Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Na
Kambi Mbwana, Dar es Salaam
YAPO
mambo mengi yanayoifanya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ishindwe
kueleweka na kuheshimika kwa wananchi wake, likiwamo hili la watendaji wake
kufanya kazi chini ya kiwango.
Watendaji
hao ambao wameaminiwa na kupewa nafasi hizo, wanawaangusha mabosi wao. Katika
hili kila mmoja ni muathirika kwa wakati wake.
Hata
wale wanaoshika nafasi hizo kisiasa, hasa wabunge, mawaziri na manaibu waziri,
baadhi yao wamekosa
uaminifu kwa watu wao, licha ya kuamini kuwa watawaletea mafanikio.
Uamuzi
wao mara nyingi huwa wa mashaka. Wanawaacha ndugu zao wakishindwa kuelewa
kwanini wamezaliwa katika nchi hii, inayojipambanua kuwa ina utawala bora na
demokrasia ya kueleweka.
Watendaji
wengi wamekuwa wakifanya uamuzi ambao wakati mwingine huwa na walakini ndani
yake.
Wanabaki wakilalamikiwa au kuogopwa kama
miungu watu, hivyo kuwa mwiba mchungu kwa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, ambaye hatasahau uongozi wake kuwa na misuko suko ya kila aina.
Nimelazimika
kuanza hivi baada ya kugundua kwamba idadi kubwa ya wananchi wamekosa imani na
nchi yao na hamu ya kuendelea kuithamini
kutokana na viongozi hao kuweka mbele maslahi yao binafsi, huku wakishindwa kuzitatua kero
kubwa na ndogo.
Kwanini
nasema hivyo? Tanzania
kila siku ya Mungu inatawaliwa na migomo isiyokuwa na kikomo. Katika hilo, wengi wanapoteza
maisha na wengineo kuacha wajane na watoto wa mitaani.
Hili
halitaji elimu ya Chuo Kikuu kuona kwamba kadhia hiyo inaacha pigo kubwa katika
jamii zetu. Mara nyingi wanaosumbuliwa na matatizo hayo ni wale wasiokuwa na
kipato kikubwa.
Wale
ambao hata mlo wa siku moja kwao ni tatizo kubwa, hivyo viongozi wanaowangiza katika
mikataba tata, isiyokuwa na faida na nchi, hakika wanawaumiza walalahoi, maana
fedha nyingi zinatumiwa bila sababu za msingi, wakati faida inayopatikana,
inaingia kwenye mifuko ya baadhi ya wakubwa serikalini.
Masikini
wanabaki wanalia. Wanaishia kulalamika. Hawajui la kufanya, hasa wanapokumbuka
kuwa kilio cha samaki, machozi yanakwenda na maji.
Kwa
mfano, hakuna asiyetaka jambo la maendeleo katika sehemu yoyote ile Tanzania.
Lakini, tunapozungumzia hayo maendeleo, tuhakikishe kuwa yanapatikana kwa haki,
ushirikiano na maelewano kwa wote, ukizingatia kwamba nchi hii ni yetu wote.
Wale
wanaoletewa maendeleo hayo, lazima walindwe, wasibuguzwe katika nchi yao.
Na inapofikia
wanatakiwa wahamishwe kwa makubaliano ya kuwalipa, basi wapewe haki zao
kulingana na thamani ya majengo yao pamoja na
mimea yao.
Kwa
bahati mbaya, baadhi yao wapo tayari kutoa roho
za wenzao, maana wameamua kufanya harakati za kuleta maendeleo kwa vurugu,
manyanyaso, wakiwa na virungu pamoja na silaha nyingine lukuki, kama njia ya kujihami itakapotokea purukushani.
Kupo
kunapotokea vurugu na pia kule kunapokuwa na utulivu katika operesheni ya aina
mbalimbali, ikiwamo ile ya kuhamishwa katika eneo moja kwenda lingine kwa faida
inayokusudiwa na serikali.
