Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU ya Yanga na Kocha
Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh.
500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) inayoendelea nchini.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji akizungumza na waandishi wa habari.
Adhabu hizo zimetolewa
na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na
makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171.
Yanga imepigwa faini
hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh.
100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting) dhidi ya African Lyon iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
Naye Kocha Bilali
amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa
maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi
la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na
Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.
African Lyon na Simba
zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa kuchezesha timu zao za
U20 kwenye mechi za utangulizi wakati zilipocheza na Oljoro JKT na Coastal
Union, Machi mwaka huu kwenye viwanja vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.
Suala la Meneja wa
Coastal Union, Akida Manchai kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu
Mwenyekiti wake Steven Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na
Coastal Union iliyochezwa Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa
Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu, huku adhabu zote zimetolewa
kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom.
No comments:
Post a Comment