https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, March 18, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Yanga hii imevurugwa?

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam 
YANGA acheni masihara na serikali. Sio kila mnalolijadili nyie na kulihitaji, basi ni zuri na linastahili kuchukuliwa kama msimamo wa Watanzania wote. Wakati mwingine mambo yanayofikiwa kwenye klabu hii kongwe yanachekesha na kushangaza pia!
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, pichani.
Katika kuliangalia hili, naukumbuka wimbo wa dada mmoja wa kizazi kipya aliposema ‘Nimevurugwa’. Mwanzo sikumuelewa, lakini sasa namuelewa, hasa baada ya kutafakari kwa kina mashairi yake na jinsi jamii yetu tunavyoishi kwa kuvurugwa vurugwa.
Hili ‘Siwezi Kuvumilia’. Ni baada ya kikundi cha watu wachache, Yanga kuipa serikali siku tano iwape majibu, kabla ya kuamua kufanya maandamano makubwa jana Jumatatu kushinikiza wapewe eneo la heka 11 zilizopo Jangwani, jijini Dar es Salaam. Kauli hiyo tata ilitolewa na anayejiita ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali. 
Mbaya zaidi, kauli yake iliungwa mkono baada ya kuipata barua ya kubariki msimamo huo kutoka kwa Katibu Mkuu wao Benno Njovu. La kushangaza zaidi, Akilimali na wenzake walijigamba kuwa uamuzi huo umetoka juu, yani chini ya Mwenyekiti wao Yusuph Manji.
Ni kweli, maana kitendo cha Katibu Mkuu kulisapoti inamaanisha kuwa wameafiki jambo hilo. Hapa inashangaza kidogo! Yanga hii ina sauti gani kiasi cha kufikia kuipa amri nzito serikali? Naheshimu ukongwe wao katika nyanja ya soka, ila si kitendo cha kutaka kuvuruga amani ya Taifa letu. 

Yanga imeanzishwa  mwaka 1935. Mwaka mmoja baadaye ilianzishwa Simba SC. Hizi zote ni timu kongwe. Zimekusanya wanachama wengi na mashabiki kila kona ya Tanzania. Lakini si sababu ya kuwapa kiburi cha kuishurutisha serikali kuchukua uamuzi kwa faida zao.
Sawa ni maendeleo, lakini niliamini klabu hii ingemtumia mwanasheria wao kufuatilia baada ya kuiwasilisha barua ya maombi kwa Manispaa ya Ilala, chini ya Meya Jerry Silaa.
Wanataka kuandamana kisa ombi lao limechelewa, vipi Simba nao waandamane? Vipi Coastal Union nao waitishe maandamano. Hizi zote ni klabu za Tanzania, hivyo zina haki sawa. Kwa kutumia busara tu, Yanga wasingepaswa kujipa mamlaka ya juu zaidi.
Ndio inawezekana viongozi wengi ni wanachama au washabiki wao. Lakini tukiamua kuchukua uamuzi kwasababu ya itikadi zetu, hatuwezi kuendelea. Hata Bunge lisingeweza kujiendesha.
Baraza la Mawaziri lisingekuwa na mashiko. Serikali inayumbishwa na vyama vya siasa, kumbe hata hizi klabu zinazopaswa kutupa burudani nazo zinataka kutupa mashaka! Au wanataka mabomu ya machozi?
Na watakaokubali kuandamana watakuwa na moyo wa chuma. Kwa rasilimali watu na rasilimali fedha za Yanga, wangeweza kuonyesha jeuri ya fedha kwa kuwahamisha watu waliokuwa upande wa juu na sio kulalamikia kutaka bonde linalozuiwa na serikali.
Hivi viongozi wa Yanga wanawaza kwa kutumia akili au matumbo yao? Nisiendelee, ila kiukweli siwezi kuvumilia na kuna kila sababu ya kuliangalia kwa kina. Ikiwezekana maandamano yapigwe marufuku na ombi lao litupiliwe mbali pia. Hapa ushabiki kando.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...