Mbunge
wa Jimbo la Vunjo, Dkt. Augustino Mrema akikabidhi jezi kwa viongozi wa
vilabu 15 vitakavyoshiriki mashindano ya Mrema Cup 2014, katika hafla
ya uzinduzi uliofanyika juzi katika uwanja wa Himo.
Na Mwandishi Wetu, Moshi
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo (TLP), Dk. Augustino Mrema, amezindua mashindano ya soka, Mrema Cup 2014, yatakayoshirikisha jumla ya vilabu 15 kutoka katika kata zote 15 ya jimbo hilo.
Akizungumza mjini hapa mara baada ya uzinduzi huo, Mrema alisema lengo la mashindano hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika jimboni hapo ni kutoa fursa za ajira kwa vijana pamoja na kuleta mshikamano katika jamii.
Dk. Mrema alisema kwa sasa hakuna sekta inayofanya vizuri katika kutoa ajira kwa vijana kama michezo huku akisistiza umuhimu wa kushiriki michezo kwa lengo la kuhamasisha Amani, mshikamano na umoja katika jamii.
“Tunazindua mashindano haya kwa lengo moja tu, kuhamasisha mshikamano, amani na udugu wetu, dunia nzima hakuna sekta inayochangia kutoa fursa za ajira kama michezo hasa mchezo wa soka, vijana wakishiriki michezo wanapata kazi lakini pia inasaidia kuimarisha Afya,” alisema Dk. Mrema
Naye, Mratibu wa Mashindano hayo, inspecta msaidizi wa polisi kituo cha himo, Laban Sospeter alisema, Vilabu vitakavyoshiriki katika mashindano hayo ni Himo, Njia panda, Kahe, Makomu, Mamba, Kilema, Mandaka, Riata, Makuyuni, Mitsubishi na Kifaru ambayo ni timu mwalikwa.
Laban alisema baada ya uzinduzi huo, wanatarajia kuanza mashindano hayo wiki ijayo ambapo katika mechi ya uzinduzi kati ya Njia panda FC na Himo SC ulishuhudia Njia panda wakiibuka na ushindi wa 1-0.
Zawadi zitakazotolewa kwa washindi ni shilingi laki tano kwa mshindi wa kwanza, mshindi wa pili ni shilingi laki tatu na mshindi wa tatu akiondoka na laki mbili fedha taslim ambapo jumla ya shilingi milioni moja zita zitashindaniwa. | | | | | | | | | |
No comments:
Post a Comment