Kwa
miaka kadhaa sasa kumekuwa na kutoelewana kati ya serikali na wananchi wa
Kwembe, Manespaa ya Kinondoni, jijini Dar
es Salaam.
Katika
eneo hilo,
zimeandaliwa zaidi ya heka 3800 ambazo kwa mujibu wa wenyeji, kunatakiwa
kujengwe Chuo cha Muhimbili na shughuli nyingine za kijamii.
Sawa,
ni jambo zuri. Hakuna asiyetaka maendeleo, maana kama
chuo kitakamilika, watasoma Watanzania wenzetu hivyo tunalipokea kwa furaha
kubwa.
Ila,
baada ya mvutano wa muda mrefu, hatimae nyumba zaidi ya 86 zimevunjwa wiki hii,
wakati malipo yao
yakiwa madogo na hayalingani na maisha ya leo.
Mtu
mwenye nyumba moja ya kawaida yenye mimea kama
vile miembe, michungwa na mingineyo kupewa Sh 400,000 huko ni kumuonea.
Wapo
waliopewa Sh Milioni 4 licha ya kuwa na nyumba nzuri za thamani sambamba na
mimea.
Uonevu
mkubwa unafanywa na serikali na dhambi hii hakika inaweza kuwaathiri siku za
usoni.
Watu
wanalalamika kwa kukandamizwa na serikali yao,
tena ile wanayoiweka madarakani. Wanapoteza imani nayo, maana maendeleo
yanayotakiwa yanasakwa kwa kupitia migongo yao.
Hawaonewi
huruma kamwe. Wananchi wa aina hiyo waende wapi? Shida zao nani wa kuzitatua?
Hili lazima watu walibaini, maana tunapoelekea ni kubaya na ipo siku watafanya
uamuzi mgumu.
Serikali
ya CCM isikimbilie tu kujivua gamba kwa baadhi ya wanasiasa wao, bali pia wale
wanaoshika vitengo nyeti, wawe na mioyo ya kibinadamu.
Wakuu
wa wilaya ambao ndio wawakilishi wa Rais wafanye kazi yao
kama inavyotakiwa.
Wasipokuwa
makini, chuki kwa serikali yao
itakuwa ya aina yake na itafikia wakati hawatakubali ushauri wa aina yoyote
kutoka kwa mtu yoyote.
Nilikuwapo
katika oparesheni ya kubomoa nyumba katika Kata ya Kwembe. Nilichokiona, haki
haijatendeka kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao.
Ndio
wamelipwa kiasi kidogo cha pesa, lakini fedha hizo haziwezi kuwasaidia wajenge
sehemu nyingine tofauti na pale walipovunjiwa, ukizingatia kwamba hawajapewe
eneo lingine kwa ajili ya kuanza maisha mapya.
Maisha
ni magumu. Watanzania wanaishi kwa kubahatisha, huku wachache wanaofanikiwa
kujenga, hulazimika kulala njaa ili wasimamishe vibanda vyao.
Maendeleo
yanapobuniwa, huona wao ndio wahusika, hivyo kuhesabiwa vijisenti vya kula
kahawa na kupewa bila kuonewa huruma.
Hii
ni dhuluma ya wazi wazi kwa serikali. Dhambi hii lazima ikemewe, maana kuna
wakati wananchi watachoka kama wanavyochoka
kila siku na kuanza kupaza sauti zao juu kwa kisingizio cha ‘Nguvu ya Umma’.
Wanaona
huko ndipo ambapo watu wameamua kujitoa kwa walalahoi, wale wanaodhulumiwa haki
zao kila wakati, hivyo kuwapa uchungu.
Tembelea
kila kona ya nchi hii utagundua malalamiko kwa serikali ni mengi mno. Ndio, wapo
watakaosema serikali haiwezi kukwepa lawama.
