Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
Na Rahimu Hemed, Dar es Salaam
INASIKITISHA kuona Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayumbishwa
na makada wake wanaotajwa kuwa na dhamira ya kugombea Urais kwa tiketi ya Chama
chao, mwaka 2015.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernald Membe
Wana CCM hawa wamekuwa wakitumia nguvu kubwa katika kuweka
sawa mitandao yao kwa ajili ya kujiweka pazuri katika kuelekea ‘ubwana mkubwa’
huo ifikapo mwaka 2015, ambapo mchakato wake umezidi kupamba moto.
Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa
Ni kitendo cha kuchanganya kichwa na kinachoweza kumtoa
Mtanzania machozi, kuona kumbe wapo watu ambao wanachowaza wao ni kuongoza tu,
hata kama hawana jipya.
Mtu hana dhamira wala utu moyoni mwake, lakini inashangaza
kuona anafanya kila awezalo kujifagilia yeye na watu wake. Kwa bahati mbaya,
baadhi yao, wanachoangalia wao ni mtandao wao kuneemeka hata kama hawana tija.
Kwa mfano, katika Chama Cha Mapinduzi CCM, yapo majina
makubwa yanayotajwa kuwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015, ambao ni Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Samuel Sitta, Edward
Lowassa na wengineo.
Ingawa hawajatangaza hadharani ukiacha, Sitta ambaye aliwahi
kukaririwa akijitangaza kuwa anafaa kuwa Rais wa Tanzania, lakini dhamira yao
inaonekana.
Mtu kama Lowassa, huwezi kuacha kumuona katika vyombo vya
habari kila siku, akidaiwa kusema hili au kutoa kile katika shughuli za kidini,
hasa kwa Wakristo wanaomualika mara kwa mara katika sherehe zao.
Najua kuwa yoyote anaweza kuwa Rais wa Tanzania, lakini
wasiwasi wangu ni hii nguvu kubwa inayotumiwa na baadhi yao katika kuelekea
kiti hicho, ambacho sasa kipo chini ya Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Katika Chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, tuliona jinsi
makada hao walivyotunishiana misuli, huku baadhi yao pia wakitajwa kumwaga
fedha katika kuimarisha makundi yao.
Ni jambo la ajabu mno. Wanachama hao wa CCM, katika kuelekea
kwenye mbio hizo, wamesababisha hadi uhasama kwa makundi yao, hasa pale wapowapigia
debe kwa njia mbaya na kuleta malumbano ya aina yake na hata kurushiana maneno
machafu.
Ni kweli usiopingika kuwa kila chama chenye uhai, ni lazima
kuwe na uhasama katika kuelekea jambo moja la maana; lakini si kama
inavyofanywa sasa na wafuasi hao wa CCM.
Hawa wameweka mbele tama ya kushika dola na sio kuwaongoza
Watanzania wanaosumbuliwa na matatizo lukuki, ikiwamo elimu duni, afya ya
kuunga unga, njaa na shida ya maji katika maeneo mengi ya yanayounda Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ukienda kwenye mitandao ya kijamii utakutana na lugha zenye
ukakasi, vijana au wafuasi wa mabwana wakubwa hawa jinsi wanavyoonyeshana
umwamba kwa kutukanana.
Utu wa Mtanzania sasa umetoweka kabisa. Nguvu kubwa imewekwa
katika kuitaka nafasi hiyo ya Ikulu. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliwahi kulikemea jambo hili.
Alisema siku zote mtu anayeng’ang’ania kwenda Ikulu anafaa
kuogopewa kama ukoma. Akasema, “Ikulu ni mahali patakatifu.” Kwamba mahala pale
hapahitaji mchezo na mzaha.
Yule anayetaka nafasi hii lazima ajipime kama kweli ana
uwezo huo kwa kuangalia na kubuni mbinu za kuinua uchumi wa Taifa kwa vitendo
na sio porojo, au kuangalia namna ya kuwajaza mapesa, maisha bora kundi lake
kwa kuwateua kwenye nafasi zenyemguso.
Hili haliwezi kukubalika hata mara moja. Kwa kuwa Tanzania
ni yetu wote, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuangalia jinsi baadhi ya wanasiasa
wetu, hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanavyotaka nafasi hiyo ya Urais kwa
uroho kupita kiasi.
Nikiwa kama Mtanzania na ninayefuatilia siasa, nimekuwa
nikifanya utafiti wangu mara kwa mara na kugundua kuwa baadhi ya wilaya au
mikoa, imeathiriwa mno na siasa za Mtandao.
Unaweza kuona Mkuu wa Wilaya hapatani na Mbunge, hasa
kwasababu watu hawa wawili wanapingana katika kambi zao. Hili si jambo zuri
hata kidogo na hakika linastahili kupingwa vikali kwa ajili ya maisha bora kwa
kila Mtanzania.
Kama sio makundi nini kingine? Mkuu wa Wilaya anateuliwa na
Rais, yani anakuwa mwakilishi wa Rais. Lakini mbunge yeye anachaguliwa na
wananchi, lakini kwa bahati mbaya, wabunge wengi huingia kwenye mtandao kabla
na baada ya Urais.
Kwa mfano, katika Uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Kikwete
alirejea tena madarakani kwa kupewa nafasi na Watanzania wanaompenda na
kumheshimu, lakini ukweli ni kwamba wale waliokuwa na dhamira hiyo ya kupokea
kijiti chake hawakurudi nyuma zaidi ya kujipanga, wakiamini kuwa miaka mitano
sio mingi.
Hivyo basi, waliogombea ubunge na kupata wakiwa kwenye kundi
hilo, waliendelea kuwa kwenye mtandao wao na walioshindwa, bado waliungwa mkono
kwa kusaidiwa kila kinachostahili.
Katika siasa za Tanzania, wapo watu ambao wanagombea wao
lakini bajeti inatoka kwa wengine. Kwa mtindo huu, utaona jinsi mbio hizi
zinavyoweza kuitikisa nchi siku za usoni.
Kwanini? Haya yote yanaletwa na dhamira ya kuwatetea
Watanzania kutoka kwenye njaa hadi kupata ahueni na maisha bora au wanataka tu
kujinufaisha wenyewe?
Fedha hizi zinazomwaga na makada hawa kutoka CCM zitarudi
kwa mtindo gani na wapi zinapotoka? Urais si jambo dogo. Kwa wanaokwenda Ikulu
kuwaongoza Watanzania hakika Ikulu ni mzigo.
Inashangaza kama wengineo wanakuwa na nia ambayo si nzuri,
ndio maana wengineo wameamua kuzalilisha watu wao, jamii yao, ndugu au binadamu
wenzao kwasababu za kijinga kabisa.
Serikali ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake, JK, inajua jinsi
inavyoyumbishwa na makada hawa. Ndio, maana wachambuzi wa mambo ya kisiasa
wanasema kutendo cha Kikwete kutowapendekeza wanaotajwa kuwania urais mwaka
2015 kwenye Kamati Kuu CC ni dalili za kuwapunguza makali baadhi yao.
Katika Kamati Kuu, majina ya Membe, Lowassa,
Sitta hayakuwapo, hivyo kuwanyima nafasi ya kuendeleza makundi yao ndani ya
Kamati hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa serikali ya CCM.
Pamoja na hayo, bado wataalamu wa mambo wanaendelea
kuchambua kuwa, mkakati huu wa Kikwete ulikuwa hatua muhimu kwake kama kiongozi
wa chama baada ya kukwama kuzuia makundi kung’ara katika chaguzi zilizopita ambapo
wafuasi wa Edward Lowassa waliibuka kidedea kuanzia katika NEC, mikoani na
Jumuiya za chama hicho, ambapo kwa siasa za Tanzania, inaweza kuwa chapuo kwa
Waziri Mkuu huyo wa zamani, aliyelazimika kujiuzulu.
Kila mmoja alishuhudia baada ya kumalizika Uchaguzi
wa wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kuwa waliochaguliwa
walikuwa wageni, hivyo binafsi alikuwa hawafamu vizuri.
Kwa jinsi hali ya mambo inavyoendelea, hatua hii ya
Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi, bila
kutajwa kuwa ni ya Lowassa, Membe au Sitta, ingawa ukaribu wa familia ya
Kikwete, ikiongozwa na mtoto wake, Ridhwani na mama yake, Mama Salma Kikwete,
watu wanabashiri kuwa wapo kambi ya Membe, ambaye kwa hakika anahitaji nguvu za
ziada ili apitishwe na chama chake kuwania urais huo kama ni kweli ana lengo
hili.
Inajulijulikana umuhimu wa Kamati Kuu, maana hatua
ya Kikwete kutopendekeza majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania
ujumbe huo, inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja
tu ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki, hivyo
ikawa rahisi kujipigia chapuo, ukizingatia kuwa kila linalojadiliwa nao
watakuwapo.
Hayo yote ni muendelezo wa nguvu kubwa ya wanasiasa
hawa wanaowania nafasi ya Urais wa Tanzania, ingawa bado wamekuwa kimya,
kwasababu wanajua kuwa sio picha nzuri kujitanga mapema kuwa wana lengo la
kuwaongoza Watanzania.
Nguvu kubwa hii inaleta picha gani? Ni kweli
wanataka kuwaongoza Watanzania au wanataka kujineemesha wenyewe? Maswali kama
haya yanahitaji yajikite katika vichwa vyetu, tuwaze na kufikiria mara mbili
kwa ajili ya nchi yetu.
Nimejikita zaidi kwenye siasa za CCM kwasababu
purukushani zao ni nyingi na pia wao ndio walioshika dola. Ingawa upinzani upo
na una nguvu kubwa, ila kwakuwa fedha na nguvu zinazotumiwa na wanasiasa kutoka
Chama Tawala, basi ni wajibu wetu kuhoji na kuwabana katika matumizi hayo
yasiyokuwa na tija.
Pamoja na matumizi hayo, pia wafuasi hao, makada hao
wa chama tawala lazima wajuwe watashindana huko kwa kadri ya uwezo wao, lakini
bado karata itabaki kwa wapiga kura, Watanzania ambao kwa hakika wanalingia
upinzani kuimarika na kuwa na imani kubwa na viongozi wa vyama vya upinzani kwa
namna moja ama nyingine.
Leo hii ambapo Chama Cha Wananchi CUF, Chadema, TLP hakika
heshima zao ni kubwa na wanapendwa na Watanzania, hivyo hawa ambao wanaona
wamezaliwa ili wawe marais, hakika kazi wanayo.
Mbio hizi, matumizi mabaya ya fedha kwa ajili ya kuneemesha
ngome zao, zinazua maswali kede kede kwa watu wenye uelewa wao, dhamira yao na
machungu ya kweli ya kuhoji kwanini wanasiasa hawa wanatumia nguvu kubwa
kuutaka urais wa Tanzania?
Wanataka nini hawa? Kama swali hili ni la uongo, basi lipo
karibu na ukweli, ndio maana pamoja na kusemwa sana, kutajwa katika harakati
hizo, wakibanwa hawakanushi, zaidi ya kusema urais sio dhambi.
Mungu ibariki Tanzania.
0766 453862
No comments:
Post a Comment