Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF),
limesema jezi mpya zilizotumiwa na Taifa Stars kwenye mechi yake ya kirafiki
dhidi ya Namibia, ni msaada wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambao wameingia
mkataba na Kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, kusaidia nchi zisizojiweza
kiuchumi.
Kwa mara ya kwanza Stars ilivaa jezi
hizo katika mechi hiyo iliyochezwa jijini Windhoek, Namibia na kumalizika kwa
matokeo ya sare ya bao 1-1, ikiwa ni mechi ya kirafiki iliyoko kwenye kalenda
ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema si ajabu kwa Stars kuwa
na jezi mbili tofauti, huku akidai huo ni utaratibu wa kawaida tu.
Wambura alisema CAF wana utaratibu wa
kusaidia vifaa vya michezo kwa nchi wanachama wake, hivyo jezi walizovaa Stars
nchini humo ni mfano wa zile zitakazotolewa na CAF.
“CAF wameingia mkataba na Kampuni ya
Adidas kusaidia jezi nchi zisizokuwa na uchumi mzuri, hivyo Tanzania ni
miongoni mwa nchi zilizoingizwa kwenye utaratibu huo.
“Stars ilianza kuzitumia jezi hizo
katika mechi dhidi ya Namibia, hivyo wadau wa michezo wafahamu hilo na zitakuwa
zikitumika pamoja na zile za zamani,” alisema.
Stars ilirejea juzi saa 1 jioni
ikitokea nchini humo, ilikokwenda kucheza mechi hiyo, kama nchi nyingine
zilivyoumana katika mechi zao.
No comments:
Post a Comment