Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI mihemko gani isiyokuwa na likizo? Nani yupo nyuma ya
wanachama hawa wa Simba? Nini hasa kiini cha mzozo huu? Haya ni baadhi ya
maswali ninayojiuliza mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Ni pale ninapoangalia mgogoro unaoendelea kuwapo miaka nenda
rudi kwa klabu ya Simba. Ndio, kuna uwezekano mkubwa mwenyekiti wa klabu ya
Simba, Ismail Aden Rage hayupo sahihi.
Na inawezekana pia anavunja Katiba hasa kwa kuangalia kuwa
Makamu Mwenyekiti wake Godfrey Kaburu alijiuzulu na nafasi yake haijajazwa hadi
wakati huu.
Katiba ya Simba inasema Makamu Mwenyekiti anapojiuzulu nafasi
yake inatakiwa izibwe ndani ya siku 90. Tangu Kaburu ang’oke, ni zaidi ya siku
200 zimepita.
Haya ni mapungufu makubwa sanjari na ubabe aliokuwa nao Rage
katika madaraka yake ndani ya Simba. Pamoja na hayo, Simba inatakiwa kufanya
uchaguzi Mkuu Mei mwaka huu.
Hivyo inaonyesha kuwa Rage ana nafasi ndogo ya kuwapo katika
nafasi hiyo, hasa kama kweli wanachama hao wamemchoka mwenyekiti wao huyo.
Kama hivyo ndivyo, sioni kwanini wanachama hao wasijipange
ili wasubiri Uchaguzi Mkuu wao. Hii siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia
kwasababu chokochoko hizi hazina tija.
Hata kama Rage akiamua kutangaza kujiuzul leo, nani anaweza
kushika nafasi yake kwa nyakati hizi za kuelekea uchaguzi? Binafsi naona huu ni
mgogoro wa maslahi.
Kuna mtu au watu wapo nyuma ya wanachama hawa ambao kila
mwaka wamekuwa wakijiweka mbele. Baadhi yao ndio walioshiriki kumsumbua Hassan
Dalali wakati yupo madarakani.
Muda wake ukaisha na wanachama hawa hawa wakamchagua Rage awe
mwenyekiti wao. Ndani ya mwaka mmoja, wakageuka na kumuona Rage si chochote.
Mgogoro huu ulikuwapo tangu mwaka 2011. Kila siku ni maneno
na mvutano usiokuwa na maana yoyote. Ndio, naweza kuwa miongoni mwa wadau wa
soka wanaotaka Rage ang’oke au akubali kuongoza kwa kufuata katiba yake, ila
kwakuwa wakati wake umeshakwisha, sidhani kama kuna haja ya kupambana naye.
Waswahili wamesema kuku wako, manati ya nini? Hata afanye
vipi, bado atatakiwa aitishe Mkutano Mkuu wa Simba utakaombatana na Uchaguzi
Mkuu ndani ya mwaka huu.
Nafikiri Watanzania wote hususan mashabiki na wanachama wa
Simba wangetulia ili mipango ya kiutendaji ifanywe kama ipo na baadaye
watakutana katika uchaguzi wao.
Hapo watafanya uamuzi wowote watakaopenda. Kinyume cha hapo
tutaendelea kubabaisha kwa kuingiza chokochoko zisizokuwa na maana na kuharibu
soka letu.
Hakika siwezi kuvumilia, hivyo kuna haja sasa ya wanachama wote
wa Simba kumuacha Rage na badala yake wajiandaye katika Uchaguzi wao
utakaotishwa kwa mujibu wa Katiba yao.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment