MAMBO FULANI MUHIMU
Wapendanao wawili.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NIMEKUWA nikijikita zaidi kuandika makala zinazotokana na
maswali ya wasomaji wangu wanaoniunga mkono tangu kuanza kwa makala haya.
Nashukuru kwa hilo, maana kitendo cha kusomwa tu, kinanipa
nguvu ya kuendelea kuwapo katika kona hii inayokujia kila Jumamosi ikichambua
mambo mbalimbali ya kimapenzi.
Kwa siku kadhaa, nimekuwa nikiulizwa maswali yanayohusu
uaminifu wa wapenzi au wanandoa. Kwa mfano, yupo dada mmoja ambaye jina lake
sipo tayari kuliweka katika gazeti la Mtanzania la Dar es Salaam Tanzania, linalochapisha makala haya kila Jumamosi, aliniuliza hivi; mpenzi wangu sio muaminifu,
maana kila ninapokwenda kwake nasikia kashfa nyingi za kutoka kimapenzi na watu
wengine na nikimuuliza anajibu ndio amefanya nao na kuomba msamaha.
Hili lilikuwa swali lililotanguliwa na maneno mengi kutoka
kwa msomaji huyo wa Mambo Fulani muhimu. Jibu langu lilitanguliwa na swali,
wakati unasikia maneno hayo kutoka kwa watu, je umefanya uchunguzi wako na
kugundua ni kweli?
Nasikitika dada huyu alijibu ni kweli, hivyo mtu huyo si
muaminifu. Ana pepo la ngono, akichukulia kitendo cha kuishi mbalimbali na mtu
wake, maana wapo mikoa miwili tofauti.
Katika hali ya kawaida, kama mwanamume anakiri ndio tabia
yake ya kutoka kimapenzi na wanawake wengine, tena akasema bila woga kwa
mwanamke wake, basi ana udhaifu.
Na maneno yake wakati mwingine huyatoa kwa maana mbili; mosi
ni kuonyesha uhuni wake, au uanaume wake kama wanavyosema watoto wa mjini.
Pili, anaongea hivyo ili mwanamke huyo achaguwe la kufanya,
kuendelea kuwa nae au kuachana nae. Kwanini nasema hivyo? Kama kweli mwanaume
anakiri kutembea wanawake mtaani kwao kwa kumwambia mchumba wake, je, akisikia
yeye wanaume wanaotoka na mtu wake atachukua hatua gani?
Mara nyingi inapotokea hatua hii, mwanaume kujua wanaotoka
na mke, au mchumba wake, huvunja uhusiano wao. Kwa sababu hii basi, jibu ni
kwamba hakuna haja ya kumvumilia mwenye pepo la ngono kwa Dunia hii yenye
maradhi mengi.
Endapo umegundua mume au mchumba wako si muaminifu, ukamuuliza
na kukiri kosa, basi achana nae hasa kama tabia hiyo itaendelea kila siku.
Kwa kawaida, aliyetembea na msichana mwingine zaidi ya Yule
wake, kwa bahati mbaya kama wanavyomsingizia shetani kila siku, hakika hawezi
kurudia kila wakati. Yani kweli kila
siku unakosea kwa bahati mbaya? Yani kila
siku shetani?
Hapana na kuna haja ya kuangalia uhusiano wetu. Unapaswa
kutoa picha kamili ya uhusiano wako. Mwambie wazi, kama bado upo busy na
mihemko ya wanawake watu wa nje, basi fanya kwanza na ukichoka utaniambia.
Huo ndio ukweli, maana mwenye mapenzi ya dhati kwa menzake
hawezi kufanya uchafu kila siku ya Mungu na kumsingizia shetani na kuomba
msamaha.
Wakati mwingine lazima watu waangalie heshima zao, maana
inapotokea mpenzi wako, mume au mke wako anakuwa sio muaminifu, hata heshima ya
kutembea mtaani inapungua.
Kila unapofika, watu wanakushangaa au kukusindikiza kwa
vidole, wakiangalia uzuri wako, heshima yako na bado unayejidanganya kuwa
unampenda, yupo ‘busy’ na wapita njia.
Jiweke kando unapoona hakuna mabadiliko kwa mpenzi wako,
maana usipokuwa makini, utaambulia maumivu kila wakati, hasa kwa kuwabaini
wanaotembea, wanaofanya uchafu na mtu wako, ingawa wewe unajiheshimu.
Hii ipo zaidi kwa wanawake, maana wakati mwingine mfumo dume
unasababisha wao wakikutwa na watu wa pembeni kuachika na wao wanapowakuta wezi
wao kuombwa msamaha, wakifikiriwa ni wepesi kusahau na maisha kuendelea.
Mapenzi ni matamu lakini yanatesa kama uliyekuwa naye si
muaminifu kwako, ukizingatia kwamba atakupa wasiwasi wa kufikiria anachofanya,
hivyo kukupa ugonjwa wa moyo bure tu.
Jichunguze wewe na mtu wako kwa faida ya uhusiano wenu, ili
mapungufu yaliyojitokeza kuachwa kama kweli mna ndoto za kufunga ndoa kwa wale
wapenzi au wachumba.
Kinyume cha hapo, ni mateso na majuto maana uliyekuwa naye
anafanya sikukuu ya kutembea na watu wa pembeni kila siku ya Mungu.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment