SIWEZI KUVUMILIA
Jerry Teegete, mshambuliaji wa Yanga.
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
INASIKITISHA kama
wapo wadau au wanamichezo wanaendelea kuamini kuwa ili wajiweke kwenye kiwango
cha juu, au kuzipatia mafanikio timu zao, basi ni lazima wapate waganga makini
wa kuwapaatia dawa za kienyeji.
Kama watu hao wapo
katika Dunia ya leo, hakika wanajidanganya, maana hatupo huko leo. Dunia ya
leo, kuweka ushirikina mbele hasa katika masuala ya michezo, ukiwamo mpira wa
miguu ni kuharibu zaidi mfumo na harakati zote za kimaendeleo.
Kwanini nasema hivyo?
Soka linahitaji muda wa kufanya mazoezi makali na wala sio kushindana kwa
tunguli. Kama ushirikina ni jambo jema katika soka, basi mikoa inayosifika kwa
uchawi leo hii ingetoa wachezaji wengi wa timu ya Taifa, au kuwajaza katika
timu zetu.
Kama upo uganga wa
kuleta tija katika michezo, kwanini Tanzania haishiriki michuano mikubwa,
ikiwamo Kombe la Mataifa ya Afrika, bila kusahau Kombe la Dunia?
Nasema hivi huku
nikiamini licha Dunia kubadilika zaidi, lakini baadhi ya wachezaji wetu
wanaamini uchawi. Ingawa huwezi kuwataja kwa majina, lakini hakika huo ndio
mtindo wao.
Kwasababu hiyo tu,
mfumo mzima unachafuka. Hatuzalishi wachezaji wanaotafuta au kulinda viwango
vyao kwa kuvuja jasho uwanjani zaidi ya wanaowaza miti shamba.
Huo sio mpango mzuri.
Na sio muarobaini wa mafanikio yetu katika viwanja vya michezo. Kwa kulijua
hilo, hakika siwezi kuvumilia kamwe na kuna haja ya kujifanyia marekebisho.
Sisi wadau wa
michezo, wanamichezo na wengineo tuwakosoe au kuwapa mawazo mapya vijana wetu
kwa kuwaaminisha kuwa uchawi sio njia ya mkato katika maisha yao.
Kuna haja ya
kupangilia muda wao. Kuhakikisha kuwa wanafanya mazoezi ya kutosha ili miili
yao kuwa imara zaidi. Wahakikishe pia wanakuwa na wataalaamu wa viungo. Vijana
hao lazima pia wajuwe ili wawe na nguvu, lazima wapangilie mlo wao.
Kama mchezaji anakula
chips kavu na soda moja, hata kama achanjwe mwili mzima, hawezi kushindana na
wachezaji wenye nguvu, kama vile Samuel Et’oo, Didie Drogba na wengineo
wanaowika katika soka la Afrika kwa timu zao za Taifa.
Hawa wachezaji haswa
wa Afrika Magharibi, ambao Ulaya wamekuwa na soko zaidi, hawagombaniwi eti
kwakuwa nchi zao ni wachawi sana, bali kwakuwa wamedhaamiria kuvuna fedha za
wazungu.
Mtu ambaye hapangilii
mlo wake, muda wake wa mazoezi kama ilivyokuwa kwa nyota wengine duniani, bado
hawezi kuwika duniani, japo nyumbani kwao kuna mkoba wa uganga.
Huo ndio ukweli wa
mambo. Yule mchezaji ambaye ana ndoto za kucheza soka kulipwa na bado akawa
hodari wa (misumari) uchawi, hakika anajidanganya na kupoteza muda wake.
Dawa ni moja tu.
Kufahamu hitaji husika, kujiwekea malengo kuanzia hatua ya chini hadi anapohitaji
mchezaji husika. Kinyume cha hapo Taifa litazidi kupata hasara bure.
Kwa sisi ambao
tumekuwa tukifuatilia soka kwa ukaribu zaidi, malalamiko ya baadhi ya wachezaji
kuwa wanarogwa yameshakuwa kawaida mno hadi kutia kinyaa.
Kwa mfano, nyota wa kulipwa
wa timu ya Yanga, Didier Kaavumbagu, alimtangaza hadharani Jerry Tegete kuwa
anamroga. Kauli kama hii ni chungu na endelezo la uchawi kwa soka letu.
Ingawa madai ya
Kavumbagu yanaweza kuchukuliwa kama uongo, lakini kwa soka la Tanzania, ni wazi
ushirikina upo na unapewa nafasi kubwa hata na baadhi ya viongozi wa timu hizo.
Kwa mfano, wapo
wanaoamini kuwa benchi la ufundi, lazima likamilike kwa kuundiwa pia mtu wa
kuhakikisha kuwa uchawi unafanya kazi ili washinde mchezo husika.
Tena mambo kama haya
hutokea zaidi kwa mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, timu kongwe zenye
‘madudu’ mengi mno. Utaona vioja vya kila aina, yakiwamo mayai viza au ndege wa
ajabu kurushwa angani.
Hatuwezi kwenda hivyo
waungwana. Siwezi kuvumilia kamwe, hivyo Shirikisho la Soka nchini (TFF),
lazima liwabane wote wenye kuendekeza vitendo vya ushirikina maana ni kaburi la
sokaa letu.
Kwa wale wasioamini
kuwa wapo watu wanaofanya ushirikina kwa soka la Tanzania, waanze kufuatilia
zaidi maisha ya wanasoka wetu, viongozi wetu na siku za mechi zao.
Utashangaa pale kipa
au beki anavyohaha kutaka kufukia uchafu wake uwanjani, akiamini ni silaha ya
kumfanya awike uwanjani, wakati ni uongo mtu na kuharibu kiwango chake.
Swali, unaweza kuroga
upate namba kwa wachezaji wenzako Tanzania, vipi ukienda kujaribiwa Manchester
United? Je, utahangaika katika Uwanja wa Old Trafford ili ufukie hirizi?
Acheni hizo, chezeni
soka, maana uchawi ungekuwa tija, mikoa inayoheshimika kwa ndumba ingetwaa
Kombe la Dunia au kuwa na klabu zinazonyakua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika au
Kombe la Shirikisho.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment