Haijawahi kutokea Tanga nzima
Watu wagombania picha kaburini
Mama wa marehemu, Sharomillionea katikati akilia kwa uchungu kwenye msiba wa mwanae.
Na Kambi Mbwana, Muheza
NOVEMBA 28 ilikuwa ndio hitimisho la maisha ya duniani ya
msanii wa vichekesho hapa nchini, marehemu Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea.
Picha ya juu na chini, waombolezaji wakilia kwa uchungu katika msiba wa Sharomillionea.
Sharomillionea alizikwa katika makaburi ya kijijini kwao
Lusanga, wilayani Muheza, mkoani Tanga, huku maelfu ya watu wakijazana eneo
lote la mtaa yaliyokuwapo makazi ya mama yake msanii huyo aliyekufa huku msemo
wake wa ‘Oh Mama’ ukitamba.
Sharomillionea pia alitunga misemo mingi ukiwamo huu wa
‘Umebugi Men’, hivyo kuonyesha yeye ni msanii mahiri na mwenye uwezo wa
kubadilisha aina ya sanaa ya uchekeshaji kutoka kuvaa vinyago hadi mtu msafi.
Kwa miaka kadhaa sasa, baadhi ya watu waliamini kuwa ili mtu
acheke ni lazima awe amevaa nguo chafu chafu, lakini msanii huyo kutoka Muheza
alibadilisha aina hiyo kwa kuigiza kama mtu
mwenye uwezo wa kifedha, akivaa nguo za thamani na hata kuweka plasta sehemu za
uso wake, akijiita Sharomillionea.
Tunda Man na Timbulo wakiwa kwenye nyuso za majonzi katika msiba wa Sharomillionea
Kwa wanaofuatilia soko la sanaa hapa nchini, miaka miwili
iliyopita kulikuwa na ugomvi kati ya msanii Bob Junior na Sharomillionea
wakigombania jina la Sharobalo, maana mwimbaji huyo wa Nichumu, yeye alijiita
Rais wa Masharobalo.
Kuonyesha kuwa yeye ni mkali wa sanaa, marehemu
Sharomillionea alibadilisha haraka na kulijenga jina alilofia nalo na kuacha
kabisa malumbano na msanii huyo wa Bongo Fleva.
Mwili wa Sharomillionea ukitolewa chumba cha maiti kwa ajili ya kupelekwa nyumbani kwao Lusanga, kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika Jumatano ya wiki iliyopta.
Katika maisha yake ya duniani, Sharomillionea anakumbwa na
wengi kutokana na kuishi kwa upendo na watu wengi. Bila kuangalia thamani na
umaarufu wake, Sharomillionea hakusita kupokea simu ya mtu yoyote, zikiwamo za
waandishi wa habari.
Jambo hilo liliwafanya watu
wengi waache makazi yao
na kumiminika wilayani Muheza kwa ajili ya kumzika marahemu Sharomillionea.
Mazishi yake haijawahi kutokea katika historia ya Mkoa mzima wa Tanga nchini Tanzania.
Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, mwenye kitambaa kichwani, akitoa maelekezo katika Hospitali ya Teule, ulipokuwa mwili wa marehemu Sharomillionea.
Wasanii mbalimbali walikuja kushiriki mazishi ya kijana
mwenzao pamoja na mashabiki walioshindwa kujizuia kulia au kuzimia na
kusababisha huduma ya kwanza kutumika sana
katika msiba wa Sharomillionea.
Nguli wa uchekeshaji hapa nchini, King Majuto, wakati wote
wa msiba huo alikuwa kimya kwasababu ya kujilinda, maana presha yake ilipanda.
Dakika za mwisho wa mazishi ya Sharomillionea, King Majuto alizungumza kidogo
kwa kusema kuwa hatatokea tajiri kama Sharomilliona hapa Tanzania.
Marehemu Sharomillionea enzi za uhai wake.
“Hatatokea Sharomillionea mwingine na mimi nikamsifia, maana
huyu jamaa alikuwa ni zaidi ya msanii wa uchekeshaji duniani aliyekuja
kuibadilisha jamii kabisa na kuacha kuigiza wakiwa wachafu au wamevaa vitumbo.
“Hata mimi wakati mwingine nilikuwa naigiza kama
sharomillionea katika filamu mbalimbali nilizocheza na Sharomillionea, hivyo
kwakweli nina uchungu sana
na sijui sanaa itakuwaje katika nchi yetu,” alisema Majuto.
Mazishi ya Sharomillionea yalifanyika kwa mujibu wa dini
yake ya Uislamu unavyotaka, hivyo watu wengi walikuwa wakilalamika, hasa
kutokana na lengo lao la kuaga mwili wa mpendwa wao aliyekufa kwa ajali ya gari
lenye namba za usajili T478 BVR Toyota
Harrier kijiji cha Songa Kibaoni, Kata ya Kwefungo, wilayani Muheza, mkoani
Tanga.
Jambo hilo
la kulazimisha kuaga mwili wa Sharomillionea lilisababisha Mkuu wa Wilaya ya
Muheza, Subira Mgalu kuingilia kati na kupangua kabisa mawazo hayo, hasa baada
ya kukuta watu wamevamia chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Teule
Muheza.
“Jamani sio tu tumeachwa na ratiba yetu, lakini pia dini ya
kiislamu haiuruhusu watu kumuaga marehemu kwa idadi yote mliopo hapa, hivyo
naomba wanawake wote, nikiwapo mimi tuondoke tuelekee nyumbani kwenye msiba na
kuwaacha wanaume wamuandae ndugu yetu.
“Sisi wanawake tunatakiwa kubaki nyumbani, kule kuna kazi
nyingi zinazohusu msiba huu, hivyo sio vizuri kuja hapa kwa ajili ya kuaga
mwili wa mpendwa wetu Sharomillionea, ingawa najua kila mtu ameguswa na msiba
huu,” alisema Subira huku akiwa kwenye presha ya hali ya juu.
Kutoa kauli hiyo, tayari lilikuwa ni tamko la kiserikali,
hivyo kusababisha polisi sasa wajiandae kuwaondosha watu hata kama
hawataki na kupisha taratibu nyingine zifanywe za kuutoa mwili wa marehemu
hospitalini hadi nyumbani kwao Lusanga kwa mazishi.
Saa tano mwili wake ulitolewa kwa utaratibu wa wasanii
wenzake hasa wale waliochelewa kufika Muheza, akiwamo H-Baba, Soprano na
wengineo kuingia sasa kwenye chumba cha kuhifadhia na kumtoa mpendwa wao kwa
ajili ya kumuingiza kwenye gari lililoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kuubeba mwili wa marehemu.
Utaratibu huo ulisababisha wasanii hao washindwe kuvumilia,
hasa Mussa Kitale, ambaye wakati wote wa usiku wote wa Jumanne na juzi Jumatano,
kijana huyo alikuwa analia tu kila baada ya dakika chache.
“Yani kweli Sharomillionea unaondoka na kutuacha wanao
katika hali kama hii? Kwanini,” yalikuwa ni
maneno yanayojirudia kutoka katika kinywa cha Kitale, mmoja wa wasanii wa
uchekeshaji anayeigiza mara kwa mara na Sharomillionea.
Kitale na Sharomillionea wamecheza filamu nyingi mno. Baadhi
ya filamu hizo ni pamoja na pamoja na Mtoto wa Mama, Porojo, matoleo yote ya
Vituko Show, More Than a lion, Sharomillionea na nyinginezo zinazofanya vizuri.
Katika kuonyesha kuwa watu walikuwa wengi katika msiba huo,
makaburini kila mmoja alishika chepe mara moja kwa ajili ya kufukia kaburi la
nyota huyo, huku wadau wengi wakikosa nafasi hiyo kwasababu ya mkanyagano wa
waliokuwa wakihitaji nafasi hiyo adimu.
