Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema katika adhma yao ya
kujenga uwanja mpya wa kisasa hawataangalia nyuma, hata kama watani zao wa
jadi, Simba SC watachekwa au kupalilia migogoro ndani ya klabu hiyo,
inayoongozwa na Ismail Aden Rage.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako
Yanga inatarajia kuingia mkataba wa kujengewa uwanja wao na
Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group mwishoni mwa mwezi wa tano na
kupokelewa kwa shangwe na wanachama na mashabiki wa timu hiyo inayoongozwa na
Yusuph Manji.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa
Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa hawataangalia nyuma kwa ajili ya kutimiza
malengo ya klabu yao kuwa na uwanja wa kisasa na wenye hadhi ya kufanana na
timu yao.
Alisema ingawa kukamilika kwa uwanja au dalili njema za
kujengwa kwake kutaibua migogoro zaidi kwa watani zao Simba, ila hilo litakuwa
jambo jingine na litapaswa kushughulikiwa na wenye klabu yao.
“Hatutaki utani katika suala hili, ndio maana tayari
tumeshakaa na wenzetu wa Beijing kwa ajili ya kushusha uwanja wenye hadhi na
kuitangaza Yanga katika maendeleo ya soka duniani.
“Wale watakaolumbana kwasababu ya maendeleo yetu watajua
wenyewe, ila kila mtu anapaswa ajuwe kuwa wanachama, mashabiki na wadau wote wa
Yanga tumeungana katika jambo hili la maendeleo,” alisema.
Katika kikao cha kuonyesha ramani ya uwanja huo wa kisasa
utakaojengwa katika eneo la Jangwani City, Uwanja wa Kaunda, kiliwakilishwa na
Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Francis Kifukwe, Lawrence Mwalusako na
viongozi waandamizi ndani ya klabu hiyo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment