Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
AMA kweli kwenye msafara wa mamba kenge
hawakosekani. Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi Extra Bongo Next Level
'Kamarade' 'wazee wa Kimbembe' Ally Choki alijikuta akimwaga machozi baada ya
watu wanaodhaniwa kuwa vibaka kujipenyeza wakati wa uzinduzi wa albamu ya
'Mtenda Akitendewa' Februari 22 mwaka huu na kumuibia saa ya silva yenye
thamani ya dola 300 sawa na sh.500,000.
Ally Choki, pichani.
Extra Bongo ilizindua albamu hiyo ndani ya
Ukumbi wa Dar Live Mbagala jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya
mashabiki na wadau wa muziki wa dansi ambapo Choki aliingia ukumbini akiwa
ndani ya gari la kubeba wagonjwa 'Ambulance' na kulakiwa juu kwa juu.
Choki, alieleza, tukio la kuibiwa
lilimkuta wakati akishuka kwenye ambulance ambapo ndani ya kundi la mashabiki
waliompokea kulikuwepo na vibaka waliofanikwa kumvua saa hiyo pasipo yeye
kujitambua. "Kwa kweli saa yangu inaniuma sana nililetewa zawadi na rafiki
yangu kutoka Qatar lakini ndo hivyo vibaka wameniingiza mjini alisema Choki kwa
masikitiko na kuongeza.
"Wakati nimepanda jukwaani ndiyo
nikashtukia nimelambwa saa, bahati nzuri simu na vitu vyangu vingine vya
thamani nilikuwa nimeviacha kwa mlinzi wangu vinginevyo hali maumivu yangekuwa
makali zaidi ya hivi.
Tukio la Choki kuibiwa linakumbusha tukio
jingine lililowahi kutokea miaka kadhaa nyuma kwa aliyekuwa rapa wa bendi ya
Tanzania One Theatre (TOT) Papii Kocha 'Mtoto wa Mfalme' kuporwa cheni na
vibaka akiwa jukwaani wakati wa uzinduzi wa moja ya albamu za bendi hiyo katika
viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Aidha Choki alisema atatoa zawadi ya
sh.300,000 kwa mtu yoyote atakayeweza kufanikisha kupatikana kwa saa hiyo huku
akitaka aliyeiba kumrejeshea kiroho safi na atampatia kiasi hicho cha fedha
pasipo kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
"Nimeamua kutoa zawadi kwa atakayewezesha
niipate saa yangu au kwa aliyechukua kuirudisha kwangu, hii ni sababu nilikuwa
naipenda sana alieleza.
No comments:
Post a Comment