Na Henry Paul, Dar es Salaam
Mwambao Soccer Bonanza ambalo hufanyika kila baada ya miezi
miwili litafanyika Jumapili katika Uwanja wa Mikocheni A. Shuleni kuanzia saa
mbili asubuhi na linategemewa kumalizika saa kumi na mbili jioni.
Akizungumza Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Lusozi Faza, alisema
kuwa Bonanza hilo kama ilivyo kawaida litashirikisha timu saba ambazo ni Boko
National Veteran, Wazee wa Kazi Veteran, Bagamoyo Veteran, Kunduchi Beach
Veteran, Mwenge Benz Veteran, Mbezi Beach Veteran na wenyeji Mikocheni Veteran.
Mwenyekiti Faza alizungumzia Bonanza hilo na kusema kuwa ni
mwisho katika mzunguko wa pili baada ya kuanzishwa katika
mzunguko wa kwanza Mei 13, 2012.
Bonanza hilo ambalo linahusisha timu hizo za Ukanda wa
Mwambao limekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa maeneo hayo huku likitoa
burudani tosha na kuwakumbusha wapenzi wa soka baadhi ya wachezaji mahiri
waliotamba enzi hizo ambao hivi sasa wamesahulika.
Wachezaji hao ni kama vile Said Mrisho ‘Zicco wa Kilosa’,
Issack Mwakatika waliochezea klabu ya Yanga na Athanas Michael aliyetamba akiwa
na timu za Malindi, Pilsner, RTC Kagera, Tanzania Stars, Lusozi Father
aliyechezea Pan African, Toto African ya Mwanza, Athumani Jumapili ‘Chama’
aliyechezea klabu ya Simba na wengine wengi.
Akimalizia Mwenyekiti Lusozi aliwataka wapenzi wote wa soka
wa kuanzia Mikocheni, Mwenge, Mbezi Beach, Tegeta, Boko, Bunju na Bagamoyo
kuhudhuria kwa wingi na kuja kuona Bonanza hilo ambalo linakutanisha wachezaji
mahiri wa zamani waliotamba wakiwa na timu za ligi daraja la kwanza Tanzania
Bara (sasa ligi kuu).
No comments:
Post a Comment