Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
RAIS wa
Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi, amevipiga vijembe vilabu vya
soka vya Simba na Yanga, kwa madai kuwa vinajiendesha kizamani kwa kutegemea
ada ya uanachama, hivyo kukalia utajiri wao.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, pichani.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Malinzi alisema kuwa mfumo unaoendesha timu za Simba
na Yanga ni mbaya na maendeleo kwao yatachelewa kupatikana na kubakia na majina
yao.
Alisema huu
si wakati wa kusubiria ada ndogo ya uanachama wakati mipango kabambe ikiwekwa
inaweza kuzinufaisha timu hizo na kuondoka kwenye kutegemea mifuko ya watu
wachache.
“Katika
uongozi wetu huu lazima wanachama wetu wabadilike na kufanya vitu vyenye maana
ili kuendeleza soka la Tanzania na kupiga hatua na kutoka hapa tulipokuwa sasa.
“Viongozi
wanapaswa kutumia vizuri nafasi zao kwa kushirikiana na wanachama wao na
wataalamu wao, ukizingatia kuwa zipo mbinu nzuri zenye tija, ukiwapo mpango wa
hisa unaoweza kutajirisha timu zetu,” alisema.
Malinzi
amerithi mikoba ya Rais wa TFF aliyemaliza muda wake, Leodgar Tenga, huku
akiingia kwa mkwara mzito na mipango lukuki ya kuiletea maendeleo Tanzania
katika sekta ya mpira wa miguu.
No comments:
Post a Comment