Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake, Twiga
Stars, Rogasian Kaijage, amesema kwamba wapinzani wao Zambia, walijiandaa zaidi
kuliko wao, hivyo wametolewa kwa haki.
Katika mechi ya juzi iliyopigwa katika Uwanja wa
Azam Complex, Twiga Stars, ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia ‘Shipolopolo,’
hivyo kutolewa kwa bao 3-2 kufuatia matokeo ya mechi ya kwanza iliyochezwa
nchini Zambia baada ya kupigwa bao 2-1.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaijage
alisema kuwa maandalizi yao hayakuwa mazuri tofauti na wenzao, hivyo ujuzi wao ulishindwa
kufanya vyema dhidi ya wapinzani wao.
Alisema ingawa walipania kuwatoa wapinzani wao,
lakini kiwango chao na maandalizi yao hayakuwa mazuri kiasi cha kuwaaminisha
kusonga mbele.
“Tumekuwa na matamanio ya kusonga mbele katika
michuano ya Kimataifa, ila lazima tufahamu namna ya kuandaa wachezaji wetu.
“Tumevuna kile tulichokipanda dhidi ya timu ya
Zambia, ambapo wametufunga bao 3-2, hivyo sisi kutoka katika michuano ya
kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Wanawake Afrika (AWC),” alisema.
Licha ya kuwa na wachezaji kadhaa wenye kutajwa kama
hodari wa kucheza soka, timu ya Twiga Stars, imeondoshwa katika michuano hiyo,
hivyo kushindwa kuwapa raha Watanzania.
No comments:
Post a Comment