Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake, bendi ya Mashujaa
leo inafanya onyesho la aina yake katika Ukumbi wa Makuti, uliopo wilayani
Handeni, mkoani Tanga.
Rais wa bendi ya Mashujaa, Chalz Baba, pichani.
Shoo hiyo imekuja katika ziara ya bendi hiyo mkoani Tanga,
ambapo Ijumaa walifanya shoo katika Ukumbi wa Mamba Club, uliopo wilayani
Korogwe, wakati Jumamosi ya jana walitarajia kufanya shoo Nyumbani Hoteli,
Tanga Mjini.
Akizungumza jana kwa njia ya simu leo, Meneja wa bendi hiyo,
Martin Sospeter, alisema ziara yao imekuwa na mafanikio makubwa, huku wakiamini
kuwa wadau na mashabiki wa Handeni watapata burudani ya aina yake wilayani
humo.
“Tunashukuru kwa kupata nafasi ya kufanya shoo wilayani
Handeni, hivyo tunaahidi mashabiki wa muziki wa dansi watapata vitu adimu
watakapokuja kuangalia kazi nzuri kutoka kwa Mashujaa.
“Mashujaa ni miongoni mwa bendi zenye mguso na nia ya dhati
ya kuwa kileleni, hivyo naamini huu ni wakati wetu kudhihirisha makali yetu katika
tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa Sospeter, bendi hiyo imelazimika kukosa nafasi
ya kufanya shoo katika jiji la Dar es Salaam, baada ya nafasi tatu za wiki
kuanzia Ijumaa hadi Jumapili kuwa katika mkoa wa Tanga, ikisafiri na wanamuziki
wake wote, akiwamo Rais wao Charles Gabriel Baba, maarufu kama ‘Chalz Baba’.
No comments:
Post a Comment