https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, February 06, 2013

CCM kukutana Dodoma mwishoni mwa wiki

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kimepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma, utata umeendelea kugubika chama hicho kuhusu kushindwa kuunda Kamati Kuu kwa miezi mitatu sasa, linaripoto gazeti la Mwananchi linalochapishwa nchini Tanzania.
 

NEC itakutana kwa siku mbili mjini Dodoma Jumamosi hadi Jumapili bila ya kuwapo kwa Kamati Kuu ya chama hicho wala kuelezwa kama kuna ajenda ya kuundwa kwake.

Kwa kawaida vikao vya NEC vinatanguliwa na vikao vya sekretarieti ya CCM ambayo inawasilisha taarifa kwa Kamati Kuu ili kupanga ajenda kwa ajili ya NEC.

Hivi karibuni, gazeti moja la kila siku lilichapisha habari kuwa Kamati Kuu ya CCM ilikuwa tayari na ingetangazwa wakati wowote, na huenda ikawa moja ya majukumu ya kikao cha NEC Jumamosi.

Katika hali hiyo, CCM iliyotimiza umri wa miaka 36 jana, iliadhimisha sherehe hizo Jumapili iliyopita mjini Kigoma, bila ya kuwa na Kamati Kuu, ambayo ilitakiwa kukaa na kutathmini mafanikio na matatizo ya chama hicho. Imepita miezi mitatu tangu CCM ichague viongozi wake wa NEC na wale wa nyadhifa za juu, lakini ukimya umetanda kuhusu kuundwa kwa Kamati Kuu.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakuwa tayari kuweka wazi ni lini Kamati Kuu ya chama hicho itatangazwa.Nape akizungumza na Mwananchi jana alisema, Chama kitakapokamilisha taratibu kitatoa taarifa na sasa kiachwe kwanza.

“Tuliwaeleza tangu awali kwamba tutakapokamilisha tutatoa taarifa, sasa kiherehere cha nini,” alisema Nape na kukata simu.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliomba muda wa kuteua Kamati Kuu baada ya uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Novemba 10-12, mwaka jana mjini Dodoma.
Rais Kikwete alitoa sababu kuwa alishindwa kufanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati Kuu wakati ule kwa kuwa wengi wao walikuwa wageni kwenye NEC na yeye hakuwa anawafahamu vizuri.

Hatua hiyo, ya Rais Kikwete iliwashangaza wachunguzi wa masuala ya kisiasa, ukizingatia kuwa wagombea wa CCM huchekechwa na vyombo mbalimbali vya chama hicho.
Vyombo hivyo ni pamoja na Kamati ya Usalama, Kamati ya Maadili, NEC na Kamati Kuu.

Hata hivyo, wachunguzi hao walitafsiri kasi ndogo ya Rais Kikwete kuteua Kamati Kuu inatokana na hofu ya makundi yaliyogubika chama hicho.

Makundi ya watu wanaowania urais mwaka 2015 ndiyo yalitawala mchakato wa uchaguzi wa CCM na Jumuiya zake, huku kukiwapo taarifa kuwa wajumbe walio wengi walifadhiliwa na makundi hayo.

Makada wa chama hicho wanaotajwa kutaka kuwania urais ni pamoja na John Maghufuli, Edward Lowassa, Samuel Sitta na Bernard Membe

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...