Awataka wanasiasa wazuie juhudi za watendaji serikalini
Apania makubwa zaidi kuhakikisha mambo yanasonga
Na Mwandishi Wetu, Moshi
ILI suala ma maendeleo liweze
kupatikana, hakika kunahitaji utayari wa kujitolea, uvumilivu na uwajibikaji kutoka
kwa jamii yote pamoja na ushirikiano na viongozi wao.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama
Juhudi hizo zikifanywa kwa makini
bila bila kuwapo kwa muingiliano wa majukumu au msuguano wa kifikra ni rahisi kupatikana
maendeleo.
Mlima Kilimanjaro ni miongoni mwa vivutio vya Utalii mkoani humo na Tanzania kwa ujumla.
Katika kulisema hilo, Mkoa wa
Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa inayopiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na
ushirikiano miongoni mwa viongozi na wananchi wake.
Utekelezaji wa mipango ya ukuaji wa
kiuchumi, inatekelezwa kwa kuzingatia fursa mbali mbali zinazopatikana, ikiwemo
uwekezaji wa muda mfupi, muda mrefu na muda wa kati, unaoendelea kufanywa na
wananchi pamoja na serikali ya mkoa.
Katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Kilimanjaro, Mkuu Mkuu wa Mkoa huo, Leonidas Gama, anasema kuwa mipango mbali
mbali ya uwekezaji na utekelezaji wake unafanikisha maendeleo.
Anasema miongoni mwa mikakati hiyo
ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Kimataifa cha Utalii, katika wilaya ya
Siha kitakachokuwa kitovu kikubwa cha mapato mkoani humo.
“Mkoa pia umeanza utekelezaji wa
mkakati wa kuwa na soko la kimataifa la mazao ya nafaka na mboga mboga
linalotarajiwa kujengwa katika eneo la Himo, wilayani Moshi mkoani hapa.
“Katika hatua za awali za
utekelezaji wa mkakati huyo tayari sekretarieti ya mkoa wa Kilimanjaro,
imesaini mkataba wa mkopo wa shilingi bilioni 10 na benki ya uwekezaji ya TIB,
kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika soko hilo,” alisema Gama.
Anasema kuwa mradi huo utaambatana
na mradi mwingine wa ujenzi wa mji wa viwanda na biashara kuzunguka soko hili
la kimataifa la Lokolova, ambapo pia litatoa ajira nyingi kwa wakazi wa mkoa wa
Kilimanjaro.
Wakati mipango hiyo ikiendelea pia
mkuu huyo wa mkoa ameendelea kutekeleza mkakati wa hifadhi ya mazingira wenye
lengo la kurejesha uoto wa asili, hasa kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Kilimanjaro
ulikuwa miongoni mwa mikoa iliyokuwa inapata mvua kwa wingi.
Anasema kuwa tathmini ya utekelezaji
wa mikakati hiyo inaonyesha kuwa malengo yaliyowekwa na mkuu huyo wa mkoa
yanaweza kufikiwa kwa kutumia kipimo cha mafanikio ya maendeleo ya utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005/2012 mkoani Kilimanjaro.
Katika ripoti hiyo ya mafanikio ya
utekelezaji wa ilani kwa kilindi hicho inaonyesha kuwa mkoa wa Kilimanjaro
umepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka saba ya utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2005 mpaka 2012.
“Mkoa umekuwa ukitekeleza na
kusimamia ilani hiyo ya CCM, pamoja na mpango mkakati wa mkoa wa miaka mitano
kwa kuweka vipaumbele katika nyanja muhimu za kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kiutamaduni.
“Katika kipindi cha miaka saba ya
utendaji kazi kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2012, mkoa umekuwa na mafanikio
makubwa katika kukuza uchumi wake na kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi
wake,” alisema RC Gama.
Anasema kuwa sehemu ambazo zimekuwa
na mafanikio na kuufanya Mkoa kuweza kuwa na mafanikio kwa kipindi hicho ni
baada ya kuimarika kwa huduma za elimu, afya, maji, barabara.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana
katika ukuaji wa uchumi, Gama anasema pato la Mkoa limekuwa likiongezeka,
kutoka shilingi milioni 714 mwaka 2005 hadi kufikia shilingi bilioni 1.448
mwaka 2008.
Wastani wa pato la mtu mmoja mmoja
nalo limeongezeka kutoka shilingi 755,037 kwa mwaka 2008 mpaka shilingi 881,884
kufikia mwaka 2010, ikiwa ni juu ya wastani wa pato la mkazi kitaifa la
shilingi 770,464.
