LIGI Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam hatua ya sita bora inamalizika kesho ambapo timu tatu zitakata tiketi ya kucheza hatua ya Kanda ili kupata nafasi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Msemaji wa DRFA, Mohamed Mharizo
Ofisa Habari wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Mohamed Mharizo, amesema leo mchana kuwa ligi hiyo
iliyoanza Aprili 15 ndio itapata wawakilishi watatu watakaouwakilisha mkoa huo
katika hatua ya Kanda.
Alizitaja mechi zitakazochezwa leo kuwa ni Red
Coast itakuwa ikimenyana na Day Break kwenye uwanja wa Kinesi, wakati kwenye
Uwanja wa Makurumla, Friends Rangers wao watakuwa wakichuana vikali na Sharif
Stars, huku kwenye Uwanja wa Airwing, Boom FC itakuwa ikikabiliana na Abajalo.
Hadi sasa Red Coast inaongoza ligi hiyo
ikiwa na pointi 8, ikifuatiwa na Abajalo yenye pointi 7, wakati Sharif Stars
inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 6.
Friends Rangers wao wanashika nafasi ya
nne wakiwa na pointi 5 huku Day Break wakiwa na pointi 3 na Boom FC ikishika
mkia kwa kujikusanyia pointi 2.
Mharizo aliwataka mashabiki wa timu hizo
kuhakikisha wanafika uwanjani kwa wingi kushuhudia mechi hizo kwa usalama ili
kuepuka kuvuruga mashindano.
“Kuna mashabiki wa baadhi ya timu
wamekuwa wakifanya vurugu, tabia hiyo si ya kiungwana na DRFA haipendezwi nayo,
ndio maana tumeona tuweke ulinzi katika baadhi ya mechi, hata kesho (leo)
ulinzi utaimarishwa ili kuhakikisha mashindano yanamalizika kwa usalama,”
alisema.
No comments:
Post a Comment