https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, February 18, 2013

Polisi Handeni wakamata wanafunzi sita waliowapiga walimu wao

Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Na Mashaka Mhando, Handeni
JESHI la polisi wilayani hapa, linawashikilia wanafunzi sita wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Handeni kufuatia vurugu walizofanya ikiwemo kumpiga mwalimu pamoja na kiranja wa shule hiyo.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Tanga, SSP Juma Ndaki, zinasema tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita baada ya wanafunzi hao kuchukizwa na adhabu aliyopewa mwanafunzi mwenzao Mussa Hussein ambaye alipewa adhabu na mwalimu wao aliyefahamika kwa jina moja la Kazi, kufuatia kitendo chake cha kuvaa viatu vya wazi.

Chanzo cha mwanfunzi huyo kupewa adhabu hiyo ilitokana na mwalimu huyo kumtoa katika mstari mwanafunzi huyo akiwa amevaa viatu vya wazi lakini katika purukushani ya kumweleza mwanfunzi huyo alionesha kama anataka kupigana na mwalimu huyo ambapo wakati mwalimu amemshika kwa ajili ya kumuonya kitendo chake hicho, alimkwaruza na kucha shingoni.


"Mwalimu Kazi alipokuwa amemuuliza kwanini umekuja shule na viatu vya Wamasai (Kanda mbuga zinazovaliwa na watu jamii ya wafugaji-Wamasai) Mussa akachukia akaanza kubishana na Mwalimu huyo...Mwalimu alipoona mwanafunzi anamjibu jeuri akamshika kama anataka kumpiga lakini mwanafunzi naye akajibu kwa kukinga ngumi, walipokuwa wakishikana mwanafunzi akachubuliwa na kucha la mwalimu akawa anatoka damu shingoni," alisema mmoja ya mwanafunzi aliyeeleza kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Aliwataja wanafunzi ambao wanashikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Ramadhani Idd Mrisho, Mwinjuma Habibu, Mussa Hussein, Athumani Yusuph, Hassain Daffa na Athumani Salimu Hassain ambao siku ya tukio hilo walimshambuliwa mwalimu huyo kwa mawe na walimu wengine hadi wakakimbia kwenda kujifungia kwenye ofisi ya Mkuu wa shule, kujisalimisha.

Diwani wa kata ya Chanika Athumani Mwinshashi, alipoulizwa alikiri kutokea tukio hilo ambalo alisema limesababishwa na wanafunzi hao kuleta vurugu na uongozi wa shule kuwafukuza kutokana na kukosa nidhamu hatua ambayo ilipelekea wazazi wa watoto hao kupeleka malalamiko yao kwa ofisa mtendaji kata Rose Semazua.

"Ni kweli lilitokea tukio hilo na wanafunzi hawa walisimamishwa sasa wazazi walipeleka malalamiko kwenye ofisi ya kata kuomba watoto wao wakaombewe ili warudi shuleni waendelee na masomo...Sasa tuliwatuma Ofisa Mtendaji wa kata, Mratibu Elimu Kata (MEK) na Mama maendeleo ya jamii waende kuwaombea kule shuleni," alisema diwani huyo.

Alisema hata hivyo, wakati viongozi hao wa kata wakiwa shuleni Ijumaa Februari 15 wakijadiliana na walimu shuleni hapo ili wawarejeshe shuleni wanafunzi hao, kabla hawajafikia makubaliano, polisi wa kituo cha Handeni waliingia shuleni hapo na kuwakamata na kuwapeleka kituoni ambako walilala.

Alisema baada ya mwalimu Kazi kushambuliwa na wanafunzi hao alikwenda polisi kufungua jalada la mashitaka kuhusu kufanyia fujo ikiwemo kipigo cha kudhuru mwili na akiwemo kiranja wa shule aliyefahamika kwa jina moja la Asharaf ambaye alidai alipigwa vibao, ngumi na mateke na Athumani Hassain, naye alifungua jalada la mashitaka.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Tanga, SSP Ndaki alikiri kutokea kwa tukio hilo na wanafunzi hao kulala kituo cha polisi, lakini alisema walishauri wazazi wa wanafunzi wakae na walimu walijadili na kuona namna gani watalitatua kwa maslahi ya wanafunzi hao ili waweze kusoma kutokana na kwamba mwaka huu ndiyo watamaliza elimua yao ya sekondari.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...