Rais Jakaya Kikwete akipeana mkono na mashujaa wetu.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
VIONGOZI wa mataifa
mbalimbali duniani, kila mara wanakutana katika vikao vya kimataifa kusaka
amani, bila amani hakuna kitu chochote kinachoweza kufanya nchi isonge mbele.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, enzi hizo.
Utasongaje mbele
wakati kila saa ni migogoro na vita? Lakini Watanzania tumejaliwa kwa kiasi
kikubwa kuwa na amani, ambayo kwa sasa kuna baadhi ya watu wanataka kuichezea.
Ni kama vile wamechoka nayo.
Lakini wakati kukiwa
na migogoro mingine ambayo haina tija, kuna kitu ambacho kimeanzishwa ili
kuwakumbusha Watanzania kuhusu misingi halisi tuliyowekewa na waasisi wa Taifa
hili.
Hiki si kingine
isipokuwa ni mbio za Uhuru Marathon, ambazo zitafanyika mwishoni mwa mwaka huu
huku Rais Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wake naye ameamua kushiriki kama
kinara na jemedari wa Taifa hili ambapo mara kwa mara amekuwa akiwakumbusha
wananchi juu ya umuhimu wa kuenzi amani iliyopo..
Akithibitisha hilo,
Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck, anasema lengo la mbio hizo ni
kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na kuuenzi urithi
waliaochiwa na viongozi waliopigania uhuru wa nchi.
Anasema urithi huo
ambao utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo, ni upendo, mshikamano,
umoja na amani iliyopo. Melleck anasema mbio hizo zitakuwa zikifanyika kila
mwaka na zitaanza rasmi siku ya tarehe 08/12/2013 na zitatanguliwa na
shamrashamra za kanda zote za Nchi yetu.
Hilo lilithibitishwa
pia na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ,
ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati zinazinduliwa jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa mbio hizo
ulienda sambamba na kuzinduliwa rasmi kwa mtandao wa Uhuru Marathon ambao
utakuwa na habari za kila aina kuhusu mbio hizo na washirika wake.
Dk. Mukangara
alipongeza wazo la kuanzishwa mbio hizo ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka,
lengo likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo miongoni mwa Watanzania na
kuuenzi uhuru wetu.
Waziri alikiri, kwa
sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa nchini, lakini hakuna ambaye alikuja na
wazo zuri la kuanzisha mbio kama hizo za kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani
nchini.
“Nawapongeza
waandaaji wa mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo hili
zuri la kuanzisha mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa nyumbani, lakini
hatukuwa tumewaza kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi uhuru wetu na kudumisha
amani yetu.
“… Kwa niaba ya
Serikali, napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na wazo hili la
kuanzisha mbio hizi za Uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba wadau na wapenda
maendeleo ya michezo kuungana na taasisi hii kufanikisha mpango huu ili uweze
kuwa na mafanikio.
“Serikali bado
itaendelea kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na wadau wenye
nia nzuri ya kuendeleza michezo nchini. Nina hakika waheshimiwa mawaziri,
wabunge, viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika binafsi na viongozi wa dini
wote watajitokeza kushiriki mbio hizi,” alisema.
Hapa ndipo tunapoweza
kusema kwamba, fikiria mbio zozote kubwa duniani kama vile London Marathon
nchini Uingereza, Paris Marathon, Ufaransa au zile zingine zenye kupendwa na
wengi zaidi duniani za Berlin Marathon zinazofanyika Ujerumani kila mwaka,
lakini Uhuru Marathon ni zaidi ya mbio.
Kwani mashindano yote
haya ni ya kutukuka, kutokana na kushirikisha wanariadha wenye majina makubwa
duniani, huku kukiwa na ushindani mkubwa zaidi miongoni mwa washiriki.
Lakini kwa sasa
Tanzania ina cha kujivunia zaidi kwa ujio wa mashindano ya mbio Uhuru Marathon.
Upekee wa shindano
hilo la Uhuru Marathon ni kutokana na aina ya washiriki wake, pamoja na kupewa
tafu kubwa na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, ambao wanataka kuiona
Tanzania inatangazwa zaidi.
