MGODI UNAOTEMBEA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SASA nimepata picha kamili kwanini Ofisi ya Bunge walikuwa
na mpango wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge
vinapofanyika mjini Dodoma.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu
Ni dhahiri Ofisi ya Bunge ilijua mengi na kuhitaji kuficha
aibu inayoweza kujitokeza, kama hii ya kuendelea kusikiliza maneno ya dharau,
kejeli na mengineyo ya kuogofya.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
Pamoja na kuwa na lengo hilo la kusitisha, lakini
wanaharakati na wadau wengine walikuwa wakali kama mbogo. Kila mmoja aligoma na
kushangaa pia uamuzi huo.
John Mnyika, Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema
Wengine waliupachika jina la kandamizi la uhuru wa habari
kwa wananchi juu ya Bunge lao. Ati maneno haya yalitolewa na waliotaka
utaratibu wa kurushwa moja uendelee kuwapo.
Ni sawa, ila kwa jinsi hali ya mambo inavyoendelea, wakati
mwingine nasema bora hata vipindi hivyo vizimwe tu. Havina faida tena na
Watanzania.
Ismail Aden Rage, Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM
Profesa Maji Marefu, Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa tiketi ya CCM
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa
Zaidi watu wanajifunza maneno machafu kutoka kwa watu ambao
eti jamii inawategemea wao. Hili ni sawa na kusubiri embe chini ya mwarobaini.
Wakati nasema haya, nakumbuka mzigo mzito wa maisha magumu yanayoendelea
kumkumba Mtanzania.
Maisha yamekuwa magumu na hakuna tena ahueni. Sio mjini wala
vijijini. Kote hali ni tete. Kwa mfano, licha ya kipato cha wananchi wengi
kubaki kama kilivyo, lakini bidhaa zimekuwa zikipanda juu kama ulivyokuwa Mlima
Kilimanjaro.
Leo nauli za mabasi yaendayo mikoani imepanda mara dufu bila
kusahau za daladala ambazo nyingi hazina ubora. Nyingine viti vinachana nguo za
abiria, lakini mwisho wa siku nauli 4oo kutoka Kimara hadi Ubungo lazima ilipwe
na kama mtu hataki atembee kwa miguu na sijaona wabunge wakisimama kwa kauli
moja kupinga ongezeko la nauli maana lipo kwa ajili ya kuwakomoa zaidi
Watanzania.
Nilitarajia wabunge wote wangepinga kwa vitendo na kuwatetea
Watanzania, maana wanajua jinsi maisha yalivyokuwa magumu zaidi ya wao
walivyolia mwaka jana bungeni na kuomba waongezewe posho ambapo baadaye Zitto
Kabwe, aliziponda kwa nguvu kwa madai zinanufaisha wabunge na sio wananchi.
Pamoja na mzigo huo wa nauli, bado zipo bidhaa ambazo ni
ngumu kuzipata kiurahisi kama huna kitu. Unga uliokuwa unauzwa Sh 200 hadi 300
mwaka 2007 sasa unauzwa kwa Sh 1500, wakati vitu kama vile sukari, mchele
vikionekana kama vile ni anasa.
Kwa kuliangalia hili, mimi nilidhani wabunge wetu wangetumia
jambo hili kuwaza namna gani ya kuwakomboa watu wao na sio kukaa kwenye viti
vya kuzunguuka na kusuta umbea.
Je hicho ndio kilichowapeleka bungeni? Je, fedha za umma
ndio matumizi yake hayo? Katika jambo hilo hakika ifikie wakati wabunge wetu
waone haya na kushikwa na uzalendo na Taifa lao.
Wasipoteze muda kujadili vitu visivyokuwa na msingi wakati
wapiga kura wao, wawakilishi wao wanakufa njaa. Kwa Tanzania ya leo yenye
changamoto lukuki hatuhitaji kupoteza muda hata robo.
Kauli kama hizi za ‘Siongei na mbwa bali na naongea na mwenye
mbwa zinaashiria kitu gani’. Wengine wanafika mbali zaidi kwa kutamka maneno
ambayo ukiyatafakari kwa kina utagundua kama sio matusi, basi hayapo kwenye
kundi la wastaarabu.
Hii sio haki na haipendezi hata kidogo. Kwanini nasema
hivyo? Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanzania (CAG), Ludovick Utouh,
amesema kuwa ndani ya serikali kuna ufisadi wa kutupwa unaohitaji kudhibitiwa
kama lengo ni kupiga hatua kimaendeleo kwa kusimamia vyema rasilimali zake
badala ya kutegemea wahisani.
Kwa sasa wahisani mbalimbali wanategemewa kuchangia bajeti
ya Tanzania kwa asilimia 30.