Baada ya kumaliza kuzika na kutoa dua zote, wasanii wenzake
walianza tena kumuombea mpendwa wao kabla nao ya kuliacha kaburi la marehemu
Sharomillionea likigombewa na mashabiki na mashabiki kupiga picha.
Tukio la picha za kupiga kaburi lililoendeshwa na mashabiki
bila kuwekwa utaratibu huo, liliendelea hadi Gazeti la Bingwa linaondoka katika
eneo la mazishi ya msanii huyo kipenzi cha wengi, wakiwamo wanawake na watoto.
Katika mazishi hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye alikuwa miongoni mwa waombolezaji, akiwa
sambamba na viongozi wote wa CCM Mkoa, wabunge na viongozi wengine wa chama na
serikali.
Sharomillionea alizaliwa Oktoba 26 mwaka 1985 Magomeni
jijini Dar es Salaam na kukulia kijijini Lusanga, wilayani Muheza mkoani Tanga,
ambapo ndipo nyumbani kwa mama yake.
Baada ya kumaliza elimu ya msingi kijijini kwao Lusanga,
kijana huyo alikwenda jijini Dar es
Salaam kutafuta maisha yake, ikiwamo sanaa ya
uigizaji, ambayo baadaye aliibukia tena katika kipaza sauti, akiimba kwa
kiwango cha juu.
Hadi anafariki, Sharomillionea alikuwa kwenye mipango ya
kuingiza sokoni albamu yake ya muziki, ikiwa ni kuonyesha kuwa ni zaidi ya
wasanii Tanzania.
Katika maisha yake, Sharomillionea hakusita kuonyesha hisia zake kwa mkoa mzima wa Tanga.
“Naipenda sana
Muheza na Tanga kwa ujumla. Mafanikio yangu sasa yametokana na moyo wa uzalendo
unaonyeshwa na watu wote wa Tanga,” hizi zilikuwa kauli zilizotolewa na
Sharomillionea kila wakati alipozungumza na vyombo vya habari.
Katika hali ya kushangaza ambayo hata hivyo haijaendelea,
jijini Dar es Salaam
kulikuwa na malumbano kutoka kwa wasanii wa Bongo Movie waliosema kuwa hakukuwa
na maana ya kunyenyekea msiba wa mtu ambaye hakuwa Bongo Movie.
Kauli hizi zilitokana na wasanii hao kuona Sharomillionea
akikana kuwa miongoni mwa kundi hilo, zaidi ya
kusema yeye ni comedy na hawezi kuwa kwenye kundi hilo linalojumuisha wakali wengi, akiwamo
Ray, JB na wengineo.
Hata hivyo kauli hizo ziligawanya wasanii wote wa kundi hilo na wengine kuanza
safari ya kuelekea Muheza tangu jumanne kwa ajili ya kufanya mazishi ya kijana
wao. Hata hivyo, mgawanyiko huo ulikoma baada ya kushuhudi umati wa wasanii
kuja Tanga, wakiwamo wa Bongo Movie, akiwamo Vicent Kigosi Ray, Wema Sepetu na
wengineo.
Mbali na Bongo Movie, pia viongozi wa Baraza la Filamu
Tanzania TAFF nao walikuwapo msibani wakiongoza taratibu zote za mazishi ya
Sharomillionea aliyekufa kwa ajali ya gari maeneo ya nyumbani kwao.
MAUMIVU
Karibia wote waliozungumza na Bingwa juu ya msiba huo, wengi
walionyeshwa kuguswa na kuumizwa zaidi na marehemu kuibiwa vtu vyake dakika
chache baada ya kupata ajali na kupoteza maisha wakati huo huo.
Makala haya yameandikwa na Kambi Mbwana aliyekuwa Muheza
0712 053949
0753 806087
Mwisho
No comments:
Post a Comment