Timu zetu ziwe na uchu wa mafanikio
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INASIKITISHA kuona bado tunaendelea kuwa wale licha ya
kufanikiwa na kuwa na wachezaji wazuri wenye vipaji vya aina yake katika suala
zima la michezo, ukiwapo mpira wa miguu.
Tanzania hii yenye kila aina ya vipaji, lakini tunapokuwa
kwenye mipango ya kimaendeleo, tunakwama na kuonyesha kuwa kumbe dhamira zetu
ni kutesa katika soka la ndani na sio nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden RageKwa bahati mbaya, hali hii zaidi huchochewa na viongozi wetu wanaofanikiwa kuwa kwenye klabu za soka; wale ambao mawazo yao huwa ni mepesi kwenye uongozi wao.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Hili si jambo zuri katika kuhakikisha kuwa Tanzania yetu inapiga hatua katika medani ya kandanda. Katika kulisemea hilo, sitaacha kuishukuru na kuipongeza timu ya Azam ambayo inaonyesha uchu wa kusonga mbele Kimataifa, lakini kazi ipo kwa wanaoona kuwa wenye haki hiyo ni klabu za Simba na Yanga tu.
Mlinda mlango wa Simba, Juma Kaseja
Hii siwezi kuvumilia. Nikiwa kama mdau wa michezo, ni vyema sasa watu tukabaini kuwa jambo kubwa linalozifanya timu zetu, hasa za Simba na Yanga zishindwe kufanya vyema ni kutokana na kupatikana viongozi wasiokuwa na malengo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji
Viongozi ambao lengo lao kubwa ni kuhakikisha kuwa
wanajiwekea mazingira ya kunyenyekewa na kuonekana wao bora, jambo ambalo
hakika likiendelea kuachwa kama lilivyokuwa bado hatutaweza kuvunja mwiko wa
kusonga mbele Kimataifa.
Huo ndio ukweli. Kwa mfano, Simba inaweza kusajili wachezaji
30, lakini kati ya wote waliosajiliwa, wapo kwa ajili ya watu Fulani ndani ya
timu hiyo, kwakuwa ndio waliolipa fedha.
Inapotokea kutoelewana, bosi aliyemsajili mchezaji husika,
huweza kutoa amri ya kucheza chini ya kiwango, jambo ambalo huchangia kuvurunda
kwa timu zetu mara kwa mara.
Hali hii haipo Simba tu. Bali Yanga mara kadhaa imekumbwa na
suala hili, kabla ya kumchagua mwenyekiti wao mpya, Yusuph Manji, ambaye naye
amekuwa akiingiza watu kwenye mfumo wa uongozi, akiwapo mtoto wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ridhiwan Kikwete, aliyepewa cheo cha
Mwenyekiti wa Maendeleo ya Jengo la Mafia.
Ndio maana nasema, kama hatutakuwa na viongozi wenye mipango
ya kweli hatuwezi kufanya vyema kamwe. Viongozi wanaowaza maisha yao na si
klabu zao hapo hakuna kitu.
Kwa mwaka huu timu ya Simba inaonyesha haina hata uwezo wa
kuchukua nafasi ya tatu kama si ya pili kutokana na ugumu wa mechi zilizosalia
na mikakati ya wapinzani wao.
Itakuwa ngumu Azam wajibweteke hadi wapitwe na Simba, au
Yanga wajilegeze na kulikosa taji hilo la Tanzania Bara. Itakuwa ni ndoto ya
mchana na haiwezi kutokea.
Ukiangalia kwa karibu, Simba inayoongozwa na mwenyekiti
wake, Ismail Aden Rage, mwaka wote huu imekuwa kwenye migogoro isiyokwisha,
tena inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na Rage.
Hii ni kwasababu amekuwa akitoa kauli za kejeli, dharau na
kudanganya, hali ya kuwa anafahamu kuwa klabu ya Simba ni mali ya wanachama na
sio ya mtu mmoja.
Naweza kusema kuwa Rage hajaweza kusimamia vyema nafasi yake
ya uongozi kwa mwaka huu wote. Mara nyingi amekuwa kwenye mambo yake binafsi
ukiwapo ubunge.
Hii ni jambo linalotakiwa liangaliwe kwa manufaa ya klabu za
Tanzania, hasa kwa kuhakikisha kuwa zinakuwa na viongozi wenye mipango mizuri
kwa maendeleo yao.
Ni bora tuambiane ukweli, japo mara kadhaa huibua malumbano
au kutokuelewana na wadau hao. Tunataka mafanikio na sio ubabe wa Tanzania
pekee.
Kwangu mimi siumii kuona Simba haijachukua Ubingwa wa Bara
msimu huu, bali nitaumia zaidi kuona hata hao Yanga watakaofanikiwa kupata taji
hilo, hawatakuwa na cha maana katika michuano ya Kimataifa, Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Hawa ni wazee wa mechi moja nje. Si Simba wala Yanga. Kwenye
michuano ya Kimataifa, hulitia aibu Taifa, maana mipango yao inakuwa bure
kabisa, ndio maana siwezi kuvumilia.
Nadhani huu ni wakati sasa wa watu wote wakiwapo viongozi wa
klabu za soka Tanzania kuona hakuna muda wa kupiga porojo zaidi ya kutenda kazi
zenye manufaa.
Kama wachezaji wazuri wapo, ndio maana wanafanikiwa
kuonyesha uwezo wao Afrika, akiwamo Mbwana Samatta aliyetokea Simba na sasa
anaipaisha mno timu ya TP Mazembe.
Wapo wachezaji wengine ambao ni Watanzania wanaocheza soka
nje ya nchi, hivyo kuonyesha kuwa viongozi wa soka Tanzania wanashindwa
kuwatumia kwa kuweka mipango thabiti yenye kuleta tija, zaidi ya kuwaamuru
wacheze chini ya kiwango, kufungisha inapotokea migongano ya kimaslahi.
Kazi kweli kweli.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment