Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Addis Ababa, Ethiopia,
jana, Februari 23, 2013 kuhudhuria utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa
Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mpango huo unatarajiwa
kutiwa saini kesho Februari 24, 2013 na Wakuu wa Nchi kutoka Ukanda wa Maziwa
Makuu, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya
Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Burundi,
Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Mhe. Ban Ki Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt.
Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC) na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) watatia saini Mpango huo
kama mashahidi na wadhamini.
Mpango huo una nia ya
kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika kutafuta amani Mashariki ya
Kongo na ukanda wote wa Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango huo pia umetilia
maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano kati ya wakuu wa
nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa
Rais, Msaidizi,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Februari, 2013
No comments:
Post a Comment