MAMBO FULANI MUHIMU
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NASHUKURU kwa dhati wewe mpenzi msomaji wa safu hii
unayeendelea kuwa na mimi kila siku kama ya leo, huku ukiendelea kuipitia kona
hii inayoelezea mambo ya uhusiano na maisha.
Wawili wapendanao
Hakika wewe ndiye wa kushukuliwa kwa kiasi kikubwa maana
umeifanya safu hii iendelee kuwapo katika gazeti pendwa. Baada ya kusema hayo,
naomba nikukaribishe Jumamosi ya leo kama kawaida yetu.
Tujadili mambo ya uhusiano kama unavyojua ndio kitu ambacho
kinawachanganya wengi vichwa vyao, baada ya kutenda kosa moja katika kipindi
cha maisha yake.
Ndugu msomaji wangu, binadamu wengi tunaumizwa kweli na
macho yetu ambayo baada ya kuona kitu hutushawishi kuona ni vizuri vinavyopaswa
kuwa vyetu na kutulia navyo.
Hata hivyo, si kila kionekacho mbele ya macho yetu ni
vizuri. Vingine ni vibaya na haviwezi kutupa furaha kamwe. Vitatusumbua tu.
Hivyo kama hapo awali ulikuwa na mpenzi wako, mchumba au mume wako, huna budi
kutulia na kuona kinachoita mbele yako si kizuri kama ulichokuwa nacho.
Kwanini nasema hivi? Wapo dada au kaka zetu mwisho wa siku
wanalia na kusaga meno kutokana na kucheza katika uhusiano wao. Watu hao licha
ya kuwa na wapenzi wazuri wanaoendana nao, lakini wamefanya makosa kwa
kulazimisha kutoka nje, kisa kuna mpita njia mmoja alimuona na kumtamani.
Si kumpenda, bali alimtamani, jambo ambalo hakika
linasababisha ndoa au uchumba wake kusambaratika. Hili ni jambo la kushangaza
kweli na linahitaji kuangaliwa kwa umakini mno.
Vyema mtu akakubali matokeo. Ni vizuri mtu akajua kuwa
aliyekuwa naye ndio mzuri na mwenye sifa zote. Makala hii ina husu watu kutulia
na kuacha mapepe yao katika mambo ya uhusiano wa kimapenzi.
Nasema haya kwasababu tunakutana nayo sana kwenye jamii
yetu. Wapo watu hasa wasichana wamejikuta wakianza moja, tena wakikutana na
wanaume wadanganyifu baada ya kutamaniwa kwa dakika chache, yeye akaona jambo
jema ni kumuacha mtu wake.
Leo wanalia, maana kule walikoacha au kulazimishwa kuachwa
kwa sababu ya kufanya mambo ya ajabu kila siku, wenzao wameshapata ndoa, au
uchumba wa kudumu,hivyo kuwaacha njia panda.
Ndio hao wanaojaribu tena kuwasumbua wapenzi wao wa zamani,
wakipiga simu kutwa kucha, kutuma barua za mwaliko au kadi za dina, kama njia
yao ya kujirudisha kwa mtu wake huyo ambaye hapana shaka nashawishika kusema
kuwa alimpenda kwa dhati.
Kwa bahati mbaya, dada huyo anavyofanya hivyo, anaumia zaidi
kwa kuona hafanikiwi, hasa kama mwenzake yupo kwenye uhusiano na mtu mwingine
na amekolea kuliko alivyokolea kwake.
Je, nini kinachoendelea hapa? Nani mwenye kufaidi mapenzi
hapa? Na aliyekosea ni nani kati ya watu hawa wawili? Ndio maana nilisema hapo
juu, tuliza akili, kwani mtu akicheza tu ni kosa kubwa.
Mapenzi ni matamani ndio endapo yakikuendea vyema, ila
yakienda tofuati matokeo yake ni magumu mno. Watu wengi wanaathirika
kisaikolojia kwasababu ya kucheza kidogo kwenye uhusiano wao.
Ni vyema watu tukawa makini, hasa kwa kutulia na wenzi wetu
kwa ajili ya kuwaza maisha mengine na sio kuwaza mapenzi kila siku, tena yale
yanayochagizwa na wapita njia.
Wangapi wanalia kutwa kucha kwa kufanya maamuzi mabaya,
aidha kwa kuwaacha waliowapenda na kudanganyika na wapita njia wasiokuwa na
mapenzi ya dhati hata dakika moja?
Sema chochote unachotaka kwa kupitia mawasiliano yangu hapa
chini.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment