SIWEZI KUVUMILIA
Msemaji wa Coastal Union, Edo Kumwembe
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA vitu kwenye mpira wa miguu vikikutokea, hasa kwa wale
wanaowekeza au kudhamini timu mbalimbali, matumbo yao huuma.
Wadhamini wa Coastal Union wanavyoonekana pichani.
Hata hivyo
haitoshi, huchanganyikiwa na kutembea wakisema peke yao, wakikumbuka fedha zao
zinamwagika na hakuna ushindi unaopatikana.
Bila kuficha, suala hili lilimsababisha mmiliki wa zamani wa
African Lyon, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji ‘Mo’ aipige
bei timu hiyo.
Hakuona maslahi zaidi ya kumpa presha na hasara ya fedha za
kuihudumia, kuanzia kambi, safari na mishahara ya wachezaji, bila kusahau
viongozi wao, kama vile Mwenyekiti, Katibu Mkuu na benchi la ufundi.
Kwanini nasema hivyo; hakika najikuta siwezi kuvumilia kuona
mwenendo mbaya wa timu Wagosi wa Kaya, Coastal Union inavyopata matokeo mabaya
licha ya wadau kutoa misaada mingi, bila kusahau ufadhili wa Nassoro Binslum.
Kwa miaka kadhaa sasa, nashangazwa na taarifa za Coastal
Union kupanda ndege kuelekea kwenye mchezo wao na Toto African ya Mwanza.
Katika mchezo huo uliochezwa Jumamosi iliyopita,. Timu hizo zilizotoka sare ya
bila kufungana.
Kwanini? Ingawa kufungwa, kushinda au sare ni matokeo ya
kawaida kwenye mchezo wa soka, lakini kwa jinsi Coastal inavyohudumiwa, nilijidanganya
kwamba sasa itakuwa tishio walau kushika nafasi ya kwanza kama sio ya pili.
Timu hiyo ya jijini Tanga, ndani ya ngome ya Mkuu wa Mkoa
Tanga, mama Chiku Gallawa, sasa inaishi kama zinavyoishi nyingine, hasa Simba,
Yanga, Azam, maana nayo inajiweza.
Huwezi kuona Coastal ya leo inalalama kushindwa kwenda mikoani kwa
kukosa nauli.
Wakati ikienda Mwanza kwa ndege, tayari uwezekano wa
kuwafikisha kwa basi wachezaji na viongozi wao hadi Bukoba kwa basi
ulishaandaliwa, hasa kwasababu ni karibu na
vijana hawawezi kuchoka, kuelekea mchezo wao na Kagera Sugar.
Hakika siwezi kuvumilia. Inauma, maana kama Coastal haifanyi
vizuri leo, ni lini tena itafanikiwa kuonyesha soka la uhakika, ishinde na kuwa
tishio zaidi. Hata kama ishindwe kunyakua ubingwa, lakini nafasi ya pili au ya
tatu ni muhimu.
Uwezo huo wanao, maana wapo vijana wenye uwezo mzuri wa
kucheza soka, kama vile Shaban Kado, Ismail Suma, Othman Tamimu, Phillip
Mugenzi, Mbwana Khamis, Jrrry Santo, Joseph Mahundi, Razak Khalfan, Daniel
Lyanga, Mohamed Sudi, Selemani Kassim, Rajabu Kaumbu, Gerald Lukindo, Ibrahim
Twaha, Gabriel Barbosa, Hamad Juma, Khamis Shengo na wengineo wanaopigania
namba katika kikosi hicho cha Coastal Union.
Hii ni aibu kubwa, maana wachezaji wameshindwa kabisa
kucheza jihadi uwanjani ili kuleta matumaini kwa wadau na mashabiki wao.
Coastal Union huwezi kuifananisha na timu ndogo ndogo kwa sasa, ikiwapo Toto
African pamoja na timu za Polisi.
Inapofikia kuendelea kukaa nafasi ya nne, tena kwa matokeo
yasiyokuwa na mashiko, ni wazi kupanda juu zaidi itakuwa ndoto. Nasema hivyo
kwasababu ligi inazidi kuwa ngumu, hivyo hakuna timu itakayotaka kufungwa
kirahisi.
Huu ndio wakati wa vijana kuonyesha kwanini wao wanaitwa
wachezaji wa mpira wa miguu. Wafie uwanjani ili wenye kutoa fedha zao, wenye
kulipa viingilio vyao kuendelea kupata moyo huo na sio kufanya mambo
yasiyoeleweka.
Hali ikiendelea kuwa hivi, ni wazi wenye moyo wao
watashindwa. Tatizo kubwa la ligi yetu ipo kwenye safari, hasa za mikoa ya
Mwanza na Bukoba. Kwa mfano Coastal kutoka Tanga hadi Mwanza na Bukoba, hakika
fedha za uongozi tu hazitoshi kamwe.
Ndio hapo wadau, akiwapo BinSlum anapoonyesha umahiri wake
kwa vijana, ndio maana anamwaga fedha zake, ingawa tunaamini anashirikiana na
wanaopenda maendeleo ya Coastal Union.
Labda niulize swali, hawa vijana wa Coastal Union wanataka
nini tena? Kama wanaishi maisha mazuri, kama wanavyoishi Simba, Yanga, Azam
nini tena zaidi? Wachezaji hawa lazima wajuwe wana deni kubwa na timu hiyo.
Mashabiki wa soka wa Tanga nzima hawataki kuona visingizio
visivyokuwa na mashiko, ukizingatia kuwa kila kitu vijana hawa wanapata. Mikoa
ya karibu yote, ikiwamo Dar es Salaam, Morogoro na Arusha basi zuri tu wanalo.
Kwa timu kama Coastal, hakika inahitaji kufanya bidii,
kujituma kwa nguvu zao zote, ili washike walau nafasi ya pili na kupata nafasi
ya kucheza Kombe la Shirikisho katika hali ya kuonyesha makali yao na kuuza
majina yao.
Wachezaji wanaangalia Simba na Yanga, kwasababu wanapata
nafasi ya kuoanda ndege mara kwa mara wanapokwenda nje ya nchi, lakini zamu
hiyo sasa ipo kwa Azam FC.
Kama timu nyingine ndogo, ikiwamo Coastal ikishika
namba mbili, walau sasa tunaweza kubadilisha fikra zetu kuwa mazuri yote yapo
kwa wakongwe, wakati si kweli.
Ndio maana nasema, wachezaji wa Coastal Union wanahitaji nini
zaidi? Au wanataka roho za wadau na mashabiki wao? Hii presha wataiacha lini?
Ni lini watacheza soka la jihadi kwa timu zote?
Katika kulisema hilo, naamini
uongozi utakaa chini na wachezaji wao kuliangalia tatizo liliopo, huku nikiomba
Mungu iendelee kubaki kwenye ligi kwa kutimua mizigo ndani ya timu.
Uongozi ndani ya timu hiyo upo chini ya Hemed Hilal (Aurora)
kama mwenyekiti, huku nikiamini kuwa mwendo huu mbovu unamuumiza kichwa kama
wanavyoumia mashabiki na wadau wao wanaoisaidia visenti vyao ili kuiwezesha
Coastal Union.
Hakika siwezi kuvumilia, maana kama kila kitu timu inapata,
wanataka nini tena?
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment