Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
YOYOTE anayeza kuinua kinywa chake kuwalaumu wachezaji wa
timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, huyo atakuwa na moyo wa chuma kupita
kiasi.
Ni kwasababu timu hiyo imekuwa ikijiendesha kwa kubangaiza
ufundi na namna ya kulinda vipaji vyao vya mchezo wa soka.
Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakishangilia moja ya mechi zao uwanjani.
Inashangaza kidogo, kunakuwaje na timu ya Taifa ya wanawake
hali ya kuwa hakuna ligi yoyote imara inayohusisha jinsia hiyo?
Hata hawa wachezaji wanachaguliwa kwa mtindo gani? Hawa
makocha wa Twiga Stars wanazingatia vigezo gani kuwapata mabinti hawa?
Hivi hawa mabinti katika maisha ya soka wanatarajia waje
kuishi kwa mtindo gani? Hivi soka kwao ni kujiburudisha au wanahitaji
kunufaishwa kwa wao kujiingiza kwenye mpira wa miguu?
Katika kujiuliza maswali yote hayo, utapata jibu kuwa
Tanzania haina malengo ya kuendeleza soka la wanawake, hivyo hata kwa hawa
vijana waliopo wanaocheza wanajitahidi tu.
Nimejikuta nikianza hivi; baada ya Twiga Stars, kuondoshwa
katika mchujo wa kuwania kufuzu michuano ya Kimataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC),
baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na timu ya Zambia ‘Shepolopolo’.
Mechi hiyo iliyokuwa na msisimko wa aina yake ilipigwa Ijumaa
ya Februari 28, katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Ikumbukwe kuwa, Twiga pia ilishawahi kufungwa bao 2-1 nchini
Zambia katika mchezo wa kwanza, hivyo kwa matokeo hayo Twiga Stars itakuwa
imeondoshwa kwa ujumla wa bao 3-2.
Ni tofauti ya bao moja tu. Kama hivi ndivyo, hakika vijana
hawa wanahitaji pongezi kubwa. Ndio, maana wametumia nguvu kubwa kulitangaza
Taifa, ambalo lenyewe haliwatangazi.
Tangu zamani tumekosa utaratibu wa kuijenga Twiga, ili iwe
imara ndani na nje ya nchi. Hatuijengi kwasababu hakuna mashindano makubwa kwa
ajili yao.
Tumeweka nguvu zaidi kwa soka la wanaume. Akina Mrisho
Ngassa, Juma Kaseja, Athuman Idd, Mbwana Samatta, Haruna Chanongo na wengineo
wanaogelea katika pesa, vipi hawa wenzao.
Vipi hawa akina Shelida Boniface, Fatuma Mustafa, Sofia
Mwasikili, Asha Rashid, Fatuma Omary, Amina Ali na wenzao nini faida ya soka
lao?
Hawa utagundua wanatumia nguvu kubwa bila kujua nini hatima
ya maisha yao. Ni kama vile wanaua mende kwa nyundo.
Wanavuja jasho bila mpango. Ni kutokana na hilo, nadiriki
kusema kwa kufungwa kwa idadi ndogo ya mabao na Zambia, hakika wamejitahidi.
Shirikisho la Soka nchini (TFF), wanapaswa kubuni mbinu nzuri
kwa ajili ya soka la wanawake. Liweke mikakati sit u ya kuwa na ligi ya kutoa
wanawake wa kuichezea timu za Taifa, ila ile itakayowapatia mwangaza wa
kimaisha wasichana kwa kupitia mpira wa miguu.
Tuone akina Mwasikili wanaishi vizuri hata kabla ya kukaa
kambini kwa siku tatu kwenye michuano ya Kimataifa, maana si njia nzuri.
Kuwa na ligi bora, itakayoshirikisha timu mbalimbali za
Tanzania, kutaongeza mvuto na hamasa kwa mabinti wengi, hivyo kuwapatia nafasi
nzuri ya kutafuta maisha ya soka nje ya Tanzania.
Hakuna haja ya kusubiri mechi za Kimataifa ndio wanaitwa
mabinti wachache, tena bila utaratibu mzuri wa kuwapata, maana hakuna
mashindano.
Hivi kweli unawezaje kuwa na timu ya Taifa, hali ya kuwa
hakuna ligi wala mashindano makubwa. Wachezaji wachache waliojulikana kamwe,
haiwezi kuwa mbeleko ya kuwavutia mabinti waliozagaa kona mbalimbali za nchi
yetu, maana hawajui faida watakayoipata.
Ndio maana nasema, huu ni wakati wa TFF kulifanyia kazi jambo
hili, maana kinyume cha hapo soka la wanawake haliwezi kusonga mbele. Haliwezi
kuwa ajira kwa watoto wa kike, hivyo itakuwa sawa pia kwa wazazi kuwagomea
mabinti wao kushiriki mchezo huo, ukizingatia kuwa miaka nenda rudi hauna faida
kwao.
Hauwezi kuvuna bila kupanda. Tupande sasa kwa kuweka mifumo
imara ya soka la wanawake. Tuweke mikakati ya kuvutia wadau na hatimae kuwa na
ligi nzuri, jambo linaloweza kuzalisha Stars imara.
Mungu ibariki Tanzania.
+255712053949
No comments:
Post a Comment