https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, January 12, 2014

Yanga waanza nyodo Uturuki

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KOCHA msaidizi wa timu ya Yanga, Charles Boniface Mkwassa, amesema kwamba kwa kutua nchini Uturuki, anaamini watakaporejea nchini Tanzania hakutakuwa na timu itakayoweza kuwatishia kwa lolote kutokana na mazoezi yao makali.

Yanga wakiwa nchini Uturuki wakijiandaa kwa mzunguuko wa pili wa ligi ya Tanzania Bara, itakayoanza Januari 25.

Yanga iliyowasili katika hoteli ya Sueno Beach Side eneo la Manavgat pembeni kidogo ya jiji la Antalya, inajifua kwa nguvu zote kuhakikisha kuwa safari yao inakuwa na mashiko ya kujiandaa na mikiki mikiki ya Ligi ya Tanzania Bara, hatua ya mzunguuko wa pili na michuano ya Kimataifa.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa katika gazeti hili jana, Mkwassa alisema kwamba hana wasiwasi na Ligi ya Vodacom, akimini kuwa vijana wake wamepata eneo murua la kujinoa dhidi ya wapinzani wao kuanzia Januari 25.


Alisema kuwa anashukuru kikosi chake kimefika salama na wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri kiafya na kifikra hivyo mazoezi yaliyoanza jana yatasaidia kuiweka timu katika hali nzuri na kuwa tayari kwa mashindano.

"Kazi yangu kubwa ni kukiandaa kikosi kiwe katika hali nzuri ili pindi tutakaporejea nchini timu iwe fiti na tayari kwa ajili ya mashindano, kwa hali ilivyo nzuri na mazingira naamini timu itabadilika na kurejea nchini ikiwa katika kiwango cha kizuri cha ushindani," alisema Mkwasa.


Aidha, Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, yeye alisema kuwa Uturuki ina hali nzuri huku wachezaji wao wakifurahia mazingira ya mji huo, huku wakifikia katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano.


“Timu ilipokelewa na wenyeji majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za huku ikiwa ni sawa na saaa 12 kwa saa za Afrika Mashariki na moja kwa moja kikosi kilielekea katika mji wa Manavgat ambapo ndipo ilipo hoteli ya Sueno Beach Side ambapo msafara mzima umefikia,” alisema Kizuguto.


Aidha timu ya Sivasspor iliyopo Ligi Kuu nchini Uturuki inayonolewa na mchezaji wa zamani Real Madrid na timu ya Taifa ya Brazil Roberto Carlos pia imeweka kambi katika hoteli ya Sueno na leo asubuhi kabla ya Young Africans kuanza mazoezi waliweza kupiga picha ya pamoja na gwiji huyo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...