Marehemu Hussein Mkiety Sharomillionea kulia, enzi za uhai wake, akiwa na King Majuto
Na Kambi Mbwana, aliyekuwa Muheza
TATIZO sio kufa, ila mazigira yaliyosababisha kifo. Hii ni
kauli inayojirudia mara kwa mara katika kichwa changu, hasa nilipohakikisha kuwa,
kweli msanii wa vichekesho hapa nchini, Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea ametangulia mbele ya haki.
Sharomillionea alifariki Jumatatu ya Novemba 26 katika
kijiji cha Songa Kibaoni, wilayani Muheza, mkoani Tanga. Kifo hicho kilitokana
na ajali ya gari lenye namba za usajili T478 BVR, Toyota Harrier na kuzikwa
Jumatano katika makaburi ya kijiji kwao Lusanga.
Mazingira ya kifo cha Sharomillionea yanashangaza. Msanii
huyo hakukutwa na nguo katika mwili wake, ikiwa ni dakika chache baada ya kufa
katika ajali hiyo iliyotokea karibu kabisa na mahali apokulia, chimbuko la mama
yake, Lusanga.
Kijiji cha Kibaoni hadi Lusanga ni kilomita tano tu. Ni
karibu mno. Kwa wanaofahamu maisha ya vijijini kama
sisi, ina maana kuwa hawa wote waliishi kwa upendo kiasi cha kushirikiana baadhi
ya vitu, ikiwamo misiba.
Katika kuliangalia hilo,
nashawishika kusema kuwa msanii huyu aliuliwa na baadhi ya watu waliovamia gari
lake na kumuibia thamani zake mara baada ya
kupinduka na kusababisha kifo cha msanii huyo.
Inauma sana.
Wapo baadhi ya watu wanaowamalizia majeruhi sehemu nyingi zinapotokea ajali za
barabarani na kugharimu roho za watu wengi. Kama
huo ni uongo, basi upo karibu na ukweli na lazima jamii iliangalie upya suala
hili.
Kila mtu ahakikishe kuwa anakuwa mlinzi wa mwenzake wakati wowote.
Pale inapotokea ajali za barabarani, basi kazi ya kwanza iwe ni kuokoa roho za
wenzao hata kwa kuwahisha katika vituo vya afya kwa kupata huduma ya kwanza.
Tabia ya kuvamia ajali hizo na kuwapora watu ni unyama. Ni
unyama kwakuwa huenda majeruhi angewahishwa hospitali angeweza kupona.
Lakini kwakuwa tangu kupata ajali anasumbuliwa kutaka
kuvuliwa saa ya mkononi, simu ya mkononi alipoiweka au pochi yake mfukoni, ni
sababu kubwa ya kupoteza roho za watu.
Serikali ya kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa lazima
wakae na kuliangalia hili. Katika kijiji cha Kibaoni kilipotokea ajali ya
Sharomillionea na kugharimu roho yake, uchunguzi ufanywe kwa ajili ya kuwabaini
waliopora vitu vya marehemu.
Hawa wasakwe. Ni zaidi ya roho mbaya. Najua wapo watakaosema
kuwa Sharomillionea ni mmoja kati ya mamia ya watu wanaokufa kwa ajali ya gari
barabarani, lakini ifikie wakati kila mtu aone ana deni kwa mwenzake.
Huu ndio ukweli. Kwanini watu tunabadilika kiasi hiki? Watu
wananyanyasika katika vijiji vyao wenyewe? Kama Sharomillionea anaporwa hata
suruali yake, mtu kutoka Tarime, Mwanza atakuwa kwenye mazingira gani?
Hapo mwanzo wa makala haya nimesema kuwa, tatizo sio kufa,
maana kumeumbwa na kila mmoja ataonja umauti. Ila ubaya ni pale watu
wanapochangia vifo vya wenzao, ikiwamo kuwamalizia ili wawaibie mali zao.
Kuwamalizia majeruhi naamanisha kutowapeleka katika vituo
vya afya vilivyokuwapo eneo la tukio badala yake watu wanaingia na kuchukua
vitu vya marehemu. Mbali na kuiba vitu hivyo, wengineo hufika mbali kwa kuvunja
hata gari lenyewe na kubeba kwa ajili ya kuendelea na maisha yao, bila kujali thamani ya mtu.
Hatuwezi kwenda hivyo Watanzania. Mara tuonapo ajali za
barabarani, basi tushiriki kuwaokoa majeruhi kadri tuwezavyo. Kuwaibia na
kuacha kuwasaidia wanapoomba msaada ni kitendo cha kigaidi kwa ujumla wake.
Huu ndio ukweli. Japo wakati mwingine unauma, lakini
tuliangalie kwa kina kwa ajili ya kuleta haki sawa kwa watu wote. Leo kwake
kesho kwako. Leo kwao kesho itakuwa kwetu. Je, wewe uliacha kumsaidia mwenzako,
vipi unanishawishi vipi nikusaidie?
Nafikiria kila mtu ataelewa namaanisha nini. Serikali Kuu,
inayowakilishwa na watu mbalimbali, wakiwamo wenyeviti wa Serikali za Mitaa au
vijiji washirikiane na vyombo vya serikali kuwatafuta vibaka hao wazoefu
wanaofanya uhuni sehemu mbalimbali hapa nchini.
Ndio maana nasema, kwa mazingira haya, Sharo Millionea
walimuua wenyewe, tena katika kijiji alichokulia. Ni aibu.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment