WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda kesho atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka 2013-14, itakayowakutanisha wanawake wanne itakayofanyika kesho katika Ukumbi wa The African Dream mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, ambayo ndiyo iliyoratibu zoezi hilo, Eric Shigongo, alisema jana kwamba shughuli hiyo itakuwa ni hitimisho la kazi kubwa ya kupokea na kuchuja kura zilizotumwa na wasomaji kumtafuta mwanamke bora ambaye ni nembo kwa taifa.
“Zoezi hili lilifanyika kwa muda wa miezi tisa, kuanzia Juni mwaka jana hadi Machi mwaka huu. Awali kabisa watu walitakiwa kutuma majina ya wanawake wanaowaona ni bora ili wapigiwe kura, watu waliitikia vizuri sana, kwani jumla ya majina 150 yalitumwa katika kipindi cha miezi miwili.
“Baada ya hapo majina hayo yakaandikwa katika magazeti na watu wakatakiwa kupiga kura ili kuwatoa wanawake ambao wanadhani hawakustahili tuzo hizo,” alisema Shigongo, ambaye kampuni yake inatoa magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Amani, Risasi na Championi.
Alisema katika awamu ya kwanza ya miezi hiyo miwili, majina ya wanawake 20 yaling’ara na hivyo kuingia katika awamu nyingine ya kupigiwa kura, ambapo baada ya muda kama huo pia, wanawake kumi walipata alama nyingi na hivyo kuingia katika awamu ya tatu na ya mwisho.
Alisema kwenye hatua hiyo ya mwisho, wanawake watano walipita ambao ni Ananilea Nkya, Anna Tibaijuka, Anna Kilango Malecela, Asha Rose Migiro na mama Maria Kham. Katika zoezi hilo, wanawake hao wenye mvuto katika jamii walichuana na mmoja wao, Nkya, kuondolewa baada ya kura zake kutotosha kwa ajili ya fainali,” alisema Shigongo.
Kwa upande wake, mratibu wa Tuzo hizo, Luqman Maloto, alisema tukio hilo la kihistoria ambalo pia litashuhudiwa na wabunge wa Bunge la Katiba walio mjini Dodoma, litaambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwemo Linah,” alisema Maloto.
No comments:
Post a Comment