Hivyo, shindano la
Uhuru Marathon, lina nafasi kubwa ya kuwabeba Watanzania kwa kutangazika zaidi,
hasa ukichukulia uzoefu mkubwa walionao waandaaji wa Berlin Marathon ikiwa
pamoja na kuchangia kudumisha amani na upendo nchini.
Mratibu wa mbio hizo,
Innocent melleck anasema, ana imani mbio hizo zitajizolea umaarufu mkubwa,
kutokana na jinsi zitakavyoteka hisia za watu mbalimbali, wakiwemo wanamichezo.
Katika mbio hizo,
zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia mbio za kilomita
3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full Marathon yenyewe
kilomita 42.
Mratibu huyo anasema
mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali,
wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa
ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa tunachotaka
kufanya katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile viongozi maarufu wa
dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili kushiriki, kwa kudumisha amani na
upendo.
“Pia tutahakikisha
kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji
mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani
kushiriki,” anasema.
Mratibu huyo
anafafanua kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha wanafanya mambo
makubwa zaidi na ambayo yataleta tija kwa taifa.
Wakati Uhuru Marathon
ikitambulishwa bungeni, kiongozi aliyeonekana kufurahishwa zaidi na hilo ni
Spika Anne Makinda, ambaye hakuishia kulimwagia sifa tu, bali alitaka hata
viongozi wahakikishe wanalifanikisha.
“Ni wazo zuri hasa
katika kipindi hiki ambacho tunapigania amani na mshikamano miongoni mwetu,
tunatakiwa kuenzi mashindano kama haya ili kutufanya tuwe wamoja zaidi,”
alisema Spika Makinda.
Msaada
wa Berlin Marathon
Melleck anasema,
wamefanya mazungumzo na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, kwani hilo
ni moja kati ya mashindano makubwa zaidi duniani, likiwa linashirikisha
washiriki mbalimbali walio maarufu zaidi.
Shindano la Berlin
Marathon au maarufu zaidi kwa jina la BMW Berlin Marathon kutokana na
kudhaminiwa na kampuni ya BMW ni maarufu zaidi ndani ya Ujerumani na duniani
kwa ujumla.
Shindano hilo la Full
Marathon la kiilomita 42.195 ambalo linawashirikisha wanariadha wa kulipwa na
wale wa ridhaa, lilianza kwa mara ya kwanza mwaka 1974 na linafanyika kila wiki
ya mwisho wa Septemba kila mwaka.
Shindano hili kwa
umaarufu wake, mwaka 2008 lilishirikisha wanariadha takriban 40,827 kutoka
mataifa 107, huku waliomaliza mbio wakiwa 35,913 na lina zawadi mbalimbali za
kuvutia.
Uhuru
Marathon je?
Melleck anasema,
ushirikiano wa Berlin Marathon una maana kubwa, kwani itasaidia kuitangaza
zaidi Tanzania na kuifanya dunia itambue umuhimu wa amani, upendo, umoja na
mshikamano miongoni mwetu.
“Wanariadha wengi
watashiriki katika mbio hizi, wengi wakiwa maarufu zaidi duniani, pamoja na
viongozi wa kada mbalimbali na hivyo kutimiza lengo tulilojiwekea.”
Mratibu huyo anasema,
kuna kila haja kwa Watanzania, kuyathamini mashindano hayo, kwani yana lengo la
kuwafanya wawe wamoja zaidi, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho kuna
majaribu ya kila aina.
“Waasisi wetu wa
taifa na wale waliopigania uhuru, walikuwa na malengo mengi na tunatakiwa
kuyadumisha hayo, hilo ndilo Uhuru Marathon inalotakapigania,” anasema.
Kwa Watanzania
itakuwa faraja zaidi, hasa ukichukulia jinsi taifa linavyoweza kufaidika kwa
kuzalisha pia wanariadha wa aina mbalimbali.
Hivyo Uhuru Marathon
ni zaidi yambio, kwani inatukumbusha tulipotoka, tulipo na tunapokwenda!
MWISHOOOOOOOOOO
No comments:
Post a Comment