Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU wa
muziki wa dansi wanaotokea katika mkusanyiko unaojulikana kama Cheza Kidansi,
juzi walifanya kikao cha kwanza na kuadhimia mpango wao kuwawezesha wanamuziki
wa muziki huo na kuwakwamua kiuchumi.
Wadau wakijadiliana jambo katika kikao hicho cha Cheza Kidansi.
Kikao hicho
kilifanyika katika Ukumbi wa Garden Breeze, ambapo kilihudhuriwa pia na mlezi
wao Yusuph Mhandeni, maarufu kama Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa Kata
ya Makumbusho katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza
katika kikao hicho, Yusuphed alisema kuwa mengi yaliyojadiliwa katika kikao
hicho ni kuona muziki wa dansi unarudi katika chati yake ili wanamuziki
wajimudu kiuchumi.
Alisema
wanamuziki wengi wa dansi hawana maisha mazuri kuliko wenzao wa Bongo Fleva,
hivyo hilo ni kati ya changamoto zinazoendelea kuwakumba.
“Aidha
tulijadili pia namna gani wanamuziki hawa wanatumika kwenye matukio makubwa
ndani ya chama na serikali, ukizingatia kuwa suala hilo litakuwa na tija kwao.
“Kwa sasa
wasanii wa kizazi kipya ndio wenye soko kubwa na kufanikisha maisha bora kwao,
ndio maana hata vituo vya redio bado vimeegemea zaidi huko, jambo ambalo
nimefurahi kuona Cheza Kidansi wamejaribu kuliangalia hili kwa kina,” alisema
Mhandeni.
Cheza
Kidansi ni kundi linalotokea katika mtandao wa kijamii linaloendeshwa kwa
kuutangaza muziki wa dansi na kuangalia changamoto zao ili kuuweka kileleni
kama ilivyokuwa awali.
No comments:
Post a Comment