Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya The African Stars Twanga Pepeta, Asha
Baraka, amesema hakuna bendi ya kushindana na wao, kutokana na ukongwe wao
pamoja na umahiri wa vijana wake wanaofanya makubwa hapa nchini.
Twanga moja ya bendi zinazofanya vyema katika tasnia ya
muziki wa dansi nchini, leo inafanya shoo yake katika viwanja vya Leaders Club,
Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,
Asha alisema bendi yao inafanya vyema katika
ulingo wa muziki wa dansi, hivyo hakuna mwingine anayeweza kusogelea mafanikio yao, hasa yakichangiwa na
wanamuziki na mashabiki kwa ujumla.
Alisema kwa miaka zaidi ya 11 Twanga Pepeta imekuwa ikiungwa
mkono na wadau wote, hivyo hakuna anayeweza kuwafanya washindwe kuendeleza
harakati zao kwa ajili ya kujiweka kileleni katika kona ya muziki wa dansi
nchini.
“Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zinazofanya vyema hapa
nchini kutokana na umahiri wa wanamuziki wote waliokuwapo kundini na wenye
machungu ya kuipaisha juu zaidi, ingawa ushindani upo kwa kiasi fulani.
“Naamini hakuna anayeweza kuiangamiza bendi yetu hata kama
wapo wenye lengo hilo,
ndio maana wamekuwa wakipita huku na huko, hivyo nadhani hakuna kinachoweza
kuturudisha nyuma kwa mikakati tuliyopanga,” alisema Asha.
Twanga Pepeta imesheheni wanamuziki mahiri, akiwamo Luiza
Mbutu, Dogo Rama, Salehe Kupaza (Mwana Tanga), Kalala Junior, Badi Bakule,
Amigo Ras na wengineo wanaofanya vyema katika kona ya muziki wa dansi nchini.
No comments:
Post a Comment