Sawa,
ila hali ikiendelea hivi, hakika itakuwa balaa. Hawa wakimka watachukua uamuzi
ambao nchi nzima tutashindwa kuwaelewa.
Je,
ni kweli kuwa wanaolalamika wengi wao ni wanasiasa na hawana hoja? Hata wale wanaonyonywa
katika migodi pia hawana hoja?
Nao
ni wanasiasa? Wale wanaomenyeka katika machimbo ya dhahabu na bado wanatakiwa
wasichukuwe fedha zao kwenye mifuko ya pensheni hado baada ya miaka 55?
Hii
ni hatari. Hakuna juhudi za kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania zaidi ya
kubuni mbinu za kuwakandamiza wale wenye kipato cha chini. Wanakandamizwa na
kuwatoa manyozi ya damu.
Wanajitahidi,
ila mwisho wake huchoka na kukubali wapoteze maisha, maana wameshindwa kuipata
hata ile haki yao
ya msingi.
Hii
sio haki. Maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuwakandamiza zaidi walalahoi,
wakati nchi ina rasilimali nyingi zinazoweza kuingiza fedha, endapo viongozi
watajipanga na kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote na sio wachache wao.
Serikali
imepoteza mvuto kwa wananchi wake. Haiaminiki tena kwa watu wake, ndio maana
wengi wao wameanza kuamka na kukimbilia katika vyama vya upinzani.
Kwa
bahati mbaya, uamuzi wao huo unaonekana kama vile wanajisumbua, maana baadhi yao hudhani hakuna chama
kizuri zaidi ya CCM.
Chama
chenye historia kubwa na Taifa hili, ingawa kwa siku za karibuni, watu wake
wameanza kuingia mahali sipo.
Wanakiacha
chama kikishambuliwa na wabaya wake, maana wao wenyewe wameacha kufanya kazi
kwa ajili ya chama na nchi kwa ujumla wanahubiri siasa za chuki na wale wengine
wanaona uongozi bora ni kuwanyonya walalahoi, jambo ambalo si kweli.
Lengo
lao ni kuangusha chama na serikali yake, ndio maana wanaposhauriwa, hukataa na
kusema eti wanaolalamika ni wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wasiokuwa na
hoja, huku wakifananisha na robo ya sukari ndani ya bahari.
Kauli
kama hizi kwenye siasa ni mbaya. Haziwezi kukiokoa chama zaidi ya kukiangusha,
hasa katika kipindi hiki kigumu kwa siasa za Tanzania, maana katika siasa somo
la kutoa wanachama ni baya kuliko lile la kuongeza wanachama na wafuasi wapya.
Na
katika hilo, ni
rahisi kupunguza wanachana na wafuasi wa zamani kuliko kuongeza wapya, hasa kwa
CCM, kinachokaliwa kooni na vyama vya upinzani.
Kipindi
ambacho wapinzani hasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) muda wote
wanashambulia kwa kufanya mikutano katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Huko
kote wanahubiri mabaya ya serikali ya CCM, wakisaidwa na wenzao CUF, chama
ambacho kinaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, maarufu kama (SUK)
chini ya Rais wake, Dk. Mohamed Ali Shein.
Kila
mmoja awe na nia ya dhati ya kutatua kero za Watanzania, huku wakiweka mbele
ubinadamu na kuacha kuwakandamiza wananchi.
Serikali
ipo kwa ajili ya kuwaongoza Watanzania wote, hivyo katika hili lazima ikae na
kujisahihisha, maana hali inavyokwenda, kuna siku lawama hizi zitawaumbua
viongozi wake, hasa wanaotoka katika chama tawala, chenye hamu ya kutawala
milele, katika upepo huu wa mabadiliko ya kisiasa.
Mungu
ibariki Tanzania.
0712
053949
0753
806087
Makala hii iliwahi kutumika katika gazeti la Mtanzania.
No comments:
Post a Comment