeleza michezo kwa namna moja ama nyingine.

Kwa wilaya ya Korogwe, naamini sasa vijana wao watakuwa na nafasi nzuri ya kuonyesha uwezo wao, sanjari na kufanya bidii ili wapate nafasi ya kuwika katika timu kubwa au hata kwenye timu ya Taifa.

Haya ndio matarajio yetu sisi kama wadau wa michezo, hivyo kwa wale wanaokwamisha juhudi za wenye kuipenda jamii na kujitolea katika suala hilo, hakika wanastahili kupingwa vikali.

Michezo ni ajira na ipo haja ya kila mmoja wetu kufanya juhudi kuwashirikisha wanamichezo wetu wakiwamo wa mikoani, maana huko ndiko kwenye wingi wa vijana wenye vipaji vya michezo.

Huo ndio ukweli wa mambo. Kila mmoja wetu lazima ajuwe namna gani anakuwa kwenye juhudi za kuibua damu change na mpya katika michezo, hasa kwa kuona kuwa tunakuwa na ligi zenye mashiko, kama ilivyokuwa hii ya Gambo Cup ambayo inafanyika chini ya udhamini wa Mkuu wa wilaya, Gambo.

Ni michezo tu, hasa soka inayoweza kuwapa ajira nzuri vijana wetu waliokuwa kwenye maisha magumu vijijini na wanaoishia kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji.

Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...