RC Gama anasema kuwa makusanyo
katika Halmashauri za wilaya na Manispaa katika vyanzo vyake vya ndani nayo
yameongezeka kutoka shilingi bilioni 2.24 mwaka 2005/2006 na kufikia shilingi
bilioni 6.082 kwa mwaka 2011/2012.
Mpango wa sasa katika kukuza mapato
yake ni kuona kuwa halmashauri hizo zinafikia lengo la kukusanya wastani wa
shilingi bilioni 12.081 kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Anasema kuwa kwa upande wa kilimo
ambacho kinachangia zaidi ya asilimia 60 ya pato la mkoa, kumekuwa na mikakati
ya kukabiliana na ufinyu wa ardhi ya kilimo, kwa kuongeza mahitaji ya pekee ya
pembejeo za na kuboresha utaratibu mzima wa usambazaji wa vocha za pembejeo.
Mkoa wa Kilimanjaro una eneo la
hekta 643,000 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo hekta 579,700 ndizo
zinazotumika kwa kilimo cha umwagiliaji, na kubainisha kuwa yapo matumaini
makubwa ya kuendeleza hekta 238,500 kwa ajili ya kilimo.
Mpango wa kuongeza vocha za pembejeo
unakusudia kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umepatiwa jumla ya vocha 181,577, ikiwa ni
ruzuku kwa ajili ya kaya 60,519, ukiwa ni mpango wa kukuza uchumi kupitia sekta
ya kilimo.
Gama anasema kuwa Mkoa wa
Kilimanjaro una viwanda vikubwa na vya kati vipatavyo 28, ambavyo vimeajiri
jumla ya wafanyakazi 4,862, sambamba na kuwa na biashara rasmi 8,800 na zile
zisizokuwa rasmi 7,080 na kutoa ajira 42,240.
Kuhusu Utalii, Gama anasema kuwa wakati
mipango hiyo ikiwa kwenye mchakato, Kilimanjaro kwa miaka saba iliyopita,
umefanikiwa kuwa na vivutio vya utalii ikiwemo hifadhi ya taifa ya Mlima
Kilimanjaro na msitu unaozunguka mlima huo, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Bwawa
la Nyumba ya Mungu na Misitu ya Asili.
Kulingana na takwimu idadi ya
watalii imeongezeka kutoka 28,417 mwaka 2003/2004 hadi watalii 52,570 mwaka
2010/2011, huku mapato yaliyotokana na utalii huo yakiongezeka kutoka shilingi
bilioni 10.15 mwaka 2003/2004 hadi bilioni 45.604 mwaka 2010/2011.
“Changamoto kubwa hivi sasa ni
kukosekana kwa hoteli zenye hadhi ya nyota tano, hivyo kulazimika kuunda kamati
ya kuibua fursa za utalii kwa madhumuni ya kuongeza vivutio vya utalii, ajira
na mapato kwa halmashari.
“Sekta ya utalii imechangia kutoa
ajira kwa vijana wakiwemo wapagazi, waongozaji watalii, makampuni ya utalii na
ajira kwenye mahoteli mbali mbali hapa mkoani,” Alisema.
Kwa kutambua hilo mkuu wa mkoa Gama,
anasema hivi sasa mkoa wa Kilimanjaro umeamua kuelekeza nguvu kupiga vita
matumizi ya pombe kwa wananchi hasa vijana wengi saa za kazi.
Anasema unywaji pombe saa za kazi ni
changamoto kubwa kwa mkoa wa Kilimanjaro, kwani wote wanaojihusisha na unywaji
huo pia wamekuwa wakipata madhara kiafya.
Unywaji wa pombe pia umekuwa
ikiambatana na vitendo vya ukahaba unaofanywa na baadhi ya wasichana ambao
wanaacha kujishughulisha na kutafuta njia ya mkato ya kujipatia kipato.
Aidha, Gama anasema kuwa ukiacha
mafanikio pamoja na mipango ya mkoa chini ya uongozi wake, kumekuwa na
changamoto ya kisiasa inayojitokeza na kuwalenga viongozi na watendaji wa
serikali katika mkoa wao wa Kilimanjaro.
Changamoto hii kutoka kwa baadhi ya
viongozi wa vyama vya kisiasa vya upinzani ya kuwakashifu na kuwakejeli
viongozi na watendaji wa serikali inatokana na hatua yao ya kudhibiti matumizi
mabaya ya fedha za serikali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo kupitia Halmashauri
za wilaya mkoani hapa.
Mathalani kwa kipindi cha miezi sita
sasa baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka vyama vya upinzani wakiwemo wale wa
kitaifa, wametoa maneno ya kashfa na kejeli wa viongozi wa serikali mkoani
Kilimanjaro, jambo ambalo kwa upande wao haliwezi kuwakatisha tamaa.
No comments:
Post a Comment