Ally Choki, Mkurugenzi wa Extra Bongo
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, amesema
kwamba sasa wamekuwa imara zaidi tofauti na walivyoanza kwa kwa kufanya juhudi
kuwapa raha mashabiki wao.
Akizungumza na Handeni Kwetu, Choki alisema kuwa
hata bonanza lao wanalopiga Garden Breeze, Magomeni kila Jumapili, limepata
mashabiki wengi kila wiki.
Alisema hali hiyo inawapa imani kuwa maendeleo yao ni mazuri
tofauti na walivyoanza, wanamuziki wengi wakitokea katika bendi za watu,
akiwamo yeye aliyekuwa Twanga Pepeta.
“Sasa naweza kusema kuwa bendi yetu imeshakuwa imara zaidi
na ndio maana mashabiki wengi wanaingia kwa wingi kwenye shoo zetu kila siku ya
Mungu.
“Naamini kinachofuata sasa ni mafanikio katika ramani ya
muziki wa dansi kutokana na juhudi zetu, mvuto na mipango ya kufanya shoo za
aina yake kwa ajili ya kuwapatia burudani kamili wadau wetu,” alisema.
Extra Bongo imepangwa kusindikiza uzinduzi wa bendi ya
Victoria Sound, ikiwa chini ya Mwinjuma Muumini, unaotarajiwa kufanyika Machi
Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment