Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa.
Na Rahimu Kambi, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa, amesema ili
kuondoa tatizo la ukosefu wa mtandao wilayani kwake, wamefikisha suala hilo
katika Wizara husika na kuahidiwa kujengewa minara mitatu katika baadhi ya
maeneo yao mapema mwaka huu.
Minara ya simu inavyoonekana pichani.
Akizungumza na Handeni Kwetu mapema wiki hii, Liwowa alisema
kuwa bila hivyo maendeleo kwenye wilaya yao yatachelewa kwasababu ya biashara
nyingi kuhitaji mtandao wa uhakika, tofauti na hali ilvyokuwa muda huu.
Alisema wananchi na wageni wengi wanaokwenda wilayani humo
kwa shughuli mbalimbali, wanalazimika kuishi kwa tabu au kurudi mijini ili
wakamilishe kazi zao hizo, jambo ambalo kama wilaya wanakabiriana nalo.
“Dunia ya leo bila kuwa na mitandao ya uhakika huwezi kupata
maendeleo ya aina yoyote, hivyo baada ya kuona suala hili, nilijaribu
kuzungumza na wenzetu ili watuwekee minara ya kufanikisha huduma za mitandao
japo kwa kiasi kidogo tu.
“Unaweza kupiga simu wakati mwingine ukose mtandao, tena
wale wanaotaka kutumia kompyuta zao ndio kabisa, hivyo nadhani baada ya
kufanikisha suala hilo kutoka kwa serikali kuu, ikiwamo Wizara ya Mawasiliano
na ile ya Habari, kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Liwowa.
Aidha, matatizo ya mtandao yamekuwa juu kwa wilaya ya
Kilindi ambayo imetokana ndani ya Wilaya ya Handeni, tofauti na wilaya ya
Korogwe, Muheza na Lushoto ambazo zote zinaunda Mkoa wa Tanga, unaongozwa na RC
wake, Chiku Gallawa.
No comments:
Post a Comment