https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, January 13, 2014

Chadema yamsafisha mwenyekiti wao Freeman Mbowe dhidi ya makombora ya Zitto Kabwe



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mhe, Freeman Aikaeli Mbowe

Kama mojawapo ya mikakati ya baadhi ya watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama, hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza; Tuhuma hizo ni pamoja na; 1.Kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha sh.Milioni 40 ili Mwenyekiti Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.

 2. Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa, sh. Milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na akalipwa. 3. Mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mbunge Mkono eti alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa sh. Milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.

 4. Mwaka huo huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa, alipokea sh. Milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni. Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kusema yafuatayo; 1. Hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. 


Ni uongo na uzushi uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM na kwamba chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania katika kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi, kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho kimepoteza ushawishi kwa wananchi.

 2. Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala. 3. Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko nchini kwamba,Mwenyekiti wa Chama Taifa, ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

 4. Kwa uhakika tunapenda kuiambia jamii ya Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko wote nchini, kwamba; Chama wala Mwenyekiti wa Chama Taifa, mahali popote na wakati wowote, hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.

 5. Tungependa kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA, badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya msingi yanayowaandamana kuhusu mikakati yao ya kuhujumu CHADEMA na viongozi wake, ambayo iwapo chama kisingeibaini na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani. 

6. Taarifa kuhusu baadhi ya tuhuma katika mkakati huo ambazo zimemlenga Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa kuhusisha shughuli zake binafsi za uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi husika. Imetolewa leo Dar es Salaam na;
Tumaini Makene Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...