Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL)
inaendelea katika raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano
zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Licha ya kuwa tayari Yanga
imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal
Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta
macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa
na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles
Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar
es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo
itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani,
sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A
itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa
African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic
Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo
itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari
kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons.
Nayo Ruvu Shooting itakuwa
nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro
JKT kutoka Arusha.
No comments:
Post a Comment