Watatukoma leo hao African Lyon
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MABINGWA wa zamani wa Tanzania Bara, Yanga SC, leo inaingia
uwanjani kumenyana na African Lyon, katika mechi iliyopangwa kufanyika katika
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mbali na Yanga, timu nyingine zinazotarajiwa kupigwa leo ni
pamoja na Coastal Union ya Tanga, iliyokaribishwa na Kagera Sugar, katika
Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Toto African na Polisi Morogoro, Uwanja wa CCM
Kirumba Mwanza, JKT Oljoro na Mgambo, Mkwakwani, wakati Mtibwa Sugar na Ruvu
Shooting, wakicheza Uwanja wa Manungu, Turiani, mkoani Morogoro.
Mechi hizo zinaingia katika mvutano wa aina yake, hasa kwa
upande wa Yanga, inayoshika usukani mwa ligi hiyo, ambayo kwa sasa imefikisha
pointi 33, akifuatiwa na Azam FC, Simba SC na Coastal Union.
Mashabiki wa soka wa Yanga, wanazidi kuipa ugumu mechi hiyo,
hasa kwa kutaka kwao timu ishinde na kushika nafasi ya juu zaidi, jambo ambalo
hata hivyo litakuwa gumu kwa timu zote mbili.
Hata hivyo, Yanga inaweza kumkosa mchezaji wake, Mbuyi
Twite, aliyeumia katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki kati ya timu yake ya
Taifa ya Rwanda ilipocheza na Uganda, mjini Kigali.
Pamoja na kukosekana kwa mchezaji huyo, tayari benchi la
ufundi linaweza kumtumia beji wake Abdul Juma, atakayewavaa African Lyon, ukiwa
ni mchezo wa Ligi ya Tanzania Bara.
Katika mechi zote za leo, tambo mbalimbali zimesikikika,
kila mmoja akitangaza kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwa ajili ya
kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye patashika hiyo.
Coastal Union kutoka kwa Wagosi wa Kaya, hawa walienda
Mwanza kwa Ndege na kuwavaa Toto African ya jijini humo, juzi walikwenda mjini
Bukoba kwa basi, huku wakisema watafia uwanjani.
Hali kazalka Kagera Sugar nao wametangaza kuwachakaza wageni
wao wa ligi, Coastal, wakisema watautumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa
ajili ya kuwaonyesha soka la uhakika Wagosi wa Kaya.
Kwa upande wa Ruvu Shooting, JKT Oljoro, Toto Afrucan,
Mgambo Shooting zote zimepania kutoka na pointi zote tatu katika mechi za leo
Jumatano, hivyo kuongeza mvuto na ushindani kwenye mechi hizo.
Katika msimamo wa Ligi hiyo, Yanga SC ina pointi 33, sawa na
Azam FC, wakitofautiana mabao ya kufungwa na kushinda, wakati Simba wao wana
pointi 28, wakitoka sare mechi mbili za mzunguuko wa pili, huku wakishinda
mechi moja dhidi ya African Lyon kwa kuifunga bao 3-1.
No comments:
Post a Comment