Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya Handeni, mkoani Tanga, Muhingo Rweyemamu, pichani chini mwenye miwani, ameendelea
kumlilia marehemu Hussein Semdoe na kusema kuwa anajaribu kuwashawishi viongozi
wenzake juu ya kuwakumbuka marehemu kwa kupanda miti.
Marehemu Hussein Semdoe, enzi za uhai wake
Semdoe aliyekuwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi
wilayani Handeni, alifariki pamoja Hassan Bwanga mwandishi wa gazeti la Uhuru
na Mzalendo na Afisa Uhamiaji wilaya, Mariam Hassan.
Akizungumza na Handeni Kwetu Blog kwa njia ya simu,
Rweyemamu alisema kuwa vifo vyao ni pengo hivyo itakuwa jambo la busara kama
wataweka utaratibu wa kuwaenzi kwa kupanda miti.
Alisema kuwa endapo jambo hilo litafanikiwa, basi utaratibu
wa kupanda miti sambamba na kutunza mazingira litakuwa na faida kwa wilaya yao
ambayo ina changamoto za uharibifu wa mazingira.
“Tutaendelea kumlilia Semdoe na wenzake kwa vifo vyao, ila
kubwa zaidi tuwaenzi kwa vitendo kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na siku ya upandaji
miti siku ya vifo vyao.
“Hili bado halikujadiliwa, ila nafikiria kuwashauri hata
watu wa Misitu juu ya suala hili,” alisema Rweyemamu.
Kifo cha Semdoe na wenzake vilipokelewa kwa majonzi makubwa,
vilivyotokea katika Kata ya Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga.
No comments:
Post a Comment