https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 23, 2014

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aunguruma mkoani Tanga, amvaa tena Zitto Kabwe


Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, amewataka Watanzania, hususan wanachama wa chama hicho kutopoteza muda kujadili suala la baadhi ya wanachama wa chama hicho waliopatikana na makosa ya usaliti na utovu wa maadili ndani ya chama hicho.

Ingawa hakuwataja wanachama hao aliowaita wasaliti, ni wazi alikuwa akiwalenga, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Tayari chama hicho kilikuwa kimeshawapokonya uanachama, Dk. Kitila na Mwigamba, huku Zitto akiendelea kubakia ndani ya chama hicho baada ya Mahakama Kuu kuizuia Chadema kumjadili.

Akifafanua, Lissu alisema, wanachama wa Chadema wanapaswa wajikite zaidi kukiimarisha chama hicho kila mahali na kujadili masuala yanayowahusu.

Lissu, ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Taifa, (BAVICHA), John Heche, alisema taifa linakabiliwa na masuala mengi ambayo yanahitaji umakini wa kila mwanachama wa chama hicho, akitolea mfano wa kujadili maudhui ya Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, ili taifa lipate Katiba mpya na bora.

Aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kwamba kutokana na uongozi mbovu, rasilimali za Tanzania zimeendelea kutafunwa na watu wachache kwa kupitia sera za ubinafsishaji ambazo zimetumiwa na watawala kama mianya ya kujigawia mali kwa mgongo wa uwekezaji, huku wazawa wengi wakiwa hawana la kufanya.

Alitumia mikutano hiyo kusoma taarifa za kila mwaka za bajeti za serikali ambazo zinaonesha mgawo wa fedha wa kila eneo kwa sekta, hususan zinazohusu huduma za jamii, akisema wananchi wengi hawajui kwa sababu viongozi wao hawataki wajue.

Kwa upande wake, John Heche aliwaambia wananchi kwamba bila kuupiga vita na kuutokomeza ufisadi ambao unaendelea kulitafuna Taifa, akidai unalelewa na Serikali ya CCM, wananchi hawatapata matumaini na maendeleo wanayoyahitaji. 
 
Alisema kuwa hata ujangili unaoendelea kwa kasi kubwa kiasi cha kutia shakani uwepo wa tembo katika mbunga za wanyama, ni matokeo ya ufisadi ambao Chadema kimekuwa kikihamasisha umma kuupiga vita kwa nguvu zote, kwa sababu utaliangamiza Taifa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...