Mbali na ufisadi huo uliozungumzwa na CAG, bali pia ripoti
inasema kuwa deni la Taifa limekuwa kwa kasi ya ajabu na kufikia Shilingi
Trilioni 22, huku mwendo wake ukishindwa kueleweka.
Aidha pia kuna tatizo kubwa la Mfuko wa Pensheni wa
Mashirika ya Umma (PSPF) zaidi ya Shilingi Bilioni 20 bila kuwapo mtiririko
mzuri wa kulipwa fedha hizo ambazo ni michanago ya watumishi wa umma.
Haya ni kati ya mambo ambayo wabunge wetu walistahili kuyavalia
njuga na sio kukalia kazi ya kupeana maneno ya kejeli na dharau. Watu waamini
nini juu ya utendaji kazi wao?
Watanzania watakuwa na imani ya dhati na baadhi ya wabunge
ambao hakika uwepo wao hauna faida. Sio siri, wapo baadhi ya wabunge ambao hata
wasingekuwapo, wananchi wanaona wangeweza kujiendesha.
Kama hivi ndivyo, ina maana heshima tena hawana. Hata wapiti
mbele za watu, ila wenye akili zao wanaona hakuna cha maana anachoweza kuambiwa
au kufanyiwa zaidi ya kusikia maneno mitihiri ya waimbaji wa taarabu kutoka
katika baadhi ya vinywa vya wabunge wetu.
Je hili ndilo kusudio? Sikatai kuwa kuepuka mabishano kati
ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni
kazi kubwa, ila ukiwekwa uzalendo hilo linawezekana.
Linapojadiliwa suala la Watanzania, kila mtu ajuwe kuwa si
kila Mtanzania ni mfuasi wa CCM au mfuasi wa CHADEMA, bila kusahau wale wa CUF,
TLP na vyama vingine vya siasa.
Katika kulijua hilo, wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, iwe ni Zitto Kabwe, John Mnyika, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Murtaza
Mangungu, Idd Azzan, Deo Filikunjombe, Mussa Azzan Zungu na wengineo lazima
wahakikishe kuwa wanaitendea haki nchi yao.
Angalia, kwangu mimi mbunge makini ni yule anayepigania
wananchi na sio kutoa maneno machafu kwa ajili ya kutetea mkate wake au chama
chake cha siasa.
Huo ndio ukweli wa mambo. Tukifanya hivyo tutaweza kuinua
ari ya utendaji kazi kwa Watanzania wote, maana viongozi wao watakuwa
wameshajitambua pia.
Kinyume cha hapo hakuna jipya. Tutakuwa na Bunge la porojo
wakayi utendaji kazi ukiwa sifuri. Tutasikia maombi ya miongozo, kanuni za
Bunge, lakini yote si kwa ajili ya Taifa letu.
Kelele hizo kutoka katika vinywa vya waheshimiwa hao
zitaishia kwenye matusi kuitana ‘boya’, mwingine anamwambia mwenzake kazi yake
eti ni kujamba jamba tu, kweli?
Ndio kazi nzuri ya waheshimiwa hawa? Katika kulifuatilia
zaidi Bunge hili nakumbuka kauli ya Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan kuwa watu
wenye nia ya kugombea ubunge eti lazima kwanza wapiti JKT.
Kwa madai huko watafindishwa uzalendo. Sawa, kauli nzuri
kutoka kwa Mbunge huyu, ila pia anapaswa kujua kuwa tatizo la Taifa letu ni
mfumo mbovu pamoja na watu kutokuwa na mapenzi mema na nchi yao.
Uzalendo mzuri zaidi mtu anajifunza tangu chekechea, shule
ya msingi au sekondari. Kama ukiona hadi amefika chuo hana uzalendo kamwe
hawezi kuupata JKT.
Si kwamba utaratibu huo ukiwekwa hawatakwenda. Watakwenda,
lakini si kutafuta uzalendo bali CV za kuwawezesha kugombea Ubunge kama njia
yao ya kuwapatia wanachokihitaji.
Hatuwezi kwenda hivyo. Ndio maana naendelea kuwaza kila
sekunde juu ya mwenendo wa wabunge wetu. Mara nyingi napatwa na hofu, je,
tutarajie kuvunjwa kwa viti Bungeni siku wabunge hao watakavyoanza kushikana
mashati na kutwangana makonde?
Kumbe je? Mbona maneno ya shombo yanatoka katika vinywa vya
wawakilishi hao wa wananchi bungeni? Je, siku hiyo Lameck Mwigulu Nchemba
atavovaana na Freeman Mbowe bungeni mtaani nako hali itakuwaje?
Nahofu Tanzania kuwa nchi ya vurugu siku za usoni kama
wabunge wasipokumbuka thamani ya kura za wananchi wao kwa ajili ya kuwatumikia
na kuwapatia maisha bora kwa Mtanzania na sio joto, suruba, njaa, mateso
wanayoendelea kukutana nayo kila uchwao.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment