Roberto Carlos mwenye nguo nyekundu akipiga picha na Yanga nchini Uturuki.
Mara baada ya kuwasili salama jana jioni katika hoteli ya
Sueno Beach Side eneo la Manavgat pembeni kidogo ya jiji la Antalya kikosi cha
Young Africans leo asubuhi kimeanza mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu pamoja na mashindano ya kimataifa barani Afrika.
Wachezaji wakifurahia picha ya pamoja na Roberto Carlos.
Timu ilipokelewa na wenyeji majira ya saa 11:00 jioni kwa
saa za huku ikiwa ni sawa na saaa 12 kwa saa za Afrika Mashariki na moja kwa
moja kikosi kilielekea katika mji wa Manavgat ambapo ndipo ilipo hoteli ya
Sueno Beach Side ambapo msafara mzima umefikia.
Sueno Hotel Beach Side ni hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota
tano, ambayo ina jumla ya vyumba 760, mabwawa ya kuogelea,viwanja viwili vya
mpira vya mazoezi kimoja kikiwa na nyasi za kawaida na kingine nyasi za bandia.
Kocha wa msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwassa kulia na Nizar Khalfan kushoto wakipiga picha na Roberto Carlos.
Kocha msaidizi wa Young Africans Charles Boniface Mkwasa
amesema anashukuru kikosi chake kimefika salama na wachezaji wote wakiwa katika
hali nzuri kiafya na kifikra hivyo anatarajiwa mazoezi yatakayoanza leo
yatasaidia kuiweka timu katika hali nzuri na kuwa tayari kwa mashindano.
"Kazi yangu kubwa ni kukiandaa kikosi kiwe katika hali
nzuri ili pindi tutakaporejea nchini timu iwe fiti na tayari kwa ajili ya
mashindano, kwa hali ilivyo nzuri na mazingira naamini timu itabadilika na
kurejea nchini ikiwa katika kiwango cha kizuri cha ushindani" alisema
Mkwasa
Young Africans inatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza wa
kirafiki dhidi ya timu ya Ankara Sekerspor iliyopo Ligi Daraja la Kwanza nchini
Uturuki.
Aidha timu ya Sivasspor iliyopo Ligi Kuu nchini Uturuki
inayonolewa na mchezaji wa zamani Real Madrid na timu ya Taifa ya Brazil
Roberto Carlos pia imeweka kambi katika hoteli ya Sueno na leo asubuhi kabla ya
Young Africans kuanza mazoezi waliweza kupiga picha ya pamoja na gwiji huyo.
No comments:
Post a Comment