Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kocha Mkuu wa Azam,
Stewart John Hall (pichani), amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26
mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa
timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa
kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa
Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni
Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi
kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga
uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na
Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa
kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika
mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye
benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya
Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea
lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4
mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina
Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye
benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji,
Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT
kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile timu ya Azam
imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati
yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam
Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia Coastal Union
imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za
maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba
iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya African
Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba
cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union
iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso ya
Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya
ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka
jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya ushirikina ya
sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye
mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage
mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers
imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha chafu
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na
kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa
faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka
kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira
miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa
zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani au kutofika
kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal
Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba
Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola
wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza
kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada
ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa vile masuala ya
wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa
na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa
hatua.
No comments:
Post a Comment