Kutokana na ukatili waliofanyiwa wakazi hao wenye ulemavu wa ngozi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inakemea na kulaani vikali matukio hayo ya ukatili ambayo yanawanyima watu wenye ulemavu wa ngozi haki yao ya kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo kwa wananchi wengine. Wizara inamtaka kila mwanajamii kulinda na kuthamini uhai wa mtu mwingine ikiwemo kuheshimu sheria na haki za binadamu.
Ikumbukwe kuwa, vitendo hivyo vya kikatili siyo tu vinaathiri aliyefanyiwa ukatili, bali pia vinagusa na kuathiri maisha ya watu wengine katika jamii; na kuchafua sifa ya nchi yetu.
Aidha, Wizara inaitaka jamii kubadilika na kuachana na imani potofu ambazo zinahatarisha maisha na usalama wa watu wengine na ambazo zinarudisha nyuma jitihada za Serikali za kupiga vita ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na watoto. Wizara inawataka wananchi wote, kuwafichua wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa walinzi wa amani katika maeneo yao ili Serikali iweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa matukio hayo, na mengine ambayo yameripotiwa na vyombo mbalimbali likiwemo la utupaji wa watoto wachanga matukio ambayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda na kuripotiwa na gazeti la MTANZANIA la tarehe 13 Februari, 2013. Tukio lingine ni la mtoto Kaselemako Mpale (14) aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kasumulu Wilayani Kyela Mkoani Mbeya ambaye alichinjwa na baba yake mzazi Mpale Mbisa (35) kutokana na imani za kishirikina. Aidha, kijana Malba Hamisi(19) wa Wilaya ya Kishapu anayetuhumia kumuua bibi yake Mindi Dotto (70) kwa imani za kishirikina.
Kutokana na taarifa hizo za ukatili ambazo zimeripotiwa na vyombo vya habari, Wizara inapenda kupongeza jitihada zilizofanywa na vyombo vya habari vyote ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili unaofanyika katika jamii jambo ambalo limeisaidia Serikali kubaini na kufuatilia taarifa za ukatili mara vitendo hivyo vinapotokea. Aidha, ripoti hizo zimesaidia kuamsha ari kwa wananchi kuripoti matukio ya ukatili mara zinapotokea, jambo ambalo limesaidia kuwachukuliwa hatua za kisheria wale wote wanaobainika kuhusika na matukio hayo. Wizara inahimiza wananchi kuendelea kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na kupuuza imani za ushirikina katika kujiletea maendeleo yao.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara
No comments:
Post a Comment