Kamanda
wa polisi mkoani Iringa Kamishina Msaidizi Ramadhan Mungi akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari asubuhi hii mjini Iringa wakati
alipozungumza nao katika ofisi zake zilizopo jengo la mkuu wa mkoa huo.
……………………………………………………………………………
Ndugu waandishi wa habari, kwa niaba ya askari Polisi wa Mkoa wa Iringa, nitumie fursa hii kuwakaribisha hapa ofisini kwetu.
Ndugu zangu tumeitana hapa asubuhi hii ili niweze kuwapa
taarifa ya usalama katika Mkoa wetu wa Iringa hususani katika Jimbo la
Kalenga katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kalenga
na usalama wa siku ya uchaguzi wenyewe.Ili iwe rahisi kueleweka taarifa
hii nitaitoa kwa kifupi sana kwa kuigawa katika maeneo matatu.
Eneo la
kwanza ni juu ya wapi tunataka tupafikie ( Where we want to go ), eneo
la pili ni lile la wapi tulipo ( Where are we? ) na eneo la tatu ni
jinsi gani tutafika huko ( How do we get there ). Tuanze na wapi
tunataka tupafikie. Sisi Polisi Mkoa wa Iringa tunataka
wananchi wa Kalenga wapinge kura kwa amani na utulivu mkubwa
siku ya jumapili tarehe 16/3/2014. Hii ndio dila yetu na
tutahakikisha tunafika hapo.
Kuhusu wapi tulipo sasa, naomba niwaelezeni kwa ufupi
sana matukio ya kijinai kuanzia tarehe 19/02/14 mpaka leo.
Ndugu zangu, kuanzia tarehe hiyo mpaka tarehe 2/03/2014
takribani wiki mbili hakukuwa na tukio lolote la uvunjifu wa
amani lililokuwa limepokelewa katika vituo vyetu vya Polisi.
Hali ilianza kubadilika tarehe 3/3/2014 ambapo baadhi ya
waandishi walifika ofisi kwangu na kunieleza kuwa kumetoka
kwenye mkutano wa CHADEMA ambapo wameelezwa na chama hicho
kuwa usiku wa siku hiyo walimkamata mtu mmoja kwa kosa la
kujaribu kuchoma moto nyumba waliokuwa wakiishi wafuasi wao
katika kijiji cha WASA. Waandishi hao walinitaka nithibitishe
kutendeka kwa kosa hilo na walieleza kuwa wameelezwa kuwa
bado halijaripotiwa kituoni. Mimi nilikataa kusema lolote kuhusu
hilo kwani lilikuwa bado halijaripotiwa Polisi. Tarehe
4/03/2014 nilifuatwa tena na baadhi ya waandishi na kunieleza
kuwa siku hiyo waliitwa na CCM na kuelezwa kuwa siku ya
tarehe 27/2/2014 walitegewa misumari katika kijiji cha WASA ili
mabasi yaliyokuwa yamebeba wafuasi wao yaweze kutobolewa
magurudumu yake, pia nao walisema tukio hilo halijaripotiwa
Polisi. Mimi nilikataa kulizungumzia swala hilo.
Ndugu wanahabari, vitendo vilivyofanywa na vyama hivyo
vililenga kuanzisha propaganda za kisiasa kwa kutumia uhalifu
kwa kupitia vyombo vya habari. Sisi Polisi tulibaini hali
hiyo na ndiyo sababu tuliamua kuwa kimya na nyinyi wenzetu
kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu pia mlikaa kimya.
Kuanzia hapo vyama vilianzisha mashindano ya kuripoti kesi
zao Polisi. Leo hii vyama hivyo vimeripoti kesi ishirini na
moja ambazo zilisababisha kukamatwa kwa wafuasi (19) wa vyama hivyo
viwili.
Ndugu waandishi, kati ya kesi hizo ishirini na moja, kesi kumi
na tisa (19) zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja kwa binadamu
ama mali, kesi hizo ni zile ndogondogo sana, kama vile kuchana mabango,
kuteremsha bendera, kuchana vipeperushi, kutukanana n.k. kesi tatu
zilikuwa zile zenye madhara kwa binadamu na mali ambazo ni kupigana
hadharani, kujeruhi na kuharibu mali. Kati ya kesi ishirini na moja
(21), kesi kumi upelelezi wake umekamilika na majalada yake yamefikishwa
kwa mwanasheria wa serikali.
Ndugu waandishi, katika kesi hizo Polisi tumeibaini mengi mfano
CHADEMA kilikuwa kikitoa malamiko kuwa tumeacha kumkamata ndugu hassan
mtenga mtuhumiwa wa kesi moja iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake. Shutuma
hizo hazina msingi kwani kesi iliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo haikuwa
ya jinai bali ya madai na tuliwajulisha hivyo. Nia ya kufanya hivyo
ilikuwa kuifanya jamii iamini kuwa Polisi ni dhaifu na wenye kuonyesha
upendeleo katika kushughulikia kesi za uchaguzi. Nashukuru Polisi
tulikuwa watulivu, hatukujibu na jamii imetuelewa sana.
Ndugu waandishi, sijui mlijulishwa na nani kwamba Padri mmoja
alifungwa kamba na alipingwa na kuburuzwa. Nanyi bila ya kuthibitisha
kwetu mkaandika habari hiyo. Tuwaeleze kuwa mtu huyo ni miongoni mwa
watuhumiwa tuliowakamata katika moja ya makosa yaliyotendeka, tulimhoji,
aliandikwa maelezo yake na alipewa dhamana. Hata siku moja hajawahi
kutoa taarifa Polisi juu ya matukio aliyotendewa. Nia ya kutangaza
taarifa hiyo ni kuzua hofu kwa wananchi na kutaka kuchochea chuki kwa
wafuasi wa dhehebu lake na wale wa dini yake.
Ndugu waandishi, pamoja na matukio hayo polisi tumekuwa
tukipokea taarifa za vitisho vya kuwepo kwa watu mbalimbali kutoka kwa
vyama vyote walioingizwa mkoani humu kwa nia ya kutenda vitendo vya
uvunjifu wa amani. Aidha, tumewasikia viongozi wa vyama wakitamba
kuingiza maelfu ya watu mkoani mwetu. Kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo
Arusha, Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura.
Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa, kila kituo
cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika
uchaguzi huo na hao ndio wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa
uchaguzi ni askari wa Jeshi la Polisi. Kufuatia hali hiyo mambo
yafuatayo yanasisistizwa sana.
1. Hatutaki
kuona walinzi wa chama chochote katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la
kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la JESHI LA POLISI.
2. Hatutaki kuona watu wasiokuwa na shughuli maalumu wanapitapita katika maeneo ya kupigia kura.
3. Siku ya uchaguzi si siku ya kampeni. Hatutaki kuona helikopita za vyama vyote zenye kuashiria kufanya kampeni.
Nawaasa
watu wote hasa wale waliotoka nje ya Iringa, sisi huku Iringa tunapenda
sana amani kuliko kitu chochote kile hivyo ikiwa wameletwa kama MAJESHI
YA KUKODIWA ili kuharibu amani ya Kalenga kama walivyozoea kufanya huko
walikotoka, Sisi Polisi na wana Kalenga tupo imara, tumejipanga vizuri
kukabiliana nao.
Aidha,
napenda kuwatoa hofu wana kalenga, wasiwe na wasiwasi kabisa, sisi
Polisi Iringa tupo imara na tumejipanga vizuri katika kuwalinda
kikamilifu. Nawaomba wajitokeze kwa wingi sana siku ya kupiga kura na
wapige kura zao kwa uhuru kabisa.
Ndugu
waandishi, nawashukuru sana kwa jinsi mlivyofanya kazi zenu kwa ueledi
mkubwa. Hata siku moja hatujawahi kusikia ama kusoma habari za uchochezi
kwa kushabikia chama chochote kile.
AHSANTENI SANA.
No comments:
Post a Comment