Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
KAMA kuna jambo ambalo
viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanakosea, ni kuona kuwa wananchi wao ni
watu wa kudanganywa wakati wote kwa kubuniwa matamko ambayo mengi hayatimizwi
kwa wakati.
Ikifanya hivyo, CCM itakuwa imejipunguza makali yenyewe.
Ujio mpya wa Sekretariet iliyoundwa na Mwenyekiti wao, Jakaya Mrisho Kikwete
mjini Dodoma,
haitakuwa na mashiko. Zaidi ya hapo nyimbo mbalimbali zinazoimbwa na viongozi
hao zitachosha masikioni.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mwenyekiti wa CCM
Kwa sababu hiyo, ili CCM iendelee kupendwa na kuheshimiwa na
Watanzania wengi, ihakikishe kuwa wananchi wao wanaishi maisha bora. CCM
ihakikishe inawabana watendaji wao ili wafanyae kazi bila kuchoka kwa ajili ya
Watanzania.
Kwa mfano, Katibu Mkuu mpya wa CCM, Abdulrahman Kinana, neno
lake la kwanza tangu alipopewa nafasi hiyo, alisema kuwa viongozi wa jumuiya
zote za chama chao walioshinda kwa rushwa, atapambana nao.
Ni kauli inayoshangaza kidogo. Na siamini kama kweli
itafanikiwa, maana hata Rais wa Tanzania,
Kikwete, ambaye ndio mwenyekiti wa chama hicho kikongwe cha siasa, alitangaza
hadharani kuwa rushwa ndani ya CCM ni kikwazo.
Kwa bahati mbaya, matamko hayo ya rushwa hayajaanza kutoka
kwa kinywa cha Kinana tu. Hata Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Wilson Mukama na
watendaji wengine wa chama, akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
waliupamba wimbo wa kujivua gamba kwa staili ya aina yake na kutolewa siku 90.
Matokeo yake hayajafanikiwa. Kutokana na hilo, wapo waliojua kuwa CCM kila
kinachofanyika, kipo kwa ajili ya kulindana zaidi. Hayo ni mambo ya kawaida
kwenye CCM. Mara kadhaa viongozi hawawezi kukata tawi waliyokalia.
Pamoja na yote hayo, CCM lazima ijuwe kuwa wanachama wao
wengi na wapiga kura katika Taifa hili wapo vijijini. Vijiji ambavyo vina
changamoto kubwa za kimaisha. Vipo vijiji ambavyo kwa miaka 51 sasa ya Uhuru
hawajui maisha bora ni wimbo gani.
Zipo Kata, Tarafa na wilaya ambazo kwakweli ukifika huwezi
kuamini maisha yanayopatikana hapo, licha ya kuona ni wana CCM na wenye mapenzi
na chama chao.
Kwa sababu hiyo, Kinana na watendaji wake badala ya kupiga
wimbo wa rushwa ambao wengi wanaona hautafanikiwa, wajaribu kutoa mawazo yao, kuwashurutisha watu
wao kuhakikisha bei za bidhaa zinashuka.
Nasema hivyo kwasababu, kelele zote zinazotoka kwa CCM sasa,
inadaiwa kuwa ni kujiweka sawa na chaguzi zijazo. Chaguzi ambazo ni za Serikali
za Mitaa kwa nchi nzima, ambapo pia utafuatwa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Watanzania wanakabiriwa na matatizo mengi ya kimaisha. Mchele
uliokuwa ukiuzwa hadi mia nane mwaka 2005, leo bidhaa hiyo inauzwa kwa Sh 1800
hadi 2000. Unga leo unauzwa shilingi 1000 hadi 1200, huku sukari, maharage
navyo vikiuzwa kwa 2000.
Kuna bidhaa nyingine kama
vile mafuta ya kula, mafuta ya taa, dizeli, petroli na nyinginezo hazishikiki
kutokana na kuuzwa bei ghari mno. Vitu hivi vinauzwa bei ya juu kwasababu
wakati mwingine watendaji hawajui wanachokifanya.
Ama wanajua, ila wanafanya kwa makusudi kwa kuangalia
maslahi yao
binafsi. Watu wanaishi maisha magumu mno katika majumba yao. Wapo Watanzania mlo wa siku moja kuupata
ni baada ta kuumiza kichwa kupita kiasi.
Zipo baadhi ya kata ambazo hazina vituo vya afya vyenye
uwezo wa kuhudumia katika eneo lote la Kata hiyo. Haya ni mambo ya kushangaza.
Bado unahitaji chama kupendwa? Bado unatarajia kuingia kwenye mbio za Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015?
Katika kulisema hilo,
naamini Kinana na watendaji wake wa chama na serikali, watakaa chini na
kujiangalia upya. Huu wimbo wa rushwa, ni mtamu ingawa umechosha. Wimbo huu hata
kama ukifanikiwa, basi ni kwa maslahi yao
viongozi.
Ni siasa zile za makundi zinazosemwa na wachambuzi
mbalimbali wa kisiasa. Kwanini nasema hivyo, wimbo huu sijui kama utafanikiwa,
kama itajulikana pia katika baadhi ya wanaotajwa kutoa rushwa, ni miongoni mwa
makundi yao.
Nasema hivi kwasababu katika siasa, suala la makundi ni
jambo la kawaida. Hakuna anayeweza kupewa nafasi kubwa kama
hatakuwa karibu na watu wengi katika chama husika. Ndio maana unasikia harakati
zikipamba moto.
Watu wanashindana katika mitaa, wilaya na mikoa kufanya kila
wawezalo kuneemesha makundi yao
kwa ajili ya siasa zao.
Baada ya kutoa katika mikutano yao katika baadhi ya mikoa, Kinana na kundi
lake pia wabuni sasa ziara ya vijijini kuangalia maisha halisi wanayoishi
Watanzania, ambao hakika ndio wapiga kura.
CCM ifanya hivyo haraka kabla ya wananchi hawa hawajamini
kuwa chama hiki kikongwe sio cha walalahoi. CCM ifanye hivyo kwa ajili ya
kujirudisha karibu na wapiga kura wake. Bila hivyo, maendeleo ya chama hiki
yatasua sua.
Hakuna Chaguzi ngumu kwa CCM kama
utakaokuja mwaka 2015. Ni uchaguzi ambao vyama vya siasa vya upinzani vimefanya
juhudi kubwa kuwafikishia elimu ya uraia Watanzania wanaoshi vijijini,
wakiamini hizo ni ngome za CCM.
Vyama kama vile Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ADC, TLP, NCCR-Mageuzi na vinginevyo
vinajipanga kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanaingia kwenye utawala
wa upinzani.
Wapinzani wanajua kuwa wapiga kura wengi wa CCM wapo
vijijini. Ndio maana tunashuhudi wakiweka mikakati mingi kuwafikia huko na
kuwakomboa kifikra. Haya ni mambo ambayo CCM inatakiwa kuyafahamu.
Isikae kutunga semi zisizokuwa na mashiko. Wanachama wa CCM
na wale wasiokuwa na vyama wanachopenda wao ni
maisha bora na sio idadi ya matamko ya kichama yasiyokuwa na mashiko
kwao, maana bado wanakufa njaa.
Huu ndio ukweli. CCM itaheshimika zaidi kwa kufanikisha
maisha bora kwa kila Mtanzania. Ndio njia yao.
Ndio wimbo walioanzisha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na kumteua Jakaya Kikwete
kuwa mgombea wao na kuchaguliwa kwa mbwembwe mno.
Watanzania wengi walimuamini Kikwete nab ado wanamuanini.
Lakini, zile ahadi alizoahidi kwa Watanzania wake, baadhi hazijafanikiwa.
Kwanini sasa CCM kama chama tawala, isiweze
kujua kupanda kwa gharama za maisha kunatokana na watendaji wao.
Kwanini CCM isione kuwa kupanda kwa bei za mafuta wakati
mwingine kunasababishwa na Waziri wake, kwa kutokuwa mkali kwa wafanyabiashara
wa mafuta wenye nia ya kunemeeka wenyewe kwa kupandisha bei ovyo ovyo.
Kwanini CCM isishangazwe na bei ya sukari kupanda wakati
kuna viwanda vinavyofanya kazi usiku na mchana, hasa kwa mkoa wa Morogoro na
Kagera. Haya yanashangaza sana.
Kwa miaka 10 ya Kikwete, baadhi ya Watanzania wameona CCM
haiwezi tena kuwakomboa kimaisha, hasa kutokana na kupanda kwa gharama za
maisha.
Hivyo hizi kelele za rushwa zinazopigwa na viongozi wa
chama, zinapaswa kuangaliwa upya, ili ikiwezekana ziende sambamba na kuwaamuru
mawaziri wake, wabunge wake, wafanye kazi kama
timu moja kwa ajili ya maisha bora.
Baadhi ya maeneo wanakuwa na maisha magumu kwasababu hata
huduma ya umeme hawajaipata, licha ya baadhi ya vijiji kupitwa na njia ya umeme
unaopelekwa katika miji mingine, bila kujua athari wanayoipata wananchi wa
vijiji hivyo.
Hatuwezi kuwa na maisha bora wakati yale yanayoweza kukuza
uchumi wetu hayapatikani kwa wakati. Kwa mfano, mahali kwenye huduma ya umeme,
wakati mwingine maisha yao yanakuwa ya kawaida,
hasa kama wananchi watautumia vizuri.
Biashara nyingi hata za kuuza maji baridi zinahitaji kuwa na
umeme, hivyo hili haliwezi kuachwa na kuendelea kukemea ugumu wa maisha kwa
kubuni njia za kupambana katika siasa za ndani zitakazokuja kuiathiri CCM.
Naamini kuna mambo mengi yanayoweza kufanywa kwa ajili ya
maslahi ya Watanzania, ingawa sitaki kujua kuwa mambo hayo yatachangiwa na
matamko ya Kinana, Nnauye, wanayotoa katika mikoa, ila ni kuona sasa Watanzania
wanaishi maisha bora.
Vipo vitega uchumi vingi ambavyo kwa hakika vikitumiwa
vizuri makali ya maisha kwa Watanzania yatapungua. Ziara za viongozi wa CCM
zihamie katika vijiji ili waone jinsi gani wapiga kura wao wataendelea
kukithamini chama chao na kukipa nafasi kubwa zaidi.
Vinginevyo, wafuasi wa CCM na wachama wake wataona hapo
walipokuwa sasa wanatakiwa waondoke na kuhamia upinzani maana chama hicho
kimeshindwa kabisa kuwaongozwa Watanzania na kuwaletea maisha